Advertisements

Saturday, January 31, 2015

BALOZI IDDI AFUNGUA MKUTANO WA 18 WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akiambatana na Makatibu na walinzi wa Baraza hilo wakitoa nje mara baada ya kufungwa kwa Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Mbweni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifunga Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa Majengo ya Baraza hilo uliyopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Aliyepo meza ya juu ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho. Picha na – OMPR – ZNZ.
*************************************************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakamilisha utafiti wa kuibua vivutio vipya vya Utalii vilivyopo katika maeneo ya vijiji nchini ambapo matokeo ya utafiti huo yatasambazwa kwa wanachi ili kuongeza uelewa wa fursa za sekta ya utalii zilizomo katika maeneo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiufunga Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa Majengo ya Baraza hilo yaliyopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi kwa Wananchi hasa wale wa Vijijini katika kuendeleza ile azma ya Serikali ya kuimarisha Utalii kwa wote.
Alisema mwishoni mwa mwaka uliopita Sekta ya Utalii imefanikiwa kutoa fursa za ajira zisizokuwa za moja kwa moja zipatazo 60,000 na zile za moja kwa moja 22,884 ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa umefikia asilimia 27%.
Balozi Seif alieleza kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika maendeleo ya Taifa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kitaasisi na kiutendaji ili kukidhi viwango vinavyokubalika kimataifa katika utoaji wa huduma za kitalii.
Alifahamisha kwamba Serikali itazidi kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango ambazo zitakuwa na uwezo wa kuingia kwenye soko la utalii na hivyo kuifanya sekta hii kuzidi kuwanufaisha zaidi wananchi ambao ndio walengwa wakuu.
Alieleza kuwa hivi sasa wananchi waliowengi hasa wakulima wamepata fursa ya kuuza bidhaa wanazozalisha mashambani kuuza kwenye hoteli mbali mbali hali ambayo imeongeza upatikanaji wa soko la uhakika wa bidhaa zao.
Alisema kuwa ili sekta ya utalii izidi kukuwa na kuleta tija hakuna budi kwa Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wananchi kuimarisha vivutio pamoja na mindombinu itakayowavutia watalii ikiwemo usafi na utunzaji wa mazingira, uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zenye viwango bora.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliziagiza Taasisi zinazohusika katika kusimamia sekta hiyo kuandaa na kutekeleza mipango itakayoamsha ari ya wananchi kupenda kutembelea maeneo yenye vivutio vya utalii kwa lengo la kukuza utalii wa ndani.
Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba kuimarika kwa utalii washirika wote wa sekta hiyo hawanabudi kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na eneo hilo yanakusanywa kikamilifu na kuingia katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Aliendelea kusisitiza umuhimu wa kuendelea kudumishwa kwa amani iliyopo hapa nchini ambayo ndiyo kichocheo kikubwa kinachotoa fursa kwa wageni na watalii kupenda kuvitembelea visiwa vya Zanzibar.
Akizungumzia sekta ya kilimo ambayo bado ni tegemeo kubwa la wananchi waliowengi katika kujipatia ajira, kipato,chakula na kuimarisha lishe na afya zao Balozi Seif alisema Serikali inaendelea kutoa msukumo mkubwa kusaidia sekta hiyo ili wananchi waweze kuongeza tija na uzalishaji na hivyo kuimarisha vipato vyao.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kwamba huduma za kilimo cha matrekta na zana nyengine za kilimo zinapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu zitakazotoa nafasi kwa wakulima kuzimudu.
Alisema mpango huo utakwenda sambamba na ongezeko la kiwango cha upatikanaji wa mbegu bora ya mpunga, dawa ya kuulia magugu na mbolea kupitia programu ya ruzuku katika kilimo cha Mpunga.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wakulima wote wa zao la mpunga nchini kuungana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kutumia fursa zilizopo kuhakikisha wanalima kwa wakati na kufuata kanuni za kilimo bora.
Halkadhalika Balozi Seif akawahimiza wakulima wote wa mazao mengine kuchukuwa juhudi stahiki kwa kufuata ushauri wa mabwana shamba na Mabibi shamba ili nao waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.
Akigusia suala la udhalilishaji wa kijinsia ambalo linaendelea kuwa changamoto licha ya juhudi zinazochukuliwa za kudhibiti vitendo viovu lakini Balozi Seif alisema bado wapo watu miongoni mwa jamii wanaoendeleza vitendo hivyo.
Alisema ni wajibu wa kila mwana jamii kuzidisha mapambano dhidi ya waovu wanaohusika na matendo hayo kwa kuwafichua na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria bila ya kuwaonea muhali.
Alisema waovu hao kwa kiasi kikubwa wanavunja utu na heshima za kibinaadamu na kuwasababishia madhara makubwa ya kimwili na kiakili.
“ Watu wote wenye taarifa za waovu hao ni vyema kutosita kufika mahakamani kwa kutoa ushahidi pale wanapohitajika na kuacha kabisa masuala hayo kumalizikia majumbani “. Alisema Balozi Seif.
Kuhusu utolewaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi pamoja na Viongozi hasa wale wa Kisiasa waelewe kwamba huduma hiyo hutolewa kwa mujibu wa sheria nambari 7 ya Mwaka 2005.
Alisema muhusika lazima atimize matakwa ya sheria hiyo kabla ya kupatiwa kitambulisho ambayo ni pamoja na Mzanzibari wa kuzaliwa, mwananchi kukaa katika eneo lake si chini ya miezi 36 sambamba na kutimiza umri wa miaka 18.
Hata hivyo Balozi Seif alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 13 { 1 } { 2 } cha sheria hiyo imetoa haki kwa mtu kukata rufaa kwa Mkurugenzi wa Vitambulisho dhidi ya Afisi ya usajili pindipo hakuridhia na mamuzi yanayotolewa au kwa waziri kama pia hakuridhika na uamuzi wa Mkurugenzi.
Alisema suala la utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari limekuwa na mjadala mkubwa kutokana na baadhi ya wanasiasa na waheshimiwa kulalamikia juu ya baadhi ya wananchi wao kutopatiwa vitambulisho hivyo kwa sababu mbali mbali.
Alielezea imani yake kwamba waheshimiwa wawakilishi, wanasiasa na wananchi hawana sababu ya kulalamikia suala hilo ambalo lina utaratibu mzuri uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitanabahisha kwamba suala zima la upatikanaji wa vitambulisho hivyo lisihusishwe na mambo ya kisiasa kwani utaratibu wa kisheria upo. Hivyo ni vyema na wajibu wa kila mwananchi kutumia sheria hiyo katika kutafuta haki yake.
Miswada Minne ya Sheria iliwasilishwa katika Mkutano huo wa 18 wa Baraza la Wawakilishi na kujadiliwa na wajumbe wa Baraza hilo ambayo ni Mswada wa sheria ya kuanzisha sheria ya kupunguza na kukabiliana na maafa Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mwengine ni Mswada wa sheria ya kuanzisha Taasisi ya ulinzi ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar, Mswada wa sheria ya kufuta sheria ya usimamizi wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu nambari 2 ya mwaka 1996 na kuweka badala yake msharti bora ya kuhifadhi, kulinda na kusimamia mazingira pamoja na mswada wa sheria ya maadili ya Viongozi wa umma na kuanzisha Tume ya maadili ya Viongozi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 11 Machi mwaka 2015 mnamo saa 3.000 za asubuhi.
SOURCE:SUFIANIMAFOTO

No comments: