ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 21, 2015

BALOZI IDDI APOKEA MAANDAMANO YA WAZAZI NA WANAFUNZI KUUNGA MKONO UCHANGIAJI WA ELIMU

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea Maandamano ya Wanafunzi na wazazi wa Wilaya ya Magharibi kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein, kuhusu uchangiaji wa elimu ya msingi na ada za mitihani kwa Kidato cha Nne na Cha Sita aliyoitoa katika kilele cha sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baadhi ya wazee na wazazi wa Wilaya ya Magharibi wakiwa katika mkutano wa Kumpongeza Rais Shein kufuta uchangiaji kwa elimu ya msingi na ada za mitihani kwa Kidatu cha Nne na Cha Sita hapo viwanja vya michezo nyuma ya Skuli ya Mwanakwerekwe “C “.
Vijana na Wanafunzi wa Skuli za Wilaya ya Magharibi wakionyesha kuunga mkono kauli ya Dr. Shein kufuta uchangiaji kwa elimu maskulini.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna akitoa kauli ya kutolewa matokeo ya mitihani ya darasa la saba na Kidatu cha pili ijumaa ijayo hapo katika Mkutano wa kupongeza Rais wa Zanzibar kutoa kauli ya kufuta uchagizji wa elimu Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapongeza Wazazi, walezi na Wanafunzi wa Wilaya ya Magharibi kwa uamuzi wao wa kupongeza Rais wa Zanzibar Dr. Shein kutokana na kauli yake ya kufuta uchangiaji wa elimu Nchini. Picha na – OMPR – ZNZ
.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaangalia hali ya ukuaji wa uchumi ili kujenga mazingira yatakayowezesha huduma za Afya kurejea kuwa bila malipo kama ilivyotangazwa na Rais wa Zanzibar kufuta uchangiaji kwa Elimu ya msingi na ada ya Mitihani ya Skuli za Sekondari.
Alisema hatua hiyo ya Serikali inalenga kuipa nguvu azma ya Chama cha Afro Shirazy Party { ASP } ya kutangaza elimu na huduma za afya bila ya malipo mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964.
Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kuyapokea maandamano ya kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kufuta uchangiaji kwa elimu ya msingi na ada za mitihani kwa Kidatu cha Nne na Cha Sita aliyoitoa wakati wa kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi Januari 12 2015.
Maandamano hayo ya kumuunga mkono Dr. Shein yaliandaliwa na wazazi na Walezi wa Wilaya ya Magharibi na kuwashirikisha wanafunzi, vijana na wazee wa Wilaya hiyo yaliyofanyika katika viwanja vya michezo vilivyopo nyuma ya Skuli ya Mwanakwerekwe “C “.
Balozi Seif alisema licha ya Sekta ya elimu kukabiliana na changamoto nyingi lakini Serikali itajitahidi kuona kwamba inajaribu kutatua kero pamoja na changamoto hizo hasa suala la uhaba wa vikalio na upungufu wa madarasa kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi katika skuli mbali mbali hapa nchini.
Aliwaasa wanafunzi waendelee kuitumia fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii na maarifa na kuacha tabia ya kukaa katika magenge yanayoweza kuharibu mfumo mzima wa maisha yao ya baadaye.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kubeba mzigo huu ili kuwapa fursa zaidi watoto wasome kwa utulivu “. Alisema Balozi Seif.
Aliwahimiza Wazazi kuwa na kazi ya ziada katika kufuatilia mienendo ya watoto wao ili kujaribu kuwalinda na vishawishi vinavyoweza kuwatia katika balaa na kuwavurugia maendeleo yao.
Alisema kwamba masomo ya ziada { yaani tuition } kwa wanafunzi yamekuwa yakitumiwa vibaya na baadhi ya wanafunzi na matokeo yake wanafunzi wa kike kuingia kwenye mtego mbaya wa kubeba ujauzito.
Akisoma Risala ya Wanafunzi wa Skuli za Wilaya za Magharibi Mwanafunzi Mwisi Juma alisema wanafunzi wa Wilaya hiyo wamefarajika na kauli ya Rais wa Zanzibar ambayo imeonyesha azma ya Serikali ya awamu ya kwanza ya kutangaza Elimu bila ya malipo.
Mwanafunzi Mwisi Juma kwa niaba ya wenzake ameiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kutenga Bajeti maalum itakayokidhi huduma za maskuli nchini kote kwa kufidia pengo hilo.
Naye Mwalimu Amour Haji Nassor akitoa salamu za Wazee na Wazazi wa Wilaya ya Magharibi amempongeza Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kwa uamuzi wake huo wa kufuta michango kwa skuli za msingi na ada za Mitihani kwa Kidatu cha Nne na cha Sita.
Mwalimu Amopuralisema michango ya skuli ilikuwa mzigo mkubwa kwa wazazi hasa wale wenye watoto zaidi ya mmoja ambayo ilikuwa ikiwapa wakati mgumu kuweza kuendesha familia zao na wakati huo huo kuhudumia fedha za skuli kwa watoto wao.
Alieleza kwamba wazazi na walezi wanatarajiwa kushuhudia ile manifesto na azma ya ASP iliyotoa ya kila mtoto wa mkwezi na mkulima wa Zanzibar asome bila ya malipo inarejea kutekelezwa kwa vitendo.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamuhuna aliwatoa hofu wananchi kwamba kauli ya Rais wa Zanzibar itatekelezwa vyema na Wizara hiyo.
Waziri Shamuhuna akifafanua baadhi ya hoja za Wazazi kuhusu ucheleweshwaji wa matokeo ya Mitihani alisema matokeo ya Darasa la saba na Kidatu cha Pili yako tayari na yanatarajiwa kutolewa Ijuma ya wiki hii.
Waziri huyo wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar aliwaeleza wanafunzi hao na wazazi wote nchini kwamba matokeo ya mtihani wa Darasa na Saba na Kidatu cha Pili mwaka huu yamekuwa mazuri ikilinganisha na matokeo ya mitihani ya mwaka uliopita.

No comments: