Advertisements

Monday, December 22, 2014

UNAMUANDALIA FUMANIZI UMPENDAYE, UMEJIANDAA KIHISIA?

Ni Jumatatu nyingine tunapokutana katika uwanja wetu huu mzuri, tukijuzana na kuelimishana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, nakukaribisha tena tujadiliane na kuelimishana mambo mbalimbali yanayotuhusu
Mada ya leo ni kama inavyojieleza hapo juu. Upo kwenye uhusiano, unahisi kwamba
mwenzi wako anakusaliti na kuna viashiria mbalimbali kwamba mwenzi wako anatoka kimapenzi na mtu mwingine.
Kutokana na hasira au kwa kutaka kumkomoa, unamuandalia fumanizi. Mwisho unafanikiwa kumnasa ‘red hendedi’ akiwa na mwizi wako. Je, wakati unafanya maandalizi ya kumfumania, pengine kwa kuita mashahidi, wapiga picha, mjumbe na polisi, lengo lako lilikuwa nini? Ulikuwa umejiandaa kwa kitakachotokea?

Huenda msomaji wangu ukashangaa kwa nini nimeuliza hivi na pengine bado hujaelewa hoja ninayotaka kuijenga ni ipi. Hapa sizungumzii yale mafumanizi yanayotokea bila kupangwa.

FUMANIZI AMBALO HALIJAPANGWA
Kwa mfano umeenda kazini na kumuacha mwenzi wako nyumbani, ghafla ukakumbuka kwamba kuna kitu muhimu umekisahau nyumbani, ukaamua kurudi bila taarifa na ghafla ukamfuma mumeo akiwa kitandani na dada wa kazi au ukamfuma mkeo akiwa kitandani na jirani au muuza genge.
Ni dhahiri kwamba aina hii ya fumanizi inakuwa haijapangwa ila ni Mungu tu ameamua kukuonesha ukweli. Hapa sizungumzii aina hii ya mafumanizi bali nataka tujadiliane kuhusu yale mafumanizi ya kupangwa.


FUMANIZI LA KUPANGWA
Kwa mfano umenasa meseji kwenye simu ya mumeo akiwekeana ahadi na mwizi wako kwamba wakutane gesti fulani wakaibanjue amri ya sita. Bila mumeo kujua wewe ukaandaa majeshi yako na siku ya tukio, mumeo akiwa na mwizi wako gesti, wakiwa hawajui hili wala lile, mnawafumania, picha za ushahidi zinapigwa, mashahidi wanaona na mtaa mzima unajua.

Au umegundua kuwa mkeo anatoka na jamaa wa mtaa wa pili wewe ukiwa umesafiri. Unaamua kumdanganya mwenzi wako kwamba unasafiri na kuacha wapelelezi wa siri wafuatilie nyendo za mkeo.
Unapoondoka tu, anawasiliana na mchepuko wake, wanapanga kukutana na kwa kuwa kuna wapelelezi umewaacha, wanakutonya kila kitu na hatimaye mnafanikiwa kuwanasa wakiwa eneo la tukio.

ULIJIANDAA KIHISIA KABLA YA KUFUMANIA?
Bila shaka umeanza kupata picha ninachotaka kukizungumzia hapa. Je, katika mifano ya hapo juu ya mafumanizi ya kupangwa, wakati unaandaa mipango ya kumfumania mwenzi wako, kichwani mwako ulikuwa unawaza nini? Ulikuwa umeshajiandaa kihisia?

Ulikuwa unataka ukimfumania umpe au udai talaka na huo ndiyo mwisho wa uhusiano wenu au ulikuwa unataka kuhakikisha kama ni kweli? Ulikuwa unataka kumkomoa mwenzi wako au mwizi wako kisha maisha yaendelee kama kawaida?

Ni ukweli ulio wazi kwamba hakuna kitu kinachoumiza moyo kama pale unapogundua kuwa mwenzi wako ana uhusiano na mtu mwingine. Hata kama unahisi tu, moyo huwa unaumia sana.
Yote tisa, kumi hakuna kitendo kinachoumiza au kinachoweza kukufanya ukaathirika mno kisaikolojia maisha yako yote kama kumfuma laivu mwenzi wako akiwa kitandani na mtu mwingine. Awe na nguo au asiwe na nguo, kitendo cha kuwafuma wakiwa wawili tu chumbani, kinaweza kukufanya ukatamani ardhi ipasuke na kukumeza.

Hakuna lugha nyepesi inayoweza kutosha kuelezea maumivu yake, wale waliowahi kuwafumania wenzi wao watakuwa wananielewa vizuri zaidi. Ninachotaka tujadiliane na wewe msomaji wangu ni hiki:
Je, kuna umuhimu wa kumuandalia fumanizi mwenzi wako wakati bado unampenda na unataka muendelee kuishi pamoja, kulea watoto na kutimiza ndoto zenu? Naomba uwe huru kutoa mawazo yako kwa namba za hapo juu halafu wiki ijayo tutaendelea kuangalia mawazo ya kila mmoja na mwisho kufikia hitimisho.

GPL

No comments: