ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 26, 2015

WANDISHI WA HABARI MBEYA WAPATIWA MAFUNZO

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Profesa Norman Sigallah, akifungua mafunzo ya Utekelezaji wa adhabu mbadala kwa wafungwa kwa Waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya yaliyotolewa na Wizara ya Mambo ya ndani katika Hoteli ya Gr Soweto jijini Mbeya.
Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Probesheni na huduma kwa jamii, Charles Nsanze, akimkaribisha mgeni rasmi
Waandishi wa habari wakiwa makini kumsikiliza mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo juu ya adhabu mbadala kwa wafungwa
Kwa picha zaidi bofya soma zaidi
Baadhi ya wawezeshaji katika mafunzo hayo
Baadhi ya wawezeshaji katika mafunzo hayo
Mr. Kawawa Mgungu (Senior Probation Officer) akiwasilisha mada katika mafunzo kwa Wanahabari.
Washiriki wa Mafunzo wakiwa ukumbini kuendelea na mafunzo hayo.
Picha ya pamoja

WAANDISHI wa habari mkoani Mbeya wametakiwa kuisaidia Serikali katika kuihamasisha jamii kuhusu uwepo na utekelezaji wa adhabu mbadala kwa wafungwa.

Aidha imeelezwa kuwa jamii pia imetakiwa kuupokea na kuutekeleza mpango wa adhabu mbadala kwa wafungwa kutokana na mpango huo kuiondolea serikali gharama kubwa ya kuwahudumia waharifu badala yake mharifu ndiye anayeihudumia jamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Profesa Norman Sigallah, alipokuwa akifungua mafunzo ya Utekelezaji wa adhabu mbadala kwa wafungwa kwa Waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya yaliyotolewa na Wizara ya Mambo ya ndani katika Hoteli ya Gr Soweto jijini Mbeya.

Profesa Sigalla alisema adhabu mbadala kwa wafungwa kutaisaidia jamii na serikali kupunguza gharama ambazo zinatolewa kuwahudumia wafungwa pamoja na Askari wanaowahudumia kwa kulipia chakula na mishahara hivyo kupitia adhabu mbadala mharifu huifanyia kazi jamii katika kutekeleza adhabu yake.

Aliongeza kuwa Adhabu mbadala ni suala geni katika jamii hivyo kupitia mafunzo kwa Waandishi wa habari yatasaidia jamii nzima kuelewa na kuipokea ikiwa ni pamoja na kutekeleza zoezi hilo pindi litakapoanza kutekelezwa kwa kupunguza wafungwa magerezani.

Alisema pia adhabu mbadala ikianza kutekelezwa itaisaidia jamii kwa kuwa itakuwa ikimuona mharifu akiwa anafanya adhabu yake pamoja na mharifu kujutia adhabu yake kutokana na kuifanya hadharani ambapo kila mwananchi anaweza kupita na kumuana hivyo kila mwanajamii kushiriki katika usimamizi.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Probesheni na huduma kwa jamii, Charles Nsanze, alisema Wizara ilipata msaada wa fedha kutoka shirika la Penal reform international la nchini Uingereza kwa ajili ya mafunzo ya utekelezaji wa adhabu mbadala kwa nchi za Afrika Mashariki.

Alisema Wizara ilichagua Mkoa wa Mbeya kutekeleza mradi huo kutokana na kukua kwa Jiji la Mbeya na ongezeko la uhalifu ambao unaweza kupelekea kuwa na msongamano wa wafungwa magerezani hivyo njia ya kunusuru hali hiyo ni kutoa mafunzo kwa wanahabari ili kuijulisha jamii kuhusu adhabu mbadala.

Nsanze aliongeza kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo kwa wanahabari ni kuutarifu umma mzima juu ya uwepo wa adhabu mbadala itakayosaidia kupunguza wafungwa wasio na ulazima wa kutumia vifungo wakiwa magereza, kuongeza idadi kubwa ya wafungwa walio nje ya vifungo pamoja na kutii sheria za mahakama.

Alisema mbali na mafunzo hayo kutolewa kwa wanahabari pia yatatolewa kwa Mahakimu wote Mkoa wa Mbeya, wasimamizi wa wafungwa magerezani na wadau mbali mbali wakiwemo waendesha mashtaka, mawakili, Polisi na askari magereza ambao watapewa mafunzo hayo katika awamu tofauti.

Aliongeza kuwa lengo la Idara hiyo ni kuishirikisha jamii na wafungwa katika utekelezaji wa adhabu mbadala na kuwarudisha wafungwa katika jamii wakiwa salama na kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

Alisema faida ya adhabu mbadala kwa wafungwa itamsaidia kuendelea kutumikia adhabu huku akiendelea kuhudumia familia yake kuliko angekaa gerezani, kuepuka kunyoshewa vidole na jamii kutokana na kutokuwa kwenye mavazi maalumu na kutekeleza adhabu yake kwa kujichanganya na jamii nyingine.


Na Mbeya yetu

No comments: