Advertisements

Monday, December 8, 2014

Simba laini sana kwa Mtibwa

Nahodha wa zamani na Taifa Stars,Mecky Mexime ambae kwa sasa anakiongoza kikosi cha Mtibwa Sugar.

Simba imejikuta ikifunzwa soka na Mtibwa Sugar baada ya jana kukubali kichapo cha mabao 4-2 katika mchezo wa kirafiki uliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Kikosi A cha Simba kucheza kwenye uwanja huo tangu ujengwe miaka minne iliyopita.

Wenyeji Simba walifungua mlango wa mabao dakika 23 kiungo Said Ndemla alipokifungia Kikosi cha Kocha Mzambia Patrick Phiri bao kabla ya wageni Mtibwa Sugar kusawazisha dakika sita baadaye kupitia kwa mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi aliyeunganisha vema mpira wa krosi murua ya beki wa zamani wa Yanga, David Luhende.

Katika dakika ya sita ya kipindi cha pili, Mtibwa Sugar wanaonolewa na nahodha wao wa zamani na Taifa Stars, Mecky Mexime, walipata bao la pili kupitia kwa Mgosi pia amezifunga Simba na Yanga msimu huu katika mechi dhidi ya timu yake.


Mgosi amekuwa na bahati ya kufunga katika mechi anayocheza dhidi ya Simba, akifunga katika sare ya bao moja msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kabla ya kufunga pia katika mechi ya msimu huu wa ligi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao moja pia, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mgosi pia alifunga bao la kwanza la Mtibwa katika ushindi wa mabao 2-0 ambao Mtibwa iliupata dhidi ya Yanga kwenye mechi yao ya kwanza ya VPL msimu huu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Septemba 20, mwaka huu.

Bao la tatu la Mtibwa lilifungwa na mtokea benchi, Mohamed Ibrahim dakika 13 baada ya saa ya mchezo huo akiendeleza makali ya Mgosi aliyefunga mabao mawili kabla ya kumpisha.

Mshambualiaji hatari wa Mtibwa Sugar msimu huu, Ame Ally Amour mwenye mabao manne VPL kwa sasa, aliipatia timu yake bao la nne katika dakika ya 80.

Mabao yote manne ya Mtibwa yalitokana na mashambulizi yaliyoanzia nyuma huku wakatamiwa hao wa Manungu, Turiani, Km 100 kutoka mjini Morogoro wakicheza soka la kuvutia la pasi fupi fupi. Baada ya bao hilo, Simba walianza kulazimisha kuingia kwa nguvu ndani ya boksi la Mtibwa Sugar na kupata penalti ambayo Mfungaji Bora wa VPL msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe aliitia nyavuni akimpeleka ndiko siko kipa aliyefungwa mabao matatu katika mechi saba zilizopita za VPL msimu huu, Said Mohamed.

Penalti hiyo ilitolewa baada ya kiungo mtokea benchi Shaban Kisiga kuangushwa na mabeki wa Mtibwa Sugar ndani ya boksi.

Kabla ya mapumziko, kiungo tishio kwa Yanga, Ndemla aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Mrundi Pierre Kwizera.

Ilikuwa mechi ya pili kwa Kikosi cha Simba kujipima nguvu ndani ya wiki moja baada ya Ijumaa kutoka suluhu dhidi ya Timu ya The Express ya Ligi Kuu ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Vikosi vilikuwa;
Simba: Ivo Mapunda, William Lucian/ Nassoro Masoud, Issa Rashid, Abdulazizi Makame, Hassan Issihaka, Said Ndemla/ Pierre Kwizera, Awadh Juma, Abdallah Seseme, Amissi Tambwe, Ibrahim Hajibu/ Shaban Kisiga na Twaha Ibrahim/ Ramadhani Singano. Mtibwa: Said Mohamed, Hassan Mbande/ Hassan Kessy, David Luhende, Dickson Daudi, Ally Lundenga, Henry Joseph, Vicent Barnabas/ Ally Shomari Sharrif, Musa Nampaka, Abdallah Juma/ Ame Ally Amour, Ibrahim Jena na Mussa Mgosi/ Mohamed Ibrahim.
    
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: