ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 6, 2015

KUNA WALIOUMBWA KUTOKUWA NDANI YA NDOA?

SALAMU zangu za heri ya mwaka mpya wa 2015 ziende kwa kila msomaji wa safu hii ya maisha. Katika mada yangu ya leo, nimeanza na kichwa cha habari chenye swali. Lakini naamini tutakwenda sawasawa mpaka mwisho.

Nimeuliza kwenye utambulisho kuwa; kuna walioumbwa kutokuwa ndani ya ndoa? Hapa nina maana ya mwanamke na mwanaume!

KWANZA TUFAHAMU HILI

Kwanza napenda ieleweke kuwa ndoa ni mpango wa Mungu kwa wanadamu. Ndoa haihusiani hata kidogo na serikali, bali serikali imeikuta ndoa tayari ipo ndipo na yenyewe ikaweka utaratibu wa kusimamia.

Nasema hivi kwa sababu Mungu alipomuumba Adam na Hawa (Eva) na kuwaambia waishi bustanini, pale aliwafungisha ndoa. Kwa hiyo ndoa ni mpango wa kiimani au kidini zaidi.

TURUDI KWENYE MADA

Dunia ina jinsi mbili, mwanamke na mwanaume. Mwanamke akiolewa anakuwa mke, mwanaume akioa anakuwa mume. Lakini wote wasipofanya tukio la muunganiko wa ndoa hawana sifa ya kuitwa mke au mume.

Lakini duniani, wapo wanawake wameolewa tena kwa ndoa lakini hawana sifa ya kuwa wake, pia kuna wanaume wameoa pia hawana sifa ya kuwa waume.

KWA NINI?

Upo utaratibu wa maisha ya ndoa na pia kuna utaratibu wa maisha nje ya ndoa. Mmoja wapo anapoishi maisha ya nje ya ndoa ndiyo hao ninaosema waliumbwa wasiwe kwenye ndoa.
Lakini kundi hili ni vigumu kujijua kwamba wapo hivyo, wengine wanang’ang’ania ndoa lakini siyo fungu lao tangu kuzaliwa.

WENYE TABIA HIZI
Siku ya Krismasi nilibahatika kukutana na mwanamama mmoja ambaye katika utambulisho wake alisema anaishi peke yake, Sinza. Wakati anakutana na mimi alikuwa na mtoto wake mmoja wa kiume mwenye miaka kama kumi hivi.

Nilimuuliza alipo baba wa mtoto, nikiwa namaanisha ni kwa nini anaishi peke yake. Sikiliza majibu yake.
“Niliachana naye! Kusema ule ukweli nilipoishi na yule mwanaume ndipo niligundua kuwa, kuna wanaume wameumbwa kuwa wanaume mpaka mwisho wa maisha yao lakini hawafahi kuwa waume.”
Nilimuuliza anamaanisha nini katika ‘ubeti’ wake huo? Akajibu:

“Yule mwanaume alikuwa akilala nje karibu kila siku. Anarudi nyumbani asubuhi. Akirudi ananukia pafyumu wakati mwingine nilikuwa namkuta na kondom kwenye mifuko ya suruali.
“Ile ilinipa picha kwamba, huwa analala kwa wanawake. Nilijaribu sana kumuweka sawa na aachane na tabia hiyo lakini wapi! Maisha hayo aliendelea nayo kwa miaka mitano tukiwa wote.

“Mbaya zaidi, hakuwa akimjali mtoto japokuwa alikuwa na fedha. Hakumjali kwa ada wala nguo za shule achilia mbali chakula. Sasa nikaja kubaini kuwa, nilikuwa nimeolewa na mwanaume lakini hakuwa na sifa ya kuwa mume. Maisha yake ni ya kuwa mwanaume tu.”

AKADAKIA HUYU MZEE

Wakati mwanamke huyo anasema hayo, akadakia mzee mmoja aliyekaa meza ya pembeni, naye akasema:

“We mama uko sahihi kabisa! Tena leo na mimi umenifungua akili. Niliwahi kuishi na mwanamke tena kwa ndoa kwa miaka kumi. Lakini miaka yote kwangu ilikuwa ya presha. Mara katembea na mchota maji, mara kalala na mgeni wa mpangaji mwenzangu.

“Nimewahi kumfumania mara tatu, tena na marafiki zangu. Kuna siku alikwenda kijijini kwao, Kondoa nikaletewa habari alivunja ndoa ya mtu kwa kutembea na mume.
“Nyumbani alikuwa hakai maana tulikuwa tuna gari. Basi akishakunywa chai, anatoka na gari kwenda kuzurura, kurudi kwake usiku, saa mbili. Mapishi yote ni kazi ya msichana wa kazi. Kufua nguo zangu ni msichana. Ilifika mahali hata kutandika kitanda ni msichana wa kazi.

“Nilipochoka sana nilimpa talaka kwa sababu imani ya dini yangu inaruhusu. Lakini kwa maneno yako wewe mama ndiyo nimebaini kuwa, hata mimi nilioa mwanamke asiyekuwa na sifa ya kuwa mke. Yule aliumbwa kuwa mwanamke tu.”

NI KWELI?

Ni suala la kujiongeza mwenyewe, kama wewe ni mke au wewe ni mume je, unatekeleza majukumu yako? Baba ndani ya nyumba anajulikana afanye nini, mama ndani ya nyumba pia anajulikana afanye nini?

Ubaba wa kulala nje ya nyumbani kila siku, tena kwa wanawake au umama wa kufumaniwa mara kwa mara na kukwepa majukumu ya nyumbani siyo sifa ya kuwa ndani ya ndoa.
Jipime wewe, upo katika kundi gani kwani si ajabu upo ndani ya ndoa kwa miaka kadhaa na kujisifia lakini kumbe wewe ni mwanamke tu na si mke au wewe ni mwanaume tu, kwa sababu ya urijali lakini si mume.

Kwa leo nafungashia virago hapa, tuonane wiki ijayo.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

ahsante sana ahsante mwandindishi wa makala haya.ni funzu zuri umetoa na kidogo nyongeze NDOA SI NDOANO, NDOA HAINA DOA.Kabla hamjafunga ndoa, muobeni mungu akupeni wake wema na mume mwema yeye peke ndo anayeweza kufanya hivyo maisha yako yote mueleke mungu wako yeye ndo suluhisho lako na msaada wako.

kila mtu kazaliwa na kupewa Baraka zake zote kwa mungu na ukiitaka kweli ndoa utaipata,kigezo chakwanza muombe mungu muachiye yeye na jambo la pili ni kwamba watu wafunge ndoa katika akili zao muwe mnawazo pamoja japokuwa ni watu wawili tafauti na jiulize kwa nini unapofunga ndoa unaambiwa nyinyi ni MWILI MMOJA,jiulize na tafakari neno hilo na je uko tayari kuwa MWILI MMOJA NA MWENZAKO?Tafakari hayo ujisha tafakari hayo basi NDOA NI KWA KILA MTU MWANAMKE NA MWANAMME WAMEUMBIWA KWENYE NDOA NA BARAKA ZA MUNGU HUTOKEA HUKO HUKO KWENYE NDOA.

Ahsante tena mwandishi kwa makala yako.

kutoka NY