ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 14, 2015

Bei ya umeme yashuka kwa Sh8

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu bei ya umeme. Kulia ni Kaimu Mgurugenzi- Umeme, Injinia Godfrey Chibulunje. Picha na Anthony Siame

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeliagiza Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kupunguza bei za umeme kwa Sh8 kuanzia Machi Mosi mwaka huu.
Akitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema kutokana na mabadiliko kwenye bei ya mafuta, thamani ya shilingi na mfumuko wa bei, gharama za kununua umeme zinatakiwa zishuke kwa asilimia 2.21.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Tanesco jana, Felchesmi Mramba simu yake ilikuwa ikiita lakini baadaye ilikatwa na hata alipotafutwa kwa mara nyingine, hali ilikuwa hivyo.
Mmoja wa maofisa wa Tanesco ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema kuwa mara zote wanapopata agizo la Ewura, kinachofuata ni utekelezaji. “Huwa ni kutekeleza, hatuna ubishi kwa hilo,” alisema.
Taarifa ya Ewura
Akifafanua, Ngamlagosi alisema wateja wenye matumizi ya kawaida, bei ya umeme itashuka kutoka Sh306 kwa uniti hadi Sh298 kwa uniti sawa na punguzo hilo la Sh8 kwa uniti moja.
Mwananchi anayenunua umeme wa Sh10, 000 anapata uniti 32.6 hivi sasa, lakini baada ya punguzo hilo kwa fedha hiyo hiyo atapata uniti 33.5. Marekebisho hayo ni kwa bei ya kununua uniti ya umeme na siyo kwa tozo za mwezi za utoaji huduma.
“Wateja wenye biashara ndogo ndogo ambao wapo kwenye kundi la T2 wao bei zitashuka kwa Sh5, wateja wa viwanda vya kati bei zitashuka kwa Sh4, wakati wateja wa viwanda vikubwa na migodi likiwemo Shirika la Umeme Zanzibar wao bei itashuka Sh3 kwa kila uniti moja,” alisema Ngamlagosi.
Hata hivyo, alisema wateja wanaotumia umeme chini ya uniti 75 kwa mwezi ambao hununua uniti moja kwa Sh100 hawatanufaika na punguzo hilo kwa kuwa wanapata ruzuku kutoka kwa wateja wakubwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchumi, Ewura, Msafiri Mtepa, alisema wateja wengi wanaonunua umeme wapo katika kundi la pili ambalo hutumia zaidi ya uniti 75 kwa mwezi na kwamba wao ndio watakaonufaika zaidi na punguzo hilo. “Wateja wanaonunua umeme chini ya uniti 75 kwa mwezi wapo chini ya laki mbili tu nchini,” alisema Mtepa.Kuhusu kanuni zilizotumika kufanya mabadiliko ya bei, Ngamlagosi alisema sheria ya umeme inaagiza bei kupitiwa upya kila baada ya miezi mitatu ili kupunguza ongezeko au punguzo kubwa kwa wakati mmoja ambalo linaweza kuleta mshituko mkubwa kwenye uchumi. “Unapofika kwenye mabadiliko makubwa ya bei hayawi yale wanayoumiza wananchi au Tanesco kwa kiwango kikubwa,” alisema Ngamlagosi.
Pia, mkurugenzi huyo alisema kuwa mradi mkubwa wa gesi unaotarajiwa kukamilika mwaka huu utakapokamilika utapunguza kwa kiwango kikubwa gharama za kuzalisha umeme nchini.
“Mitambo yote ya dizeli na mafuta ya ndege ambayo Tanesco sasa hivi wanaitumia na wazalishaji binafsi wanaitumia, maana yake itabadilishwa sasa itumie gesi badala ya mafuta,” alisema.
Aliongeza kuwa mwaka huu mitambo yote ya dharura ya umeme inatarajiwa kuondolewa nchini na hivyo kuipunguzia gharama Tanesco ya kuilipia jambo litakalosaidia kushuka kwa bei za umeme.
Baada ya gesi kuanza kutumika, Ewura itafanya utafiti mwingine kuhusu gharama halisi ya kuzalisha kutokana na mabadiliko makubwa yatakayokuwa yametokea.
Desemba 10, 2013 Bodi ya Wakurugenzi wa Uwura ilitoa agizo la mabadiliko ya bei za umeme unaotozwa na Tanesco kwa kipindi cha miaka mitatu, ambapo bei za sasa zilianza kutumika Januari Mosi 2014.
Baada ya Ewura kupitia gharama hizo mwaka 2014, ilibaini kuwa bei ya mafuta mazito ya kuendesha maitambo iliongezeka kati ya Januari na Julai kutoka Sh2, 273 mpaka Sh2, 312 sawa na asilimia 35. Hata hivyo, kutoka Agosti bei hiyo ilishuka na kufikia Sh2, 099 Desemba.
Pia, katika mwaka huo Tanesco ilikadiriwa kuwa ingezalisha na kununua umeme wa kiasi cha uniti milioni 5,561.39 kutoka katika vyanzo vya mitambo ya mafuta na gesi asilia. Ewura ilibaini kuwa uniti zilizozalishwa na Tanesco pamoja na zile zilizonunuliwa kutoka kwa kampuni binafsi zilifikia milioni 3,674.93, sawa na punguzo la asilimia 29 ikilinganishwa na makadirio.
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika alisema uamuzi uliochukuliwa na Serikali umechelewa kwa sababu bei ya mafuta kwenye soko la dunia ilishuka muda mrefu. Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho kutoka Kituo cha Haki na Sheria (LHRC), Harold Sungusia alisema wananchi hawapaswi kufurahia punguzo hilo kwa sababu hawajui kiasi gani cha fedha kimepotea tangu bei ya mafuta iliposhuka kwenye soko la dunia.
“Tunaweza kufurahi halafu ikaja bei kupanda ghafla,” alisema Sungusia.
Mfanyabiashara wa chipsi katika Kijitonyama, Alois Mushi alisema serikali imejibu kilio cha wananchi waliokuwa wanataka bei ya umeme na nauli zishuke kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. “Tunashukuru wamesikiliza kilio chetu, japokuwa hadi watu walalamike ndiyo wanasikiliza, sasa tunasubiri nauli nazo lazima zishuke,” alisema Mushi.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Kuna uvumi kuwa umeme umepanda kwa kiwango kile ulichoshuka ni kweli?