ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 6, 2015

Nyumba za mtuhumiwa ujambazi zachomwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda

Wananchi wa kata ya Igurubi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wameteketeza nyumba tano za mtu wanayemtuhumu kuwa jambazi.

Kufuatia kitendo hicho, wananchi hao sasa wamelazimika kuzikimbia nyumba zao kuhofia kukamatwa na Jeshi la Polisi ili mkono wa sheria uchukue mkondo wake.

AFISA MTENDAJI ANENA
Afisa Mtendaji wa Kata ya Igurubi, Mdeka Said, akizungumza na NIPASHE jana, alisema wananchi hao walichoma nyumba hizo zinazomilikiwa na Mahona Malendeja, mwishoni mwa mwaka jana baada ya kumtuhumu kuwa amekuwa akijihusisha na vitendo vya ujambazi.

Said alisema kuchomwa moto kwa nyumba hizo kumetokana na baadhi ya wananchi kukamatwa na polisi kufuatia tukio la kuchomwa nyumba za mtuhumiwa wa ujambazi mwishoni mwa mwaka jana.

Alifafanua kuwa kati ya nyumba zilizochomwa moto, mbili zimeezekwa kwa bati na tatu za tembe ambazo thamani yake haijajulikana.


Said aliwataja wananchi waliokamatwa na polisi kuwa ni Mbeshi Reuben, Shija Jilala, Ng’ombe Igoye, Masesa Pamba, Martin Charles, Lushuminkono Maige, Emmanuel Mwizamhindi na Mwandu Shusha.

KAULI YA DIWANI
Naye Diwani wa Kata ya Igurubi, Edson Sadani, alisema kitendo kilichofanywa na polisi cha kukamata wananchi hao siyo cha kiungwana kwa kuwa hawakushirikisha uongozi wowote wa kjiji wala kata.

Sadani alisema polisi wamekuwa na tabia ya kulinda wahalifu wanaosumbua katika kata hiyo na kusababisha wananchi kukosa imani na jeshi hilo ambalo lina jukumu la kulinda raia na mali zao.

MWENYEKITI AZUNGUMZA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwakwangu kilichopo kata hiyo, Luhende Swala, alisema polisi waliingia katika kitongoji chake bila kumtaarifu kiongozi yeyote na kuanza kuwakamata wananchi.

Swala alisema kufuatia tukio hilo, wananchi walishikwa na hasira na kujikusanya na kwenda kuchoma nyumba tatu za tembe za Malendeja na idadi ya nyumba zilizochomwa kufikia tano.

Alisema baada ya kuchoma nyumba hizo, kundi hilo la wananchi, lilielekea katika nyumba za baba mzazi wa mtuhumiwa wa ujambazi kwenda kuzichoma, lakini kabla ya kutekeleza lengo lao, polisi walifika eneo la tukio na kuanza kufyatua risasi za moto kuwatawanya.

Hata hivyo, akijibu tuhuma hizo akiwa katika Kituo cha Polisi Igunga, Malendeja alisema yeye si jambazi wala hajawahi kupatikana na shitaka lolote linalohusu ujambazi.

Alisema kilichosababisha nyumba zake kuchomwa moto na wananchi hao ni wivu wa kibiashara kwa kuwa yeye amekuwa mfanyabiashara mkubwa anayeuza mafuta ya petroli, dizeli, kununua ngozi na mazao mchanganyiko.

KAULI YA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda, alipoulizwa kuhusiana na tukio alisema yupo likizo na kutaka apigiwe simu Kaimu Kamanda.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Juma Bwire, alisema hajapewa taarifa na wasaidizi wake kuhusiana na tukio hilo.
 
SOURCE: NIPASHE

No comments: