ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 23, 2015

Mbowe aibua mapya mfumo wa BVR.

Asema mtaalamu alionya Tanzania haijawa tayari, Usajili ukiendelea utasababisha machafuko ya kisiasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amedai kuibua nyaraka zinazoonyesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ilishauriwa na mtaalamu wa mashine za BVR kutoka Marekani kuwa Tanzania haijawa tayari kwa teknolojia hiyo.

Akifungua kikao cha baraza la uongozi wa chama hicho Kanda za Nyanda za Juu Kusini jana alisema, Mshauri Mwelekezi kutoka Marekani Darell Geusz ambaye ni mtaalam wa mashine za usajili wa wapiga kura kutumia mfumo wa kieletroniki (BVR) alichukuliwa kuishauri Tume kuhusu mashine hizo.

Alisema nyaraka hizo zinaonyesha ushauri uliotolewa na mtaalam huyo kwa Tume ni kuwa Tanzania haijawa tayari kwa teknolojia hiyo kwa sababu hakuna vifaa, utaalam na wataalam.

“Mtaalamu huyo alishauri wakilazimisha kuendelea kuzitumia mashine hizo watasababisha machafuko ya kisiasa nchini,” alisema.

Mbowe pia alitoa nyaraka nyingine zinazoonyesha jinsi Nec imekuwa ikiandaa kwa siri utaratibu wa BVR bila kuwashirikisha wadau.



Wakati Mbowe akiibua madai hayo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Tanzania Bara), John Mnyika, alisema kauli ya Jaji Mstaafu Damian Lubuva dhidi ya viongozi wa siasa aliyoitoa juzi imelenga kufunika kombe mwanaharamu apite.

Juzi Jaji Lubuva aliwaasa viongozi wa siasa kutotumia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kama mwanya wa kuanzisha fujo.

Mnyika alisema Chadema hakitanyamaza bali kitaendelea kutaka upungufu katika mashine za BVR kufanyiwa kazi.

Alisema chama chake kimenasa taarifa za mawasiliano kati ya Tume na Taasisi ijulikanayo kama, IPSITI zikionyesha kwamba Nec haijafanya marekebisho ya mapungufu yaliyopo kwenye BVR.

Alisema serikali hususan Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anapaswa kujitokeza hadharani kuelezea sababu za kutoshughulikia upungufu ulio onekana licha ya ripoti ya wataalam kubainisha.

Pia alisema Pinda anapaswa kuueleza umma sababu za serikali kutotoa fedha kamili kwa Tume hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wapiga kura.

“Pinda awaeleze Watanzania ukweli kuwa Serikali haina fedha kwa sababu wahisani walisitisha misaada ya kibajeti, hii ilitokana na kashfa za ufisadi wa kifedha,” alisema na kuongeza:

“Wahisani walisitisha fedha za misaada ya kibajeti kabla ya bunge halijafikia maamuzi ya sakata la Akaunti ya Escrow, misaada mingine iliyositishwa inahusu sekta ya maji na afya, ndiyo maana miradi mingi kwenye Halmashauri sasa haisongi mbele,” alisema.

Mnyika alisema mkutano ujao wa bunge wataenda kuyaeleza kwa kina kuhusu misaada hiyo ya maji na afya iliyositishwa.

“Leo tunapata madhara syo tu miradi ya kimaendeleo kukwama, wananchi wanakosa huduma muhimu za afya na maji kwa sababu ya fedha kutumika kwenye mianya ya ufisadi badala ya maendeleo,) “ alisema na kuongeza:

“Ukosefu huu wa fedha umeathiri pia tume katika zoezi muhimu kwa ajili ya uchaguzi utakaowawezesha Watanzania kupata viongozi bora na kuzuia mianya ya ufisadi,” alisema.

Alisema kitendo cha Jaji Lubuva kuvinyamazisha vyama vya siasa wakati BVR zina upungufu ni sawa na funika kombe mwanaharamu apite.

Mnyika alisema chama chake kitaendelea kuzungumzia udhaifu na upungufu huo ambao mwisho unaweza kusababisha watu kuandikishwa zaidi ya mara moja.

Alisema endapo watanyamaza nchi itaingia katika machafuko kwa kuwa upungufu uliopo kwenye mashine hizo ni mkubwa.

“Kuacha kujadili suala hili nchi itaingia katika hasara ya kutumia fedha kwenye uandikishaji wakati huo, hii ni kuruhusu mianya ya uchakachuaji wa uchaguzi na kusababisha kutokuwa huru na haki,” alisema.

Aidha chama hicho kimeonyesha wasiwasi wa kutokamilika kwa zoezi la uandikishaji mwezi Aprili 30 kama ilivyotakiwa kutokana na siku ambazo zitakazotumika kila mkoa.

“Lubuva amesema Njombe watatumia siku 28 wasiwasi wetu ni kwamba ikiwa siku hizi zitatumika na maeneo mengine, itafika Aprili 30, baadhi ya maeneo yatakuwa hayajakamilisha zoezi,” alisema.

Aidha, kutokana na wasiwasi huo, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete asogeze mbele hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika ndipo lifanyike.

Pia Mnyika amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda aeleze lini kamati ya bunge itakutana na Tume ili kuepusha nchi kuingia katika machafuko.

Kuhusu kauli ya Tume ya kuvitaka vyama vya siasa kusaidia kutoa elimu uandikishaji kwa wananchi, Mnyika alisema chama chake kimeitikia wito huo na kina kusudia kwenda mkoani Njombe kuzindua kampeni ya elimu ya mpiga kura maarufu kama ‘R to R BVR’ ikimaanisha Region to Region BVR. Hata hivyo, alisema baada ya kupeleka taarifa jeshi la polisi kuhusiana na mkutano wa uzinduzi huo, wamekataliwa kufanya hivyo kwa maelezo kuwa kutakuwa na zoezi la uandikishaji huo.

Alisema licha ya polisi kuzuia lakini wataendelea na zoezi hilo na kumtaka Mkuu wa jeshi hilo awaagize polisi kupokea mikutano hiyo ambayo imekusudiwa kufanyika kila mkoa.

No comments: