ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 2, 2015

ISHU SIYO MATATIZO BALI NAMNA TUNAVYOYAPOKEA NA KUYATATUA!

Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijaalia uzima na kunipa afya pamoja na nguvu za kutosha hivyo kuniwezesha kuendelea kutimiza yale ambayo naamini nastahili kuyatenda katika kila siku ya maisha yangu.

Ndugu zangu, mwaka ndiyo umeanza hivyo! Najua wengi wetu tuna malengo ambayo tumepanga kuyatimiza ndani ya mwaka huu wa 2015. Hilo ni jambo jema na nikufahamishe tu kwamba, maisha bila malengo hayana maana.

Jiwekee malengo na kuwa tayari kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza mbele yako, dhamira yako kubwa iwe kufika pale unapopataka.Hata hivyo, katika kutimiza malengo yetu kuna wakati tutakumbana na matatizo, hii ni kwa sababu matatizo katika maisha ya binadamu ni kitu cha kawaida.
Hakuna anayeweza kuyaepuka na ndiyo maana hakuna anayeweza kupitisha siku bila kukumbwa na tatizo, liwe dogo ama kubwa.

Lakini, utafiti unaonesha kwamba miongoni mwetu wapo watu ambao wanapokumbwa na matatizo hushindwa kuyachukulia kuwa ni ya kawaida, badala yake wanaishia kwenye kuvunjika mioyo na hata kumkufuru Mungu.

Ni wazi kwamba binadamu tunatofautiana katika namna tunavyoyapokea matatizo pale yanapotukabili, lakini baadhi ya watu wanapitiliza katika namna wanavyoyapokea kwani inafikia wakati mtu anapopatwa na tatizo huingia katika hali fulani ya kuona dunia ni mbaya na maisha ni yenye upendeleo.

Anashindwa kuyaangalia matatizo hayo kwa umakini na kuyakubali kisha kuangalia uwezekano wa kuyatatua, matokeo yake sasa tatizo linazidi kuwa kubwa.Katika maisha tunapoingia katika hali kama hii ni sawa na kujizuia kusonga mbele katika kupata ama kutafuta kile ambacho tunakitaka katika maisha yetu ya kila siku.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba hali ya kukata tamaa inapopiga hodi katika nafsi zetu huwa tunashindwa kufanya yale ambayo ni ya muhimu na kuishia kwenye kusononeka.Aidha, wengine wanapopatwa na matatizo badala ya kuyatafutia ufumbuzi hupandwa na hasira na wakati mwingine kuchukua uamuzi ambao haustahili.

Kwa mfano umekuwa katika uhusiano na mtu ambaye ulitokea kumpenda sana lakini ikafikia kipindi ukamkosa, aidha baada ya kufariki ama kuachana. Au fikiria umepata barua ya kuachishwa kazi au kama ni mwanafunzi umefeli katika masomo yako yote, hivi utajisikiaje?

Wapo ambao wamefika hatua ya kukatisha maisha yao kwa kukumbwa na matatizo kama hayo. Lakini je, huo ndiyo ufumbuzi sahihi? Hatuoni kwamba kwa kufanya hivyo ni sawa na kumkufuru Mungu?
Wengi wetu tunapokuwa katika matatizo tunaona kwamba maisha yamefika mwisho, tunaona Mungu ni mwenye upendeleo ama tunapopatwa na matatizo, Mungu anatuadhibu, dhana ambayo haina ukweli ndani yake.

Ndiyo maana kuna wakati unaweza kumkuta mtu anapokumbwa na tatizo fulani akasema; “Maskini mimi, nimemkosea nini Mungu.” Anasema hivyo kwa sababu anahisi yeye hastahili kupatwa na matatizo bali wanaostahili ni wale wakosaji tu.Ukweli ni kwamba, matatizo hayachagui mtu, humtokea kila mtu na wakati wowote lakini pia yana ufumbuzi wake.

Hivyo basi unapokumbwa na matatizo si vizuri kabisa kuanza kunung’unika bali fanya kila uwezalo kutafuta ufumbuzi tena kwa kutumia mbinu sahihi. Ninachopenda kushauri ni kwamba, kama unasumbuliwa na tatizo fulani si wakati wa kukata tamaa na kuona kwamba huna haki ya kuendelea kuishi.

Fahamu unayo nafasi ya kukabiliana vilivyo na matatizo hayo. Elewa unapokabiliwa na tatizo fulani kisha ukashindwa kutafuta ufumbuzi, unaweza kulifanya tatizo likawa kubwa zaidi ama kuzua tatizo lingine.

GPL

No comments: