Balozi Seif akiwapungia mkono wananchi waliohudhuria ufunguzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo { Makonyo Conference Cetre } wakati akiingia kwenye eneo hilo. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Bishara, Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi ukumbi wa Mikutano uliopo Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Kisiwani Pemba.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Biashara na Serikali Kisiwani Pembna m,ara baada ya kuufungua rasmi Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo Uliopo Wawi Chake chake Pemba.
Balozi Seif na mwenyeji wake Waziri wa Biashara Mh. Mazrui akiwapunghia Mkono washiriki wa hafla ya ufunguzi wa Ukumbi wa Mikutanop wa Makonyo wakati akiwasili kwenye uwanja wa Mkutano.
Kikundi cha Utamaduni ya Wilaya ya Mkoani kikitoa burdani safi ya ngoma maarufu ya kibati wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo kwenye shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baadhi ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Pemba wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufungua rasmi Ukumbi wa Kisasa wa Mikutano wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } {Makonyo Conference Hall } hapo Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Pemba ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kusherehekea miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema hatua hiyo ya ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa pia itasaidia kuondokana na usumbufu wa malazi kwa wageni mbali mbali wa Kitaifa na Kimataifa watakaofika katika ukumbi mpya uliojengwa na shirika hilo kwa ajili ya Mikutano.
Balozi Seif alisema Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar ni miongoni mwa Mashirika ya Umma yanayofanya kazi zake vizuri ambapo ujenzi wa ukumbi wake wa Mikutano wa Makonyo ni sehemu moja wapo ya mageuzi ya maendeleo yanayoendelea kutekelezwa na Shirika hilo.
Alitoa wito kwa Taasisi nyengine za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia sasa ni vyema zikautumia ukumbi huo wa Makonyo kwa mikutano na shughuli nyengine lakini wahakikishe wanalipa kodi ili fedha zinazopatikana ziweze kuibua miradi mengine ya Maendeleo.
“ Ukumbi lazima upewe heshima yake kwa kuendeleza ujenzi wa vyumba vizuri vya hoteli vitakavyotumiwa na hata viongozi wa Kitaifa badala ya kubabia hoteli zisizo na kiwango “. Alisema Balozi Seif.
Aliwatahadharisha wasimamizi wa Ukumbi huo kuhakikisha kwamba kila atakayetumia ukumbi huo analipa kwanza ili uweze kujiendesha wenyewe na kuwacha kutegemea Shirika lenyewe au Wizara husika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameupongeza Uongozi na watendaji wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar kwa juhudi zao zinazopelekea zao la Karafuu nchini kuzalishwa kwa wingi na kupatikana kwa bei nzuri ya mauzo kwa wakulima.
“ Naishukuru Bodi ya Wakurugenzi, Uongozi wa Shirika na watendaji kwa juhudi zao ulio bora wa mashirikiano uliowezesha Shirika hilo kupiga hatua kubwa za maendeleo “. Alisema Balozi Seif.
Alisema mipango bora ya Shirika hilo imesaidia kuwakomboa wakulima wengi wa zao la karafuu wa Unguja na Pemba kwa kuuza karafuu zao kwenye vituo vya shirika hilo kwa faida kubwa Serikalini.
Aliwaomba wananchi wajitahidi kadri ya uwezo wao kuelimishana nuu ya kulienzi zao la Karafuu linaipatia mapato makubwa Serikali Kuu pamoja na wananchi wenyewe.
Balozi Seif alisema hakuna sababu ya kukatwa kwa miti ya mikarafuu kwa ajili ya kuni au mkaa kwani tabia hiyo ni kinyume na sheria. Hivyo Viongozi na wananchi wanapswa kushirikiana kuzuia tatizo hili na ikiwezekana hatua kali zichukuliwe kwa wale wanaojihusisha na ukataji onvyo wa miti hiyo ya mikarafuu.
Aliuomba Uongozi na Watendaji hao wa ZSTC kuongeza juhudi katika kuhakikisha karafuu za Zanzibar zinazalishwa kwa wingi katika kiwango kinachokubalika kitaalamu duniani.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la ZSTC Bwana Kassim Maalim Suleiman alisema shirika hilo limo katika harakati za mageuzi iliyojipangia katika kipindi cha miaka 10.
Bwana Kassim alisema ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo ni miongoni mwa mageuzi hayo ambayo sasa yako katika kipindi cha miaka mitatu tokea ilipozinduliwa Bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo mwaka 2012.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Biashara aliiomba Serikali kuifuatilia changamoto inayolikabili Shirika hilo la Ofisi yake iliyoko Mjini Dar es salaam ambayo ni jengo la Shirika la Nyumba Tanzania.
Akisoma risala ya wafanyakazi wa shirika hilo mwakilishi wa Chama cha TUICO – ZSTC Ndugu Suleiman Juma alisema Wafanyakazi wa shirika hilo wameahidi kutekeleza wajibu wao kwa nguvu zao zote.
Nd. Suleiman alisema watendaji wa shirika hilo wamefarajika kufuatia Shirika hilo kuwa miongoni mwa Taasisi za umma zinazolipa kodi kwa wakati na kufikia hatua ya kupata zawadi bora kutoka kwa Kodi ya Mapato Tanzania.
Alisema zipo changamoto zinazosababisha kupunguza ari ya watendaji wa shirika hilo hasa suala zima la mabadiliko ya Mishahara ya wafanyakazi ambalo limekuwa sugu na kuleta usumbufu mkubwa.
Alisema shirika kupitia chama cha wafanyakazi cha TUICO limeshakamilisha taratibu zote za maombi ya kufanyiwa marekebisho ya mishahara ya wafanyakazi kwa kutumia sheria nambari mbili ya mwaka 2011 ya utumishi Serikalini.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika Hafla hiyo Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Mh. Nassor Ahmed Mazrui aliwataka wananchi kushirikiana na Uongozi na watendaji wa shirika la ZSTC ambalo ndilo linalojenga uchumi na Maendeleo ya Taifa.
Waziri Mzrui alielezea matumaini yake kutokana na juhudi za wafanyakazi kujituma katika muda wote na kulisababishia shirika hilo kuwa kigezo kwa mashirika mengine ya Serikali.
Aliwahakikishia wananchi kwamba shirika la Taifa la Biashara Zanzibar litafanya biashara zote kubwa kutokana na mabadiliko ya biashara duniani ili lizidi kuimarika na kusaidia kuchangia mapato ya Serikali.
“ Hakuna sababu kwa wafanyakazi wa shirika la ZSTC kutokufanyiwa marekebisho ya mishahara yao kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kuliimarisha shirika hili kiuchumi. Hili kama mimi ni Waziri nitahakikisha nalisimamia kwa nguvu zangu zote “. Alisema Waziri Mazrui.
Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo uliopo Wawi chake chake Pemba ujenzi wake umegharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni mia Nne na Thamanini na Nane { 488,000,000/-.
No comments:
Post a Comment