
Iringa. Ikiwa imebaki miezi tisa kabla ya Watanzania kufanya uamuzi wa kumpata Rais wa awamu ya tano, Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe ameitahadharisha CCM kwa kusema isipokuwa makini, upinzani utashinda katika Uchaguzi Mkuu.
Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe ni ya kwanza kutolewa na kiongozi mkubwa serikalini tangu kuanza kwa mwaka huu.
Dk Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana akiwa katika ofisi za CCM za Mkoa wa Iringa kabla ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake, ukiwamo Uwanja wa Ndege wa Nduli na kuzungumza na wadau wa usafiri.
“Tunaekelea kwenye uchaguzi, kama kawaida ya chama chochote kikubwa kilichotawala kwa muda mrefu, CCM tunajimaliza sisi wenyewe, lakini siyo kwa ajili ya utekelezaji,” alisema.
Alisema Serikali ya awamu ya nne imefanya mambo mengi ya maendeleo, ikiwamo kurahisisha usafiri na kuwainua kiuchumi wa wananchi na Taifa.
Dk Mwakyembe alitaja sababu zinazoweza kukifanya chama hicho tawala kupoteza kura nyingi katika uchaguzi huo kuwa ni migogoro ya ndani ya chama.
“Nimalize kwa kukitakia Chama cha Mapinduzi kazi njema, tujipange vizuri kwa Uchaguzi Mkuu ujao.
“Ndugu zangu, niseme kitu kimoja. Wenzetu wanajua namna ya kupata uongozi, ni rahisi sana kwa chama chetu kupotea katika ramani.
“Wenzetu wanapata uongozi kutokana na migogoro yetu wenyewe, sisi tunashikiana marungu, huku wapinzani wakipita katikati.
“Uchaguzi unaokuja ushindi wa wenzetu utakuwa mkubwa sana. CCM tusipotambua hilo, tutachapana makonde.
“Ukweli, siyo kitu cha kufurahisha sana... tunapika maharagwe yanachukua muda mrefu sana kuiva, tuko tayari hata kutumia kuni mbichi, yakikaribia kuiva tunaanza kubishana kuhusu kijiko, mwenzetu aliyekuwa hahusiki anakuja kula yote,” alisema.
Kauli ya Dk Mwakyembe imekuja huku baadhi ya makada wa chama hicho wakiwa tayari wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.
Katika hatua nyingine; Dk Mwakyembe aliwataka viongozi wa Mamlaka za Viwanja vya Ndege Iringa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushughulikia tatizo la wavamizi wa eneo la Uwanja wa Nduli.
“Hivi sasa Serikali ina miradi mingi sana, inajenga miundombinu ya miradi ya ndege ili watu wengi waweze kunufaika na huduma ya usafiri wa ndege, tumemaliza Uwanja wa Mpanda na Mafia. Sasa tupo katika ujenzi wa kiwanja cha Kigoma tunajenga jengo la abiria, kwa kuwa ni cha mpakani tumeamua kurefusha uwanja kufikia kilomita tatu.
“Tunaendelea na upanuzi wa Uwanja wa Mwanza utakaokuwa mkubwa kuliko vingine vya Afrika Mashariki, tunajiandaa kukarabati Uwanja wa Kia na Songwe,” alisema.
Kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Thomas Haule alisema Serikali imetenga Sh3.8 bilioni kwa ajili ya mradi wa upembuzi yakinifu kwa miradi 11 ya ujenzi wa viwanja hivyo. Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kufanya uchunguzi ili kubaini nyumba zilizojengwa ndani ya eneo la Uwanja wa Nduli. “Natoa wiki mbili, mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa uwe umefanya uchunguzi huo ili kama kuna ujenzi wa nyumba upigwe marufuku,” alisema.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment