ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 3, 2014

Nchi nzima ina wajibu wa kudai fedha zetu za escrow

A Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la Mwaka l949 linasema: “Maandamano ni haki ya wananchi pale wanaposhindwa kupata haki zao kwa njia ya mazungumzo, vikao, majadiliano au kupiga kura.”
Maandamano hupeleka ujumbe dunia nzima hasa katika ulimwengu huu wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano.
Hili ni azimio la Umoja wa Mataifa (UN), ndiyo maana tunaona nchi nyingine duniani huwa zinafanya maandamano nchi nzima na polisi hawathubutu kuyazuia wala kuua raia kwa sababu ni haki yao kikatiba.
Suala la pesa za umma zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow limekuwa gumzo kubwa nchini kwa muda mrefu sasa.
Ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), na uchuguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwenye akaunti hiyo, umemalizwa na ripoti zimetolewa na sasa kinachobaki ni kuisoma na kufikia tamati kama pesa iliibwa ni nani anahusika?
Kwa vile suala hili limegusa utendaji wa viongozi wa ngazi za juu serikalini pamoja na wanasiasa wengine, linaonekana kusuasua katika kulitolea jawabu sahihi.
Wahenga walisema: “Wajinga ndio waliwao.” CCM imewafanya Watanzania ndio wajinga na ndio wanaoliwa, lakini nina imani muda si mrefu Watanzania wataamka usingizini na kuanza kuitetea nchi na mali zao.
Naandika hoja yangu bila hofu yoyote kwamba “sasa dawa pekee iliyobakia kwa Watanzania kudai haki zao, zikiwamo pesa za escrow ni wananchi kupaza sauti zao.”
Nasema hivi kwa kuwa maandamano ni haki ya kikatiba kwa wananchi kupata kile wanachotarajia.
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), nimeipitia kwa ufasaha na nimegundua kuwa wamepitia ukaguzi wa CAG na uchunguzi wa Takukuru kwa makini nao wakatoa ripoti yao na uthibitisho wa kutosha kuwa kuna Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Madini na Nishati pamoja na watendaji wengine serikalini wamehusika na upotevu wa pesa za escrow ama kwa kukusudia ama kwa kutojua, kitu ambacho kimeelezwa kuwa ni uzembe.
Kitu kinachonishangaza ni hili la baadhi ya wabunge wa CCM wasiotaka wahusika wawajibishwe ambao walionekana kupata msaada wa Spika wa Bunge.
Swali langu; kwanini tuwalinde wezi kwa akili zote, roho yote, nguvu zote, na uwezo wote?
Kama kuna chembe ya hofu ya Mungu ndani ya wabunge wa CCM na hata wale wa upinzani. Lazima watambue kwamba kumlinda mwizi ni dhambi kubwa mbele ya Mungu na mbele ya wananchi maskini Watanzania.
Katika amri 10 za Mungu, mojawapo inasema: “ Usiibe kwa sababu mwizi ni muuaji.” Wengi tunajiuliza kama wabunge wa CCM wanatetea waovu sasa tutumie njia gani kudai pesa zetu za umma zilizoliwa na wajanja wachache? Ndipo nikapendekeza kuwa ‘dawa’ pekee kudai pesa zetu za Escrow ni kufanya maandamano ya amani nchi nzima ili kupeleka ujumbe kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na kwa Watanzania wote na dunia nzima.
Kamati ya PAC chini ya Zitto Kabwe kwa kusaidiana na wabunge wa upinzani na wale wazalendo wa CCM, watoe tamko la kuhitimisha mjadala huu na kupeleka ujumbe kwa Rais kwamba “sasa tumechoka kuendelea kuwalinda wezi wa mali ya umma”.
Hata hivyo, nafikiria pia vyama vya siasa, kupitia jumuiya zao zote, vipaze sauti bila kukoma ili kupeleka ujumbe barani Afrika kwamba Tanzania mambo si shwari na dunia nzima itambue wizi huu unaowatesa Watanzania.
Tunaomba katika maandamano hayo ya amani vyombo vya ulinzi na usalama vilinde maandamano hayo bila kuanzisha vurugu na mwishowe maafa yasiyotegemewa.
Viongozi wa dini zote waitishe maombi, sala na kutoa mafundisho juu ya madhara ya wizi na ufisadi uliokatazwa na maandiko matakatifu. Mafundisho hayo yatolewe kwa ufasaha mkubwa ili waumini waweze kuyaelewa ili kuepusha makwazo.
Mafundisho yaonyeshe wazi jinsi Mwenyezi Mungu anavyochukia na kulaani wala rushwa kwa sababu wanapotosha haki ya wanyonge na maskini.
Hata hivyo, viongozi wa dini wakishauriana jinsi ya kutoa kilio hiki kwa pamoja na kupeleka ujumbe kwa Rais Kikwete, wananchi wa Tanzania, Bara la Afrika na dunia kwa jumla.
Nina imani polisi hawawezi kuharibu maandamano hayo kwa sababu kwanza itakuwa ni sala na ya pili ni ya amani na hata siku moja dini haziwezi kuwa kicheocheo cha fujo, machafuko na maafa
Waumini wa madhehebu ya dini yote nchini wanaunda kundi kubwa sana la wanajamii ya Watanzania, hivyo wanao wajibu wa kuonyesha kwamba wanakerwa na kuchukizwa na wizi wa fedha za umma.
Pia kuonyesha wizi ni dhambi na dhambi huzaa mauti ya mwili na roho.
Kwa kumalizia mada yangu, naomba niwashauri Watanzania wenzangu kwamba nchi yetu imefika mahali pabaya.
Baba wa Taifa letu linaloteseka, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitufundisha kitu kimoja kizuri, “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.” Basi kwa mantiki hii naomba Watanzania wote bila kujali imani yako, itikadi ya kisiasa, kabila, rangi, cheo, elimu na kipato chako tupaze sauti kwa pamoja kwamba wezi hawa wa fedha za umma sio tu wazirejeshe, lakini pia wachukuliwe hatua za kisheria. Wafilisiwe na wakae jela.
Watanzania simameni pamoja, inueni mioyo kwa Mungu pamoja, inameni vichwa vyenu pamoja, inukeni pamoja na mpaze sauti pamoja na Mungu wenu kama walivyofanya Waisraeli.
Kumbukeni njia pekee iliyobaki kudai pesa kwa sababu serikali ya CCM inaogopa maandamano kuliko kumwogopa Mungu na wananchi walioiweka madarakani.
Mungu Wabariki Watanzania.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

wenye nchi yao wameshachukua chao Tanzania ni shamba la bibi kila mwenye kuhisi anauwezo na nafasi ya kujitotea mipesa anajichotea na kuiwacha nchi kama maiti inasubiri kuzikwa tuu.

hali ya hewa hii itapita,kama sakala kibao zilizopita.

piga box lako walishe ndugu na wazazi wako bongo kwisha kazi usiumize kichwa wenye nchi wanajua wanacho kitenda katika nchi hii.