Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.
Stori: Gabriel Ng’osha
BAADHI ya viongozi wa dini jijini Dar es Salaam, wametoa neno juu ya vurugu zilizofanywa wiki iliyopita na vijana wanaosadikika kuunda kundi linalojulikana kama Panya Road, Risasi Jumatano lina habari kamili.
Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa, aliliambia gazeti hili kuwa ukosefu wa ajira ni sehemu mojawapo inayozalisha makundi ya ajabu, hivyo serikali inapaswa kujipanga na kutengeneza mifumo ya ajira kwa vijana ili kuwaepusha kujiingiza katika makundi tishio na hatari.
“Hawa wanavamia, kupora na kuumiza watu ovyoovyo. Hata katibu mkuu wa mkoa wa Dar naye ni mhanga, alipotelewa na simu yake katika harakati za kuwakwepa hao wahuni, ukosefu wa ajira kwa vijana ni bomu kubwa na baya sana zaidi hata ya al shabbabi.”
Kwa upande wake, Mchungaji Ifrahimu Mwansasu wa Kanisa la Hosana Life Mission, alisema makundi hayo yanasababishwa na malezi mabaya ya kiimani na kitabia, kitu alichokiri hata yeye kuwahi kupitia akiwa kijana kabla ya kuokoka na kuitaka serikali ikae nao na kujua sababu ya wao kuwa kama walivyo.
“Yawezekana vijana wameingia bila kupenda kwa msukumo wa madawa ya kulevya, ugumu wa maisha na kadhalika, ila naamini katika roho wa kweli kwa Mungu kila kitu kinawezekana.”
Kundi la Panya Road, mwishoni mwa wiki iliyopita lilizua tafrani kubwa jijini Dar es Salaam baada ya kuwavamia, kuwapora na kuwajeruhi watu katika maeneo mbalimbali, lakini Jeshi la Polisi chini ya Kamanda Suleiman Kova lilifanikiwa kuwadhibiti.
1 comment:
wakawafuate wabunge wa ccm huko bungeni na huko ikulu wakawafanyia balaa lao mafisadi wenzao.
Post a Comment