Januari 28, mwaka huu, Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa hiyo, Leo Mapunda, aliwaandikia barua wakuu wa shule za sekondari za wavulana na wasichana Songea, Matogoro, Mashujaa, Matarawe na Mfanyakazi, akiwaelekeza kuwa wanafunzi na walimu wote wanapaswa kuhudhuria sherehe za CCM zilizokuwa zinafanyika kitaifa mkoani humo katika Manispaa ya Songea.
Wabunge walihoji suala hilo kutokana na madai kwamba, serikali ndani na nje ya Bunge imekuwa ikitoa kauli za kuwazuia viongozi na wanasiasa kuwatumia wanafunzi kushiriki katika masuala ya siasa, hasa katika vyuo na shule. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Suzan Lyimo, alisema hayo kupitia swali lake la msingi wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu, bungeni jana.
Alisema kitendo hicho kilifanywa katika maadhimisho hayo na Mkuu wa Mkoa huo, Said Mwambungu na viongozi wengine wa mkoa, huku wakitambua umuhimu wa elimu na watoto hao ni wanafunzi wa shule ya msingi, ambao hawajawa na maamuzi ya chama wanachokitaka.
"Mheshimiwa waziri mkuu, unatambua umuhimu wa elimu, lakini vilevile Chama Cha Mapinduzi mnadai kwamba mna wanachama zaidi ya milioni 10. Je, ni kwanini msitumie wanachama wenu kwenye sherehe hizo?" Alihoji Suzan.
Aliongeza: "Mnaenda kutumia wanafunzi tena wa shule za msingi ambao hawajawa na maamuzi ya chama gani wanakitaka?"
Akijibu, Pinda alisema alijua kuwa swali hilo lazima lingeulizwa.
Hata hivyo, alisema ‘mtoto wa nyoka ni nyoka’ na kufafanua kuwa CCM ina mfumo wake, ambao umeshuka mpaka kwenye ngazi ya chipukizi.
"Kwa hiyo, chipukizi hawa ni watoto, ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana CCM. Ndiyo maana chama kiliwatumia ilikuwa nzuri na ilipendeza sana," alisema Pinda.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa watoto hao hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, kama alivyosema Suzan, suala la ushiriki wao katika maadhimisho hayo, halina madhara.
"Kwa sababu bado ni wadogo mno. Wao walichokuwa wanafurahia pale ni ile paredi na kuonekana wamepiga sare ile basi.
Kwa hiyo, sisi wengine tuliokuwa pale tulifikiri ni jambo zuri sana," alisema Pinda.
Pamoja na majibu hayo, Suzan alisimama na kuuliza swali la nyongeza akisema amesikitishwa na majibu ya waziri mkuu, ambaye ni kiongozi mkuu wa shughuli za serikali bungeni anayepaswa kusimamia utawala bora.
Alisema pamoja na kwamba, watoto hao ni wadogo, waziri mkuu anatambua kwamba baadhi, wazazi wao ni wa vyama vya upinzani.
"Ni kwa nini kuwe na double standard (undumilakuwili) wakati watoto hawa lengo lao ni kusoma na siyo kufanya siasa?" Alihoji Suzan.
Akijibu swali hilo, Pinda alitaka CCM iachwe kuendelea na utaratibu wake wa chipukizi na kwamba, haoni kama kuna tatizo kubwa kwa sababu mfumo huo ndivyo ulivyo kwenye chama hicho.
"Sasa tukisema tuanze leo kubishana juu ya jambo hili sidhani kama itakuwa ni halali," alisema Pinda.
Naye Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, aliomba mwongozo wa spika, akisema majibu ya waziri mkuu yamekiuka haki za binadamu kwa kuwa yanalazimisha wanafunzi kushiriki shughuli za kisiasa.
Alisema wanazo barua, ambazo mkuu wa mkoa huo alimwandikia ofisa elimu kuwalazimisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana na Wavulana ya Songea kuvaa sare za CCM na walimu waende kwenye maadhimisho hayo kwa lazima.
"Sasa hili jambo ni kinyume cha haki za binadamu na ni kinyume kwa nchi, ambayo inafuata mifumo ya kidemokrasia. Huwezi kuwalazimisha watu...sasa mwongozo wangu ni kwamba, waziri mkuu afute kauli yake," alisema Mkosamali.
Akijibu, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimtaka Mkosamali kama alichokiomba ni mwongozo, amri au au ushauri na kujibiwa na mbunge huyo kuwa ni mwongozo akitaka waziri mkuu aende bungeni kufuta kauli yake ili watu wasilazimishwe kufanya shughuli za kisiasa wakiwa watoto.
Hata hivyo, Spika Makinda alisema: "Mwongozo wangu, usimlazimishe (waziri mkuu)."
Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba, alisema waliambiwa waombe wenyewe na upenzi wao na baada ya jioni kutoka shule ndiyo walifanya gwaride lao siyo wakati wa kazi na kwamba, hata maadhimisho hayo yalifanyika Jumapili, ambayo siyo siku ya kazi.
Alisema hayo wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na ile ya Maendeleo ya Jamii kuhusu utekelezaji wa kazi zake kwa kipindi cha Januari 2014 hadi Januari 2015, bungeni jana.
Hali hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa Bunge, Kidawa Khamisi, kuingilia kati na kumtaka Komba ajikite katika kuchangia hoja iliyokuwa mezani wakati huo.
Hata hivyo, Komba alisema alichokuwa akikifanya ni kujibu kwanza suala hilo ili lisilete mchanganyiko.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Christowaja Mtinda, alisema elimu nchini inafanya kazi kwa kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa na nchi, hivyo walimu na wanafunzi hawaruhusiwi na wala hawana ruhusa ya kushiriki katika sherehe za chama chochote cha siasa.
Mtinda alisema kuna barua iliyotoka kwa Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenda kwa wakuu wa shule za sekondari za Songea Boys, Songea Girls, Matongoro, Mashujaa, Matarawe na Mfaranyaki.
Barua hiyo ambayo NIPASHE imeiona, yenye kichwa cha habari "Yah: Walimu na wanafunzi kuhudhuria sherehe za CCM kitaifa Uwanja wa Majimaji tarehe 1/02/2015", yenye kumbukumbu Na. SO/MC/E.10/4/51 ya Januari 28, mwaka huu, iliyosainiwa na Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Songea, Leo Mapunda.
Mtinda alisema katika barua hiyo, Mapunda anawaeleza walimu, watumishi, wasio walimu na wanafunzi kwamba, "sote lazima kuhudhuria."
"Hii haikubaliki wala hatuwezi kuifurahia jambo hili. Ni uvunjaji wa katiba ya nchi, haikubaliki hata siku moja. Ndiyo maana wanafunzi wa shule za sekondari na shule za msingi za serikali wanafeli," alisema
Alisema suala hilo linahitaji kufanyiwa uchunguzi na tafakuri ya hali ya juu na kumweleza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na naibu wake kwamba, hawataki kulisikia tena jambo hilo.
Mtinda alisema pia hoja ya kuwapeleka wanafunzi kwenye shughuli za kisiasa baada ya muda wa masomo siyo sahihi, kwani baada ya masomo mwanafunzi anatakiwa kufanya majukumu ya kimasomo na kupumzika.
Alisema sera ya elimu inasema kwamba, mwanafunzi asome siku 196 kwa mwaka, hizo ni baada ya kuondoa siku za sikukuu, likizo zao fupi na ndefu na Jumamosi na Jumapili.
"Siku 196 mwanafunzi anatakiwa awe darasani anasoma. Siku za mapumziko anatakiwa afanye assignments (majukumu za kimasomo), afue nguo zake, apumzike, aende kwenye michezo, refresh, siyo kwenda kwenye sherehe za kisiasa. Chama Cha Mapinduzi kinaaibisha sera ya elimu na elimu nchini," alisema Mtinda.
Suzan akichangia mjadala huo, alisema wanafunzi wanapokuwa shuleni Jumamosi au Jumapili, maana yake wanajiandaa kwa programu mbalimbali, hivyo haijapangwa siku hizo kupumzika kwa maana kwamba, kutokusoma.
Alisema mfumo wa elimu nchini umeporomoka na elimu yenyewe imeporomoka na kwamba, aliyeiporomosha ni serikali kwa kuhakikisha kwamba watoto wanafanyishwa mambo yaliyo nje ya utaratibu wa elimu.
"Na ninamshangaa sana mheshimiwa waziri mkuu anapobariki masuala haya,...waziri mkuu yeye ndiye serikali hapa bungeni. Anapojibu maswali hivyo ovyo, inatuonyesha kabisa upendeleo na kutokuelewa maana ya elimu. Tunapeleka taifa kaburini," alisema Suzan.
Aliongeza: "imesikitisha na Tanzania nzima imeona ni jinsi gani nchi hii isivyokuwa na viongozi waadilifu."
CHANZO: NIPASHE

8 comments:
Oh please! Kama mmekosa cha kujadili bungeni kaeni kimya au mrudi makwenu. Watu wazima mnakaa kujadili petty things badala ya kujadili dawa, huduma mahosipitalini, ajali za kila siku. Mnajadili sherehe za CCM. So what's the big deal kama watoto walihusishwa. Mbona sie tulicheza halaiki na tulifurahia sana. Hadi leo nakumbuka. Sikuona tunalazimishwa.Kwetu was great. So please leave Waziri mkuu alone. Please discuss vitu vya maana. Watu wanakufa kila siku sababu ya magonjwa n.k nyie mwadiscuss sherehe.
yaani hadi wana bore hawa watu hicho siyo kitu chakupeleka bungeni,huo uwanja wa majimaji nilihusika kujenga kwa kujitolea wakati nikiwa darasa la pili,na mimi siyo CCM, lakini hivyo vyama vyenu vinafanya mpaka ule uwanja unakufa hakuna tena shule ya kujitolea kama ilivyokua miaka ile, huo uwanaja umejengwa kwa 49%ni watato wa shule , yaani hapo ndiyo naona bora ccm ibakie, hakuna kiongozi wa upinzani wote ni wapuuzi.
First anonymous has a valid point. The foundation of a civilized society is based on the good example given to the youth- the people they see around them, social activities based on social science, environment and political structure. During the ujamaa politics of Arusha Declaration, many students from all over the country walked many miles and days to support the Ujammaa regime. Those students who are now adults provided the foundation of leadership that most people are enjoying now. We all know that we have a challenge in solving social economic issues, but the challenge should not be directed to petty discussion in the parliament that has no social economic impact in the society, as a whole.
You anonymous ....you are ignorant. Huna nadharia ya utawala bora wala hujui serikali inaendeshwa kivipi. Shule zinahudumiwa na walipa kodi, mimi na wewe. Walimu wanalipwa na walipa kodi, mimi na wewe. Mimi si mfuasi wa chama chochote lakini nalipia kodi ili mtoto wangu wasomeshwe na nisingependelea jasho langu litumike kwa kuwafurahisha wanachama wa chama chochote hata kwamba ni CCM. Na si watu wote wanapendelea CCM. Hapo zamani kulikua na halaiki lakini chama kilikua kimoja tu na watu wote walikua wanachama wa chama hicho. Be sensible and unbiased.
We anony wa kwanza akili yako bado iko kwenye ukungu mzito sana. Eti "petty things" hivi unajua uzito wa Elimu wewe? Vitu kama hivi vikiachwa bila kuwa na mwongozo makini vina athari kubwa sana, kwa wanafunzi na kwa jamii inayofuata demokrasia. Jaribu kufanya michezo ya hovyo hovyo nchi nyingine alafu ulete majibu mepesi kama hayo unone kama serikali haita anguka. Waziri mkuu angebanwa ajiuzuru kwa majibu hayo. Toa ukungu, amka usingizini.
Hilo ni jambo la maana sana. Wanafunzi na waalimu waende kwenye shughuli za kisiasa kwa utashi wao siyo kulazimishwa na shinikizo la chama fulani. Huu ni utaratibu wa nchi na siyo siasa. Wewe kama ulifurahia halaiki hiyo ni juu yako. Hao wabunge wanajua wanacho kifanya. Walivyoanza kupiga kelele za Escrow watu waliwabeza. Nchi itaendelea kwa kukosolewa mambo makubwa na madogo.
I repeat again petty things! Naujua sana uzito wa elimu. I am well rounded. Wasting people's time discussing gwaride while people are dying everyday bila dawa e.t.c Hao wanafunzi waliachishwa shule mwezi mzima? Give me a break!
It's insane how you and many other ignorant people think by mentioning "kukosa madawa" will add value to your any of argument. As if the issue was a debate between which should be discussed between "ukosefu wa madawa" or "CCM using students for its own ceremonies." A well rounded person don't even know how the Parliament operates. Kinaitwa kipindi cha maswali na majibu ndugu. Toa ukungu.
Post a Comment