Moshi. Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo ana siku 72 za kuamua kugombea tena kiti hicho au la, ili kupisha wanachama wengine watangaze nia.
Ndesamburo anaonekana yuko njiapanda kutoa uamuzi, huku taarifa zilizozagaa zinadai kwamba hagombei tena.
Mbunge huyo ni miongoni mwa wabunge wakongwe wa upinzani, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1991.
Ndesamburo ambaye amekuwa mbunge kwa vipindi vitatu vya kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, alipotafutwa jana kuzungumzia tetesi hizo alisema: “Wakati ukifika nitasema kama nagombea au sigombei.”
Kutokana na kuzagaa kwa taarifa hizo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kinadaiwa kusubiri kwa hamu tamko la Ndesamburo, ambaye amekisumbua chama hicho kwa miaka 15 mfululizo.
Katibu wa Chadema, Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alikiri kuwapo kwa minong’ono ya Ndesamburo kutogombea, lakini akasema Katiba inamruhusu kuomba tena kuteuliwa na chama kugombea.
“Katiba inasema jimbo lenye Mbunge wa Chadema halitangazwi nia ya kugombea hadi Aprili 30 ya mwaka wa uchaguzi. Bado tuna takriban siku 30 kabla ya wengine kutangaza. Lakini wanachama wote wana haki ya kugombea sambamba na Ndesamburo,” alisisitiza Lema.
Kigugumizi hicho cha Ndesamburo kinaonekana kuwavuruga wanachama wa Chadema wenye nia ya kugombea, wakisema kama angeweka wazi, wagombea wangeanza kujipima nguvu.
Hata hivyo, wakati Chadema ikitoa kauli hiyo, CCM imetamba kuweka mgombea bora na mwenye sifa.
Tayari makada wawili wa CCM wameonyesha nia ya kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.
Katibu Mwenezi wa CCM Moshi Mjini, Priscus Tarimo alisema chama hicho kimejipanga kukabiliana na mgombea yeyote atakayeteuliwa na Chadema.
“Sisi tunasikia kwamba Mzee Ndesa (Ndesamburo) hatagombea tena, lakini huu ni uvumi ila sisi tumejipanga safari hii na tayari kuna makada wetu wameshatangaza nia chinichini,” alisema.
Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, alianza mageuzi miaka ya 1990 akiwa miongoni mwa wanachama wa mwanzo wa Chadema, akiwa na kadi namba 10.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment