ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 15, 2014

Mbunge ataka waliojenga mabondeni wasaidiwe

Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Naomi Kaihula (pichani), amesema tatizo la wakazi wa mabondeni linatatulika endapo serikali itaweka mikakati mizuri ya miundombinu katika maeneo hayo.
Kaihula alisema kuwaondoa wakazi hao kwa ajili ya tahadhari ya mafuriko ni jambo zuri, lakini kwa kuwa wakazi hao wanaishi kihalali katika maeneo hayo, wanatakiwa kuandaliwa eneo mbadala.
Akizungumza na wakazi wa Jangawani jijini Dar es Salaam juzi, Kaihula alisema wakati wakazi hao wanajenga nyumba zao katika eneo hilo serikali ilikuwa inawaangalia, lakini haikuchukua hatua zozote, lakini sasa ndipo imeona kuwa ni tatizo. 


Aliongeza kuwa wapo watu ambao maisha yao yote wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo, hivyo kuanza kuwaondoa bila kuwaandalia maeneo ya uhakika ni kuwanyanyasa.
Alisema ili kuwasaidia wakazi hao, serikali inapaswa kujenga nyumba za kisasa na kuweka miundombinu imara katika maeneo hayo yanayoweza kuhimili mafuriko na kuwapa kipaumbele wakazi hao kuishi katika nyumba hizo badala ya kuwafukuza kama inavyofanya hivi sasa.
“Suala la serikali kuwaondoa wakazi wa mabondeni kwa ajili ya tahadhari ya mafuriko ni jema, lakini ni lazima ikumbuke kuwa wakati wakazi hao wanajenga nyumba zao katika maeneo hayo ilikuwa inawaona na wapo baadhi ya wakazi ambao wamezaliwa hapo na wamezeekea hapo, unapowaondoa bila kuwaandalia eneo mbadala ni kuwaonea,” alisema.

No comments: