Sunday, January 25, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA JESHI LA WANANCHI (JWTZ)




Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa kwa wananchi na Vyombo vya Habari kuhusu mgogoro wa eneo la TONDORONI lililopo katika Wilaya ya Kisarawe kama ilivyokaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari hapa nchini.
Taarifa zilizotolewa na kukaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari kwamba Wanajeshi wametumia nguvu kuwatoa wananchi eneo la TONDORONI na baadhi yao kudai kupotelewa na mali zao siyo za kweli na ni za kuwapotosha wananchi kwa sababu wananchi hao walitaarifiwa kuondoka kupitia uongozi wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B. Aidha, walipewa muda wa kutoa vitu vyao na wao kuondoka.
JWTZ linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa hatua ya kuwaondoa wananchi wavamizi kutoka katika eneo la kambi ya Jeshi kwa uangalifu, umakini na kulikuwa na usimamizi wa hali ya juu na hakuna mali ya mwananchi iliyoporwa kama ilivyodaiwa. Ifahamike kwamba; Jeshi linaona ni bora lilaumiwe kwa kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hatarishi ya jeshi ambayo hutumika katika mafunzo yanayohusisha risasi za moto, zana hatari za kijeshi na mabomu ambayo wakati mwingine hulipuka baada ya muda fulani kupita badala ya kuwaacha wakae katika maeneo hayo kutokana na sababu za kisiasa au ushabiki mwingineo na hivyo kuwa katika hatari ya kuweza kuumia vibaya au kupoteza maisha yao na mali zao.
Pia ni vema tukajua historia ya tatizo hili.
Mnamo mwaka 1978 eneo linalojumuisha vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B na kilichokuwa kijiji cha TONDORONI lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya JWTZ. Baada ya maamuzi hayo Kikosi cha JWTZ kilihamia TONDORONI mwaka 1981na kukalia eneo la hekta 4197. Serikali ililipima eneo la TONDORONI kisheria mwaka 1984 na eneo lote liliwekewa mawe ya mipaka.
Baada ya hapo, Serikali ilifanya tathimini ya malipo kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilikuwa mwaka 1987/88 na wakati huo kulikuwa na wananchi wapatao 1,508. Awamu ya pili ilifanyika 1992/93 ambayo ilijumuisha tathmini ya nyumba na majengo ambapo wananchi wengine 955 walifanyiwa tathimini.
Kufuatia tathimini iliyofanyika malipo yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwaka 1996 malipo yalifanyika kwa barua kumbukumbu Na. FE 98/371/01/73 ya tarehe 11 Juni 2003.
Malipo mengine yalifanyika mwaka 2002 na 2006. Baada ya Malipo hayo, mengine tena yalifanyika mwaka 2012 kutokana na kesi ya madai Na. 144/1996. Kwa hiyo madai ya msingi ya wananchi yalishalipwa na sheria ya uchukuaji ardhi imetekelezwa kikamilifu.

Hata hivyo, mwaka 2005 baadhi ya wananchi wachache walifungua kesi Na. 78/2005 ambayo baadae ilifutwa na mahakama. Tarehe 10 Dec 2013 M/kiti wa kamati ya Ulinzi ya Wilaya Kisarawe alikwenda eneo la TONDORONI kuwasomea wananchi maamuzi ya mahakama akiandamana na mwanasheria wa Wilaya ya Kisarawe.

Pamoja na taarifa hizo kupitia uongozi wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B. wananchi wachache wameendelea na kazi zinazochangia kuharibu mazingira hasa ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa na kuwasha moto mara kwa mara hali inayotishia usalama wa kambi na wa wananchi wenyewe ikizingatiwa kwamba hili ni eneo la mafunzo ambapo risasi za moto hutumika sambamba na zana zingine hatari za kijeshi katika eneo hilo.

Wananchi waliowengi wanajua ukweli kuwa eneo la TONDORONI linamilikiwa kihalali na JWTZ, lakini wapo wananchi wachache wamekuwa wakiingia kinyemela katika eneo hilo na kufanya ujenzi mpya usiku licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika kuwaelimisha na kuwashauri kuwa waache tabia hiyo ya kulivamia eneo hilo la Jeshi, jambo ambalo hugunduliwa na kuzuiliwa uendelezaji wa ujenzi huo.

Jeshi linawataka wananchi wachache wanaovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya kijeshi; kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria lakini pia kwa mara nyingine tena kuendelea kuwakumbusha wananchi kuhusu madhara yanayoweza kuwapata wananchi wanaovamia maeneo ya Jeshi na kujenga katika maeneo hayo.

Jeshi litaendelea kushirikiana na wananchi wema na kuheshimu mipaka iliyopo baina ya makambi yake na maeneo ya wananchi lakini pia litaendelea kuwaondoa wale wachache wanaojenga katika maeneo yake kinyume cha utaratibu.

Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano

Makao Makuu ya Jeshi, Upanga

No comments: