Advertisements

Sunday, December 21, 2014

Mwelekeo mpya; Ukawa wasema serikali ya mseto inanukia 2015

Dar es Salaam. Matokeo ya awali ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi kote hivi karibuni yanaonyesha kuwa wananchi wamebadilisha mitazamo yao dhidi ya vyama vya siasa na hivyo kutoa picha mpya kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Uchaguzi huo uligubikwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo nchini kiasi cha Serikali kuwaondoa kazini wakurugenzi wa halmashauri tano kwa kushindwa kuusimamia vyema, pia umevipa vyama na Serikali nafasi ya kujitafakari upya.
Kwa upande mmoja, uchaguzi huo umewapa nguvu wapinzani kwa kuongeza idadi ya viti, lakini umeivuta nyuma CCM baada ya kupoteza zaidi ya nafasi 2,600 za uenyekiti wa vijiji na mitaa ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2009 ilipopata jumla ya viti 12, 042.
Vyama vya upinzani vimefanikiwa kuongeza kibindoni viti 1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2009 ambapo vilipata nafasi 1,230 za wenyeviti wa mitaa na vijiji.
Matokeo haya yametoa mwelekeo mpya kwa vyama vya siasa nchini, wapinzani wakiamini huo ndiyo ufunguo wao kuelekea Ikulu mwakani, CCM wakiamini kuwa huko ni kujikwaa tu na wataendelea kubaki Ikulu mwakani kwani bado wanakubalika kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza mjini Dodoma hivi karibuni, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda alisema kwamba wakati CCM ikifanikiwa kupata ushindi wa jumla wa mitaa na vijiji 9,406, vyama vya upinzani vimepata nafasi 3,211.
Katika matokeo hayo CCM kimepata vijiji 7,290 kikifuatiwa na Chadema yenye vijiji 1,248. CUF imeshika nafasi ya tatu kwa kuwa na vijiji 946, ikifuatiwa na UDP yenye vijiji vinne na TLP na NLD vyenye viwili kila kimoja.
Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM kimechukua jumla ya mitaa 2,116. vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni Chadema (753), CUF (235), ACT (9), NCCR - Mageuzi (8) wakati vyama vya TLP, UMD, UDP na NRA vimepata mtaa mmoja kila kimoja.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo nchini, wananchi watapiga kura leo baada ya kushindwa kufanya hivyo Desemba 14 kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema matokeo hayo ni dalili kuwa CCM itafanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani.
Ingawa waziri huyo alikiri kuwa vyama vya upinzani vimechukua maeneo mengi kuliko uchaguzi uliopita, alisema vyombo vya habari vinatumika kupotosha hali halisi na kuifanya CCM kuonekana kuwa imepoteza viti vingi kuliko uhalisia.
Matokeo hayo yanaonyesha CCM imepoteza viti zaidi katika mikoa wa Dodoma, Lindi, Mtwara, Iringa, Arusha, Singida na katika baadhi ya majimbo ya Dar es Salaam.
Nape akiri makosa
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye naye alisema makosa yanayofanywa kwenye kura za maoni katika chama hicho ndiyo yanayokigharimu na badala yake kupeleka furaha kwa wapinzani.
Alisema katika baadhi ya maeneo wananchi walipiga kura za hasira ili kuiadhibu CCM baada ya majina ya watu waliowataka kugombea uongozi kutopitishwa na chama hicho.
“Tunajua kwamba kuna maeneo mengi ambayo wapinzani wameshinda. Ukiangalia CCM tulifanya makosa katika kumweka mgombea, hivyo kusababisha hasira ambazo kwa kweli zimewafurahisha wapinzani lakini sisi zimetugharimu,” alisema.
Serikali ya mseto yanukia
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alisema wananchi wameamua kuvipigia kura vyama vinavyoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya kubaini kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi ya kuwapatia maisha bora.
“Hasira ya wananchi dhidi ya CCM imetokana na mchanganyiko wa mambo mengi, wananchi wamechoka kupewa ahadi zisizotekelezeka kuhusu kupewa maisha bora, kupambana na ufisadi na kuchakachuliwa kwa maoni kwenye Rasimu ya katiba,” alisema Mnyika.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ubungo alisema lengo la Ukawa ni kuingia Ikulu mwaka 2015 na kwamba iwapo wananchi wataendelea na imani waliyoionyesha kwenye uchaguzi huo, upinzani wanatarajia kupata viti vingi zaidi ya CCM bungeni.
“Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Waziri Mkuu anatoka kwenye chama chenye wabunge wengi, haiwezekani Waziri Mkuu na Rais watoke vyama tofauti, CCM italazimika kuunda serikali ya mseto,” alisema.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha kuwa wananchi hawapotezi imani na Ukawa, tayari Chadema kwa upande wao wameandaa mwongozo na mafunzo maalumu kwa viongozi wa mitaa waliochaguliwa.
Wakati Ukawa wakishangilia idadi kubwa ya viti waliyopata kwenye uchaguzi huo, baadhi ya wananchi wanaonyesha wasiwasi kuhusu viongozi waliochaguliwa kwa madai kwamba baadhi yao hawana sifa ila walipigiwa kura ya ndiyo ili kuiadhibu CCM.
Akizungumzia suala hilo, Mnyika alisema sifa ya kwanza ya kiongozi ni kuaminiwa na wananchi waliomchagua na kwamba kabla ya kupata nafasi ya kugombea walipitishwa kwenye mchujo wa ndani ya chama.
“Sifa nyingine ya uongozi ni uadilifu na ushirikishaji wananchi kwenye uamuzi ndiyo maana tunaamini wataongoza vizuri, mafunzo tuliyowaandalia ni nyongeza tu,” alisema.
Profesa Safari
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari anasema Ukawa inaweza kuingia Ikulu kwa njia rahisi kupitia Uchaguzi Mkuu ujao endapo mambo matatu yatatekelezeka kwa sasa.
Profesa Safari alitaja mambo hayo kuwa ni kukamilika kwa maboresho ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura, kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi na kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto ya kuwafikia wananchi wengi vijijini.
Alisema kuhusu Daftari la Wapigakura, idadi kubwa ya vijana na wafuasi wa Ukawa kwa sasa hawana fursa kwani hawana sifa za kupiga kura hivyo kukamilika kwa zoezi hilo itakuwa kitanzi kwa CCM.
“Matokeo ya uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa yanaonyesha kuwa kura za wapinzani zitaongezeka maradufu lakini tutafanikiwa endapo daftari litawafikia vijana wote wenye sifa kwa asimilia mia moja,” alisema na kuongeza:
“Jambo la pili, ni kufanikisha kuwafikia wananchi wengi vijijini, kwa sasa tumeshasambaza pikipiki zaidi ya 2,000 katika vijiji mbalimbali katika kanda kumi tulizofikia.”
Alisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kupitia chama chake amefanikiwa kuwafikia wananchi wengi kutokana na ziara zake kote mikoani mpaka vijijini, ambako ndiko waliko wapigakura wanaohitaji mabadiliko.
Profesa Safari alitaja kikwazo kingine kuwa ni uwepo wa Tume ya Uchaguzi isiyokuwa huru tangu mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini.
“Tume ya Uchaguzi tumekuwa tukiipigia kelele mara nyingi ifanyiwe maboresho lakini hakuna hatua zozote. Tunahitaji kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo inaweza kusahihisha dosari zilizojitokeza kwenye chaguzi zilizopita,” alisema Profesa Safari.
Katika hatua nyingine, Profesa Safari alisema matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamechagizwa zaidi na sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ambalo liliibuliwa na Gazeti la The Citizen.
Profesa Lipumba
Naye Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema endapo umoja huo ungefanikiwa kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi huo, CCM ingeanguka vibaya.
Profesa Lipumba alisema katika maeneo mengi waliyoshindwa na CCM, kura zilionekana kutofautiana kwa idadi ndogo hali ambayo wangeweza kushinda endapo wangeunganisha kura zao kwa mgombea mmoja.
Akitoa mfano, Profesa Lipumba alitaja maeneo waliyofanikiwa kuunganisha nguvu ambayo ni Kimara, Kigamboni, Ubungo na Kijitonyama yaliyopo Dar es Salaam, Ukawa ilishinda.
“CCM wangeanguka vibaya, lakini ni changamoto iliyojitokeza kwa wawakilishi wetu kutoelewana, kutofahamu juu ya azimio letu kama Ukawa,” alisema na kuongeza:
“Kwa hivyo tunaomba imani ya Watanzania iendelee kuwapo, tutafanya tathmini ya kina ili kuepuka athari hiyo mwakani.”
Kibamba
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema kiburi cha baadhi ya watendaji ndicho kilichoifikisha CCM mahali ilipo hivi sasa na kwamba endapo Rais Kikwete hatawachukulia hatua viongozi hao, huenda hali ikawa mbaya zaidi kwenye uchaguzi ujao.
Pia, alisema CCM imefanya vibaya kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na Serikali kusita kuwachukuliwa hatua viongozi waliotajwa kwenye sakata la uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu.
“Mchakato wa Katiba Mpya utazidi kuathiri uchaguzi ujao, kwa sababu wapo baadhi ya watendaji wa CCM wanadhani kura ya maoni ipigwe baada ya uchaguzi mkuu,” alisema.
Hata hivyo, Kibamba alisema CCM inapaswa kumshukuru Katiba Mkuu wa chama hicho, Kinana ambaye alizunguka nchi nzima akizungumza na wananchi.
Wasomi
Mdhahiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Danford Kitwana alisema CCM haina jambo jipya la kufanya kwa wananchi ili iendelee kukaa madarakani zaidi ya kutekeleza ahadi ilizotoa.
Alisema iwapo chama hicho hakitafanya hivyo huenda hali ikawa mbaya zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwani inaweza kupata kura chache zaidi huku za vyama vya upinzani zikipanda.
“Hata hivyo muda uliobaki chochote kinaweza kutokea na kubadilisha hali ya hewa,” alisema.
Kwa upande wake, Dk Benson Bana kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema Watanzania wameichoka CCM kwa sasa.
“Vijana wengi wanaamini kuwa Chadema ndiyo inaweza kuwa tumaini na mbadala wao kwa CCM, walijipanga na matukio ya ufisadi yakawabeba ndiyo sababu ya kutoa ushindani kwenye Serikali za Mitaa,” alisema Dk Bana.
Awali, Dk Bana alisema kuwa Ukawa wana uwezo wa kuendesha Serikali bila hofu yoyote ya kuyumbishwa kutokana na msingi wa Katiba, sheria na kanuni zinazoendesha Taifa.
“Nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na Ukawa siyo muungano wa kwanza kujaribu hatua hiyo, Kenya upinzani wameingia kwa muundo kama huo na nchi inaongozwa,” alisema.
“Wangeongeza idadi kubwa ya wafuasi kwa sababu Watanzania wamechoshwa na CCM na wanatamani kuona dhamana ya kura yao kupitia nguvu ya chama kimoja,” alisema.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama alisema hakuna tafiti zinazoweza kuonyesha nafasi ya Ukawa kuchukua Serikali, lakini wameonyesha juhudi za kuleta ushindani.
“Ukawa wamethubutu, wamejaribu hivyo tunatakiwa kusubiri sanduku la kura kwa sababu wananchi wenyewe ndiyo watakuwa na majibu kama watakuwa tayari kwa pamoja kuleta mabadiliko ya kimfumo,” alisema Profesa Mlama.
Matokeo ya CCM yashuka
Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2004 yanaonyesha kuwa CCM ilipata asilimia 88.4, huku vyama vya upinzani vikiambulia asilimia 11.6.
Mwaka 2009, CCM kilivuna kura nyingi zaidi kwa kupata asilimia 93.70 baada ya kujiongezea asilimia 5.3 kutoka kura za awali. Hata hivyo, mambo hayakuwa mazuri kwa vyama vya upinzani kwani vilijikuta vikipata asilimia 6.30.
Kwa upande mwingine takwimu za matokeo ya CCM katika chaguzi mbalimbali zinaonyesha kushuka tangu mwaka 2005 wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani.
Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kitaifa, alipata asilimia 80.28 dhidi ya vyama vya upinzani vilivyokuwa vimepata asilimia 19.72.
Uchaguzi uliofuata CCM iliporomoko kwenye kiti cha urais hadi asilimia 61.17 huku vyama vya upinzani kwa pamoja vikiambulia asilimia 38.30.
Ripoti ya Twaweza
Ripoti ya utafiti ya Taasisi ya Twaweza kuhusu maoni na matakwa ya wananchi kuhusu uongozi wa kisiasa iliyotolewa Novemba mwaka huu, ilieleza kuwa kama Watanzania wangepiga kura mwaka huu CCM ingepata asilimia 54.
Kwa mujibu wa utafiti huo, imani ya wapenzi wa CCM juu ya wagombea wao watarajiwa inashuka kila mwaka. Mwaka 2012, Edward Lowassa alipata asilimia nane, 2013 (20) na 2014 (17).
Mizengo Pinda mwaka 2012 alipata 23, mwaka 2013 na 2014 alipata asilimia 14. John Magufuli mwaka 2012 alipata asilimia 8, 2013 (6) na 2014 asilimia tano.
MWANANCHI

No comments: