Advertisements

Saturday, February 28, 2015

Mbowe atoa ushahidi kesi ya shambulio.


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (53), anayekabiliwa na kesi ya shambulio dhidi ya mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ameileza mahakama kwamba alilazimika kumtoa nje kwa nguvu nje ya kituo cha kura, Nasir Uronu, kwa madai kuwa alikuwa na utambulisho bandia ambao hautambuliki na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) isipokuwa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Akitoa ushahidi jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa, aliiambia mahakama kuwa uamuzi wake ulitokana na mwongozo wa barua elekezi iliyotolewa na NEC, ikiwataja waangalizi halali walioruhusiwa kuingia ndani ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi huo, kuwa ni Jumuiya ya Ulaya (EU), Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) na Kamati ya Waangalizi wa Uchaguzi Tanzania (Temco).

“Nilipata taarifa kutoka kwa mgombea udiwani wa kata ya Machame Kaskazini (Chadema), Clement Kwayu kwamba kuna waangalizi watatu wa Bakwata katika vituo vilivyopo Nshara wakati hawajatajwa kwenye barua ya mwongozo.

Nilifika pale na nilipomtaka ajitambulishe alikaidi na nikamtoa nje na wale wenzake wawili wakakimbilia kusikojulikana…Nilipompigia simu Msimamizi wa Uchaguzi, Meleckzedeck Humbe alisema hajapata taarifa na hamfahamu,” alidai Mbowe.

Aliendelea kudai, kwamba kama ni kweli alimpiga makofi mawili Uronu, mbona hakuna msimamizi wa uchaguzi wala wakala yeyote aliyeitwa mahakamani kutoa ushahidi wa kuthibitisha alimpiga mtu anayejiita mwanaglizi wa ndani wa Bakwata.

“Mashtaka haya dhidi yangu ni ya kupika, kwa sababu hata ushahidi uliotolewa mahakamani ni wa kuungaunga na unatia shaka.

Kimsingi sijawahi kumpiga kijana huyu ndani wala nje ya kituo, kwa sababu vituo vyote vilikuwa vina ulinzi wa kutosha, ningekamatwa kwa kosa hilo,” alidai Mbowe.

Katika uchaguzi huo, Mbowe alikuwa mgombea ubunge wa jimbo la Hai kwa tiketi ya Chadema. Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mpelembwa anayesikiliza kesi hiyo, alisema mahakama hiyo imeusikiliza kwa makini maelezo ya shahidi huyo na mahakama hiyo ina ahirisha shauri hilo hadi Machi 20, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Mbowe ambaye anatetewa na mawakili wawili, Albert Msando na Rajab Issa, anadaiwa kumshambulia kwa kipigo Uronu akiwa katika zahanati ya Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kaskazini, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo, katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi katika uchaguzi huo wa ubunge jimbo la Hai kwa kupata kura 28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM), kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.

Nje ya mahakama, Mbowe alikuwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) Salum Mwalimu huku mahakama hiyo ikiwa imezungukwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya chama hicho.
CHANZO: NIPASHE

No comments: