Na Maryam Kidiko/Kijakazi Abdalla Maelezo Zanzibar
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilali amesema kuwa matumizi bora ya teknolojia ya habari yatawawezesha wanafunzi kupata elimu bora kwa urahisi.
Hayo ameyasema leo katika skuli ya Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi Unguja wakati wa uzinduzi wa darasa la kompyuta ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kutimiza miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kuwa matumizi bora ya kompyuta yatawafanya wanafunzi kuimarika vizuri kielimu wakati dunia hivi sasa imo katika mfumo wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya habari.
Alisema kuwa teknolojia ya habari imekuwa kwa kiwango kikubwa jambo ambalo limekuwa likichangia ukuaji wa uchumi katika Taifa.Amewashauri wanafunzi kutumia maendeleo ya teknolojia hiyo kwa mambo yanayoweza kuwasaidia katika maendeleo ya masomo yao na maisha ya baadae.
.
“Vijana itumieni teknolojia hii katika njia zilizosahihi ili iweze kuwaletea faida” alisema Dkt. Bilali. Amewataka wanafunzi waongeze bidii zaidi ili waweza kumudu masomo hayo na kuleta maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla .
Alisema kuwa matumizi ya komputa yanarahisisha kufundisha wanafunzi kwa njia rahisi na kuweza kujifunza mambo mbalimbali kupitia teknolojia hiyo na kupelekea kutanuka kiakili.
Aidha Dkt. Bilali ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa china kupitia kampuni ya ZTE kwa msaada wa kompyuta 50 na kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaenea kwa kiasi kikubwa. Dkt. Bilali amesema msaada huo utaweza kuleta changamoto zaidi kwa wanafunzi na kuwa na wataalamu wengi waliobora kwa maendeleo ya taifa
Amesema kuwa Serikali inathamini sana michango inayotolewa na marafiki wa maendeleo na Serikali itahakikisha michango hiyo inakuwa na faida kubwa kwa Taifa. Katika risala yao walimu wa skuli ya Kiembesamaki wameiomba Serikali kuwawekea Uzio katika Eneo la skuli pamoja na usafiri kwa walimu na Wanafunzi.
Skuli ya Kiembesamaki Sekondari inajumla ya Wanafunzi 1,800 kwa sasa na katika sherehe za uzinduzi huo Dkt. Bilal amechangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya maendeleo ya skuli hiyo.
IMETOLEWA NA IDARA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
1 comment:
napenda vazi lake kama la nyerere choline mjamaa wa kweli huyu.
Post a Comment