Leo katika mada yetu nazungumzia jinsi wapendanao wanavyotenganishwa na simu za mkononi huku kwenye upande wa ndoa ikisemwa watu wawili waliooana wanakuwa mwili mmoja.
Labda turudi katika imani mbalimbali, maandiko yanasema kuwa, mwanamke na mwanaume wanafunga ndoa na kuishi kama mke na mume, wanakuwa si wawili tena bali mwili mmoja!
MAANA YA WAWILI KUWA MWILI MMOJA
Ninavyojua mimi, maana ya neno hili la wawili wanakuwa mwili mmoja na si wawili tena lina maana kwamba, wanandoa wanatakiwa kuishi kwa umoja, furaha ya mke iwe pia ya mume, matatizo ya mume yawe pia ya mke.
Kama kuna kulala na njaa, iwe kwa wote. Kama kuna maumivu kwa maana ya mmoja kuugua, basi mwingine pia awe anaumwa kama mwenzake. Ndiyo maana halisi!
LAKINI SASA
Lakini cha ajabu sana, katika wanandoa, imeibuka tabia moja yenye kutia shaka sana! Vitu vingi wanandoa wanashirikiana kasoro kitu kimoja tu! Simu ya mkononi!
Ukikuta wanandoa wanashirikiana kwa simu za mkononi hao wamemshinda shetani! Yaani mke anaweza kushika simu ya mumewe akaingia kwenye meseji na kujisomea anazotaka na mume naye ikawa vivyo hivyo! Walio wengi, kwenye simu wanakuwa siyo mwili mmoja, bali wawili kama walivyokuwa kabla hawajafunga ndoa!
TATIZO LIKO WAPI?
Niliwahi kuzungumza na baadhi ya wanandoa wake kwa waume kuhusu simu zao na ushiriki wa wenza wao katika kuzitumia.
Nilibaini kwamba, wanandoa wengi, hawapendi simu zao kushikwa na wenza wao kwa sababu zina ‘vimeo’. Vimeo kwa maana ya namba za michepuko na meseji zao ambazo zikionwa lazima jambo moja litokee, kama si ndoa kuvunjika basi hata umwagaji wa damu hutokea!
SIKILIZA MANENO HAYA!
“Mimi na mwenzangu (awe mke au mume) tumekubaliana kabisa hakuna kushika simu ya mwenzako. Mimi simu ya mume wangu sishiki wala yeye hashiki ya kwangu.
“Unajua tabia ya kushikashika simu ya mwenzako kuna siku unaweza kukumbana na meseji za ajabuajabu halafu ikawa ugomvi mkubwa,” alisema mama K, mkazi wa Ubungo-Kibangu, Dar.
“Mimi na mke wangu baada ya kufunga ndoa tu, tuliwekeana utaratibu, kila mmoja asishike simu ya mwenzake! Kwa hiyo mimi ya kwake hata ikiita nimekaa nayo jirani sipokei na yeye pia,” alisema Salum Mohamed, mkazi wa Mabibo, Dar.
AKILI IKO WAPI?
Maamuzi ya wote hao ni mazuri sana, tena sana kwani yanadumisha amani na ndoa yenyewe. Nasema hivi kwa sababu ndoa za siku hizi zinavunjika sana.Lakini mimi katika tafakari yangu kichwani kama mwanadamu niliyepewa uelewa na Mungu napingana na busara inayotumika kwa wanandoa kuwekeana ukuta kwenye simu.
Kwa nini kuwe na ukuta? Kunafichwa nini kwenye simu mpaka mke asishike ya mumewe wala mume asishike ya mkewe? Hii siri inayolindwa hapa ni ipi kama kweli wakati wa kufunga ndoa ilikubaliwa kuwa wawili wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja?! Kama ni mwili mmoja tangu lini kichwa kikaikataa miguu?
JIONGEZE
Mimi naamini, anayeanza kuweka hii busara ana jambo zito analoficha. Maana kama meseji itaingia kwenye simu ya mwenza wako wewe ukasoma, ikawa ni ya mchepuko si iko wazi kwamba mwenzako si mwaminifu?! Sasa kuweka sheria hii ni sawa na kusema ‘endelea kuchepuka’ ila nisijue! Jiongeze mwanamke, jiongeze mwanaume!-GPL
No comments:
Post a Comment