Advertisements

Friday, February 13, 2015

NATAFUTA KAZI NIMNADI RAIS AJAYE!

UCHAGUZI Mkuu wa tano wa Tanzania katika mfumo wa vyama vingi vya siasa unatazamiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. Ingawa haijafahamika tarehe wala ni nani hasa atapewa nafasi hiyo ya kumrithi Jakaya Kikwete, angalau majina kadhaa yanatajwa, kutoka kambi zote.
Wapo wanaotajwa kutoka CCM na kambi ya upinzani kwa ujumla wao, ambao kwa jinsi tunavyoendelea, ni wazi kuwa watawakilishwa na mgombea kutoka kundi la Ukawa. Kiuhalisia, hawa ndiyo wapinzani wakubwa wa chama tawala, kwa sababu walio nje ya umoja huu, hawana nguvu.

Wote tunajua, kila mmoja anajipanga katika kundi analoamini litashinda. Kuna rafiki yangu mmoja huwa ananipigia kelele kila siku, akiniambia nisimame nihesabiwe, nisije sema sikuambiwa. Nabakia kucheka tu.
Mimi siyo mtu wa kusimama kinyonge na kuombea kudura za kuhesabiwa. Ninaamini nina mchango mkubwa wa kuutoa kwa mtu atakayenipa kazi ya kumnadi katika harakati zake za kuelekea magogoni, lakini sharti tukubaliane.

Siwezi kuwa kama wale wapiga mbinja wanaotegemea bahati nasibu.
Kama nilivyosema mwanzo, wagombea watakaoshinda urais, kwa maoni yangu, watatokea CCM au Ukawa, ingawa kwa uzoefu wa jinsi chaguzi zetu zinavyoendeshwa, chama tawala kina nafasi kubwa ya kushinda katika nafasi hii. Kwa maana hiyo, ajira hii ninaitafuta, kwanza kabisa kutoka CCM, lakini wakiona sina vigezo, basi hata mgombea wa Ukawa nitamfanyia kazi.

Ili niwe katika kiwango huru cha kumnadi mgombea urais atakayehitaji huduma yangu, ni lazima nimpe masharti ambayo anapaswa kukubaliana nayo, vinginevyo, aniache kwa sababu nitamfanyia kampeni yeyote nitakayeona anafaa wakati ukifika.

Sharti la kwanza kabisa analopaswa kukubaliana nalo ni kunishawishi kwa hoja kuwa kweli yeye anafaa kuwa kiongozi wa taifa hili. Na ushawishi huo, hautategemea kiasi gani cha fedha atanipatia, bali mbinu gani atatumia ili kuwanusuru mamilioni ya Watanzania na maisha duni wanayoishi.

Nisipokubaliana na mbinu zake, aniache. Hii ni kwa sababu nikiweka kigezo cha fedha atakazonilipa, sitakuwa nimetoa mchango kwa taifa langu kwa sababu mimi sihitaji fedha zaidi ya hizi zinazoniwezesha kuishi hivi ninavyoishi.

Ingawa wao mamilionea wananiona mimi hohehahe, lakini nina uhakika mamilioni ya wananchi wanaishi duni kuliko mimi. Hao ndiyo ninaotaka na wenyewe wainuke angalau wafikie hapa nilipo. Na hawa hawawezi kuinuliwa kwa kuongopewa, watainuliwa kwa kuambiwa ukweli wa mbinu za kubadili maisha yao, kwa sababu wakiziafiki, watashiriki kujiinua!

Kwa hiyo hilo ndilo sharti langu la kwanza. Nipe hoja nizikubali, kama unadhani nitafanya kazi hiyo kwa fedha, count me out!La pili, ambalo pia ni muhimu sana, sitatumika kumchafua mgombea mwingine. Sioni faida ya kufanya hivyo kwa sababu kama nitakuwa nimesharidhika na mikakati yake, hakuna hata sababu ya kuhangaika na wapinzani wake, wa nini sasa wakati tutawamaliza kwa hoja tu? Kwa hiyo akija mtu na kuniambia kazi yangu pia itajumuisha na kumtukana, kumzushia, kumkejeli na kumdhalilisha mpinzani, mie asinihesabie kabisa.

Ningeweza kutaja sifa zingine ambazo wanaonitaka niwe mpiga debe wao walipaswa kuzijua, lakini hizi ndizo kubwa, kwa sababu zingine zitakuwa zinaingia katika vifungu vidogo vidogo, kama vya uadilifu, uzalendo, uucha Mungu na nyinginezo.

Kuhusu uwezo wangu kwa kazi hizo, wala wasiwe na hofu, kwa sababu ninao ufahamu mkubwa mno wa matatizo ya wananchi, kwa vile hata mimi nakumbana nayo. Kwa hiyo nitakapomwambia bosi wangu kuhusu tatizo la afya, elimu, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kero zingine za watu, ajue ninazifahamu na nimeshaunguzwa nazo!Ninawakaribisha sana waheshimiwa wagombea, hasa kutoka CCM!
SOURCE:GPL

No comments: