Advertisements

Friday, December 19, 2014

Mzee wa miaka 70 jela kwa kukata mti


Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imemhukumu Zuberi Lubengela (70) kutumikia kifungo cha miezi sita jela, kwa kosa la kukata mti aina mgunga wenye thamani ya Sh. 100,000, mali ya kanisa la TAG lililopo kijiji cha Kiganza.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, David Ngunyale, baada ya upande wa mashtaka kuiridhisha mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.

Hakimu Ngunyale alisema mahakama inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wazee wengine wenye tabia kama yake.

Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wawili mahakamani hapo ambao walithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alikata mti aina ya mgunga wenye thamani ya Sh. 100,000 mali ya kanisa la TAG kinyume cha sheria.

Hakimu huyo alisema mshtakiwa alingia kwenye shamba la kanisa hilo na kukata mti huo bila idhini ya mchungaji wa kanisa hilo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Alisema mshtakiwa ametiwa hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo na kabla ya kutoa hukumu alimtaka ajitetee.

Mshtakiwa huyo alijitetea kuwa, ana watoto tisa wanaomtegemea, wake wawili wanaomtegemea, hivyo anaomba mahakama imhurumie na impunguzie adhabu.

Hakimu Ngunyale alitupilia mbali utetezi huo na kusema mshtakiwa atakwenda gerezani miezisita ili akajifunze namna ya kuishi na jamii na akimaliza kifungo hicho atakuwa raia mwema.

Awali, akisoma hati ya mashtaka, Inspekta wa Polisi, Athumani Mshana, alidai kuwa, Mei 9 mwaka huu, saa 3 asubuhi, katika Kijiji cha Kiganza, wilaya ya Kigoma, mshtakiwa bila halali na kwa makusudi alikata mti aina mgunga wenye thamani ya Sh. 100,000 mali ya kanisa la TAG, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Watanzania ni lazima tujifunze jinsi ya kutunza mazingara yetu. Miti ni nchanzo cha hewa safi-climate change, mvua, chakula-matunda nakadhalika. Huyu jaji amefanya kitendo kizuri na ameonyesha mafano mzuri kwa majaji wengine na viongozi wa tanzania kwa kutunza mazingara.

Anonymous said...

Mtu anahukumiwa miezi sits wakati waliokula mabilioni Wako nje nchi hii! Na huyo Ni mzee jamani lo!

Anonymous said...

na bado mnaichagua ccm na na visomo vyenu vyote mlivyosoma na explosion zote mzizo pata kuwa huko majuu,mweeeeeeeeeeee mfyuuuuuuuuu.

akheri asiye soma kuliko waliosoma na kuwa huko majuu na bado kuwapigia makofi ma ccm mafisadi.