ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 15, 2014

UKIFANYA HAYA, HAUSIGELI HATAKUCHUKULIA MUMEO-2

Uhali gani msomaji wangu wa kolamu hii, nakukaribisha tena kwenye uwanja wetu tuendelee kujadiliana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Wiki iliyopita tulianza kujadili sababu zinazoweza kumfanya mumeo akatoka na hausigeli.
Leo tunaendelea na sababu ya tatu na mambo ya kuzingatia ili kuzuia tatizo hili.

3. KUKOSA UAMINIFU
Sababu nyingine inayosababisha wanaume kutoka na mahausigeli wao, ni kukosa uaminifu kwa wanaume wengi. Kutokana na utafiti mdogo nilioufanya, wanawake wengi wamesalitiwa kwa waume zao kutoka na mahausigeli kwa sababu ya kukosa uaminifu.
Kwamba mwanamke anajitahidi kufanya kila kitu kumfurahisha mumewe lakini kutokana na tamaa ya ngono, mwanaume huyo anashindwa kuridhika na kuanza kumtongoza hausigeli kisha kutembea naye.

MFANO HALISI
“Habari ndugu mshauri, naitwa Osana au mama Robert kutoka Ruvuma. Nimeona mada ya hausigeli kutembea na waume zetu. Ni kweli ubize unasababisha lakini kwa upande wangu, hausigeli hajawahi kumpikia mume wangu hata niumweje, hajawahi kumfulia hata nichokeje, chumba changu hajawahi kuingia na hajui hata kitanda kipoje. Bafuni kwangu ndiyo kabisa.

“Kazi yake ni kuosha vyombo na mezani navitoa mwenyewe lakini mume wangu alinivizia nimeenda msibani akamtongoza hausigeli wangu, alimkataa mpaka alilia. Akavizia usiku na kugonga mlango na kumwambia amfulie nguo usiku, alikataa na kumwambia kuwa mbona hajawahi kufua nguo zake? Mwisho alitimiza alichokuwa anakitaka.

“Hausigeli mwenyewe ni mdogo hata ungo hajavunja, alikuwa anasubiri matokeo ya darasa la saba. Hebu ona sasa, ni tabia mbaya ya mwanaume au mimi nina kosa gani? Naomba uuandike ujumbe huu gazetini.”

Huo ni ujumbe kutoka kwa msomaji wangu kama alivyojitambulisha mwenyewe. Hii yote inazidi kuipa nguvu sababu ya tatu kwamba wanaume wengine wanaendekeza ngono na kukosa uaminifu kwenye ndoa zao. Umeona jinsi msomaji hapo juu alivyojitahidi kutimiza wajibu wake lakini mumewe bado akatoka na hausigeli. Inasikitisha.

NINI CHA KUFANYA?
Baada ya kuona sababu zinazochangia mume kutembea na hausigeli, tuhitimishe mada yetu kwa kuangalia nini cha kufanya ili kuzuia hali hii. Jambo la kwanza ni kwa wanawake ambao wapo kwenye ndoa, kutojisahau katika kutimiza majukumu yao ya kila siku yanayohusu ndoa.

Kama wewe ni mama wa familia na una msichana wa kukusaidia kazi, ni vizuri ukawa na utaratibu wa kumfanyia mumeo mambo yote muhimu. Usiache dada wa kazi amfulie mumeo nguo, atandike kitanda unacholala na mumeo au ampikie na kumuandalia maji ya kuoga.

Hayo ni majukumu ambayo unapaswa kuyafanya wewe mwenyewe. Muachie dada wa kazi majukumu mengine kama kuwalea watoto na kufanya usafi wa nyumba lakini mambo yote yanayomhusu mumeo, fanya wewe mwenyewe.

Pia jambo jingine, ni kuepuka kumfanya hausigeli akazoeana na mumeo hadi kupitiliza. Ni makosa kumuacha dada wa kazi sebuleni akiangalia runinga na mumeo wakati wewe umelala. Pia kuwa makini na mazingira yoyote yanayoweza kutoa mwanya kwa wao kuzoeana.

Mwisho ni kwa wanaume wenyewe kuwa waaminifu kwenye ndoa zao na kuwatunzia heshima wake zao, hata inapotokea wamesafiri na kuwaacha na mahausigeli. Mwanaume anayempenda mkewe na kujiheshimu yeye mwenyewe, kamwe hawezi kumtongoza hausigeli! Badilika. Tukutane wiki ijayo kuangalia ni mambo gani unayopaswa kuyafanya ili kuondoa kabisa mianya ya kuibiwa mumeo na hausigeli wako. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

GPL

No comments: