ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 7, 2015

CCM, CUF WALIANZISHA

Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Hivi sasa mimi ni kiongozi halali kwa mujibu wa sheria,”
Dar es Salaam. Utata mpya umeibuka kuhusu matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya wagombea watatu waliotangazwa washindi kuwekwa kando ikidaiwa kuwa badala yake walioshindwa waliapishwa kuchukua nafasi zao, hali iliyozua vurugu kubwa zilizotulizwa na polisi kwa mabomu ya machozi Ubungo jana.
Kutokana na hali hiyo, wafuasi wa CUF wanaodai wagombea wa chama chao ndiyo walioshinda, waliibuka na kutanda nje ya Hoteli ya Landmark kupinga kuapishwa kwa baadhi ya wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa CCM katika Wilaya ya Kinondoni, hatua iliyosababisha baadhi ya wagombea na mashabiki kushushiwa kipigo hadi polisi walipoingilia kati kwa kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Vurugu hizo zilizodumu kuanzia saa tatu hadi saa tano asubuhi, zililenga kuzuia wateule watatu wa mitaa ya Ukwamani, Pakacha na King’ong’o kuapishwa kwa madai kuwa siyo walioshinda.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Msisiri, Juma Mbena alivamia eneo hilo akidai kuwa Gasper Chambembe (CUF), ambaye alishinda katika mtaa huo hakustahili kuapishwa, kitendo kilichosababisha ashushiwe kipigo na wafuasi wa CUF.
Licha ya Mbena kupigwa na kuchaniwa nguo, pia Sultan Jetta (CCM) ambaye alitangazwa kushinda katika Mtaa wa Ukwamani, Kawe alizuiwa na wafuasi wa CUF kuapishwa, wakidai kuwa mgombea wao, Nasri Mohammed Mashaka ndiye aliyestahili kuapishwa. Alipogoma, walimkamata na kumshushia kipigo hadi alipookolewa na polisi.
Baadaye Jetta alirudishwa ukumbini chini ya ulinzi wa polisi na kuapishwa pamoja na wenyeviti wenzake 153 kati ya 191 wa Wilaya ya Kinondoni.
Aliyekuwa mgombea wa Mtaa wa Pakacha Kata ya Tandale, Hussein Juma Mpeka (CUF) alidai kuwa licha ya uchaguzi huo kuvurugika, alipewa barua ya kuitwa kuapishwa lakini baada ya kufika eneo hilo alikataliwa kuingia ukumbini, badala yake aliyeruhusiwa ni Nassib Omary Kalenga wa CCM.
Hali ilivyokuwa
Shughuli ya kuapisha wenyeviti hao ilianza saa mbili asubuhi na baada ya saa moja, wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo walikusanyika eneo hilo ili kushuhudia uapishwaji huo.
Kati yao walikuwapo viongozi wa vyama vya CCM na CUF wa Wilaya ya Kinondoni pamoja na wagombea walioeleza kuwa walishinda katika uchaguzi na matokeo yao kutangazwa lakini hawakupewa barua za uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika.
Waendesha bodaboda na wananchi wanaofanya biashara zao kando ya hoteli hiyo nao walikusanyika kwa lengo la kushuhudia kinachoendelea hali iliyowafanya polisi waliokuwa katika magari mawili aina ya Landrover Defender kuwataka wananchi hao kuwa watulivu.
Mmoja wa wakazi wa Kawe, Anna Cheupe aliyekuwa eneo hilo alisema licha ya kuwa ni mwanachama wa CCM, hakufurahishwa na kitendo cha matokeo ya Mtaa wa Ukwamani kubadilishwa, kauli ambayo iliungwa mkono na watu waliokuwa karibu yake.
Wakati idadi ya watu ikizidi kuongezeka, polisi walisikika wakiomba msaada kwa wenzao na ilipofika saa 3.55 asubuhi magari mengine mawili yalifika na askari waliokuwamo kuanza kupiga mabomu ya machozi mfululizo kwa nusu saa.
Mabomu hayo yalisababisha wananchi kukimbia ovyo na wengine kunusurika kugongwa na magari yaliyokuwa yakipita katika Barabara ya Mandela kabla ya kufungwa kwa muda.
Risasi zilipigwa hewani ili kuwaokoa watu waliokuwa wakishambuliwa kwa kupigwa huku sauti zikisikika, “Piga hao wezi…, mwizi, piga mwizi huyo. Tuuweni tumechoka kuonewa, Pigeni tena nyingine hewani.”
Polisi waliwaokoa Mbena na Jetta na kuondoka nao na baadhi ya wenyeviti waliokuwa wakisubiri kuapishwa walizirai. Askari waliokuwa hawana vifaa vya kufunika uso, waandishi wa habari na wahudumu wa hoteli walikimbia kutafuta maji ya kunawa uso.
Utata wa matokeo
Kutokana na utata, kila chama kilikuwa na matokeo yake. Mwenyekiti wa CUF, Kata ya Kawe, Bakari Mozina alisema katika Mtaa wa Ukwamani, mgombea wa chama hicho alipata kura 568 na CCM 560 lakini matokeo yalibadilishwa.

“Tunashangaa kwa nini ameitwa kuapishwa mgombea wa CCM wakati sisi ndiyo tulioshinda?” alihoji.
Alisema licha ya utata wa matokeo, pia kulikuwa na utata wa majina… “Katika karatasi ya kupigia kura kulikuwa na jina la Seleman Mohammed Jetta, anayeapishwa leo (jana) ni Sultan Jetta ambaye tunapinga asiapishwe.”
Wakati Mozina akieleza hayo, Jetta alisema yeye ndiye mshindi katika mtaa huo kwa kuwa alipata kura 561 na CUF wa alipata kura 548. Katika Mtaa wa King’ong’o, aliyekuwa mgombea wa CUF, Abubakar Nyanguma aliyedai kuwa alishinda alisema: “Mimi nilipata kura 461 na mgombea wa CCM, Demetrius Mapesi alipata kura 450, cha ajabu barua ya kuitwa kuapishwa amepewa mwenzagu badala ya mimi.”
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Wilaya ya Kinondoni, Danstan Tido alisema washindi watatu katika wilaya yake wamenyimwa barua za kuitwa kuapishwa na ndiyo chanzo cha wafuasi wa chama hicho kujazana eneo hilo ili kushuhudia nani atakayeapishwa.
“Washindi wa mitaa ya King’ongo, Pakacha na Ukwamani ndiyo waliostahili kuapishwa leo baada ya kutangazwa washindi katika uchaguzi uliopita. Lakini tunashangaa kuona kuwa hawakupewa barua za kuwatambua, hii siyo demokrasia tunayoitarajia katika mfumo huu wa vyama vingi,” alisema Tido.
Mmoja wa wafuasi wa chama hicho kutoka Kawe, Jafari Makonyola alisema walikwenda katika hoteli hiyo kuhakikisha kuwa wanaostahili ndiyo wanaapishwa na si vinginevyo.
“Lengo letu ni kuona tuliyemchagua ndiye anayeapishwa na ikishindikana basi asiapishwe yeyote. Matokeo ya uchaguzi ni lazima yaheshimiwe kwa kuwa wanaochaguliwa wanakuja kufanya kazi na wananchi, hivyo ni lazima tuwaridhie,” alisema Makonyola.
Mpeka alisema, “Ilinishangaza maana ofisa mtendaji aliniita na kunipa barua ambayo inaonyesha kuwa mimi ni mshindi. Niliipokea na kufika pale ukumbini na nilifanikiwa kuingia ndani ila baada ya muda alinifuata na kuniambia kuna tatizo, alinitoa nje na mgombea wa CCM akaingia ndani na kuapishwa. Sijaelewa nini kimetokea na sijui nini nifanye.”
Kauli ya Jetta
“Baada ya kuondolewa hapa nilipelekwa Kituo cha Polisi Urafiki ambako nilipewa PF 3 ili nikatibiwe na baadaye chini ya ulinzi mkali kama nilivyoondoka nilirudishwa hapa na kuendelea na zoezi hili. Hivi sasa mimi ni kiongozi halali kwa mujibu wa sheria,” alisema Jetta.
Kauli ya mkurugenzi
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Nati alisema wenyeviti walioapishwa jana ni 154 kati ya 191 lakini alipoulizwa sababu za wajumbe wengine kutohudhuria shughuli hiyo aling’aka akisema, “Baadhi ni wagonjwa na wengine wana sababu zao… nyingine ongeza wewe mwandishi, mimi nitajuaje kila sababu ya mshiriki kutohudhuria?”
Alipotakiwa kufafanua sababu za kuvuruga matokeo ya uchaguzi na kuathiri uapishwaji wa wenyeviti hao, mkurugenzi huyo alikataa kuzungumza.
Awali, akizungumza na wenyeviti hao, Nati alisema hakuna atakayedhulumiwa nafasi yake... “Ngoja niwape neno la uchokozi, ikitokea mtu asiyehusika akasaini (fomu za kiapo), mfano mwandishi wa habari au mhudumu wa hoteli, hatutamtambua kwa kuwa hausiki. Wenyeviti wote tunawatambua hivyo kuweni na amani,” alisema Nati.
Lipumba akoleza
Katika hatua nyingine; Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amewataka wananchi wa Kata ya Buguruni kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli ya kuapishwa kwa wenyeviti wa mitaa wa Manispaa ya Ilala leo ili kudhibiti uchakachuaji unaofanywa dhidi ya vyama vya upinzani.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara jana, Kata ya Buguruni jana, Profesa Lipumba alisema ufisadi wa CCM umekithiri mpaka kwenye matokeo ya uchaguzi ambayo tayari yanafahamika kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa ni jukumu la wakazi wa kata hiyo kutetea haki yao ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Aliwatahadharisha wasikubali kumpokea mwenyekiti ambaye hawajamchagua katika mitaa yao.
“Ni jukumu lenu kulinda kura zenu, lakini ni muhimu zaidi kulinda matokeo wakati wa kuapisha. Zoezi la kuapisha wenyeviti limevurugika kule Kinondoni, sasa kesho ni zamu ya Ilala. Mjitokeze kwa wingi ili wasifanye kama walivyofanya Kinondoni,” alisema.
Profesa Lipumba aliwashukuru wananchi wa Kata ya Buguruni kwa kuwachagua wenyeviti wa mitaa kutoka CUF, hali aliyosema inathibitisha kuwa wamechoshwa na ufisadi unaofanywa na Serikali ya CCM.
Kata ya Buguruni ina mitaa sita, kati ya hiyo, CUF imeshinda mitano, mmoja ukichukuliwa na CCM.

Imeandikwa na Julius Mathias na Fidelis Butahe, Peter Elias. Mwananchi

No comments: