ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 16, 2015

PLUIJM AONGEZEWA MKATABA YANGA

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.

Na Hans Mloli
BAADA ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, kufanikiwa kuiongoza timu hiyo kufanya vizuri katika mechi zake kadhaa ikiwemo ya kimataifa dhidi ya BDF XI ya Botswana, hatimaye uongozi wa klabu hiyo umeamua kumuongezea mkataba.
Uamuzi wa kumuongezea mkataba kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana, ulikuja baada ya kikao cha viongozi wa Yanga kilichoketi takriban wiki moja iliyopita kwa lengo la kufanya tathmini ya ufundishaji na uwezo wa kocha huyo.

Kikao hicho kilitoka na majibu kuwa Pluijm anafaa kuendelea kuinoa timu hiyo kulingana na idadi ya mechi alizoshinda na soka linalotandazwa uwanjani kwa sasa na vijana hao wa Jangwani tangu atue rasmi Desemba, mwaka jana, hivyo tayari mpaka sasa kamati ya mashindano ipo kwenye mchakato wa kuzungumza na Pluijm juu ya mkataba huo mpya ingawa haukuwekwa wazi kuwa utakuwa ni wa muda gani.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amefafanua kuwa tathmini imeonyesha kwamba Pluijm amekuwa na asilimia nyingi zaidi za kuibuka na ushindi katika mechi za mashindano yote alizoiongoza timu hiyo tangu aliporithi mikoba ya Mbrazili, Marcio Maximo aliyefungashiwa virago siku chache baada ya kufungwa mabao 2-0 na Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe.

“Kama tulivyosema kuwa kocha tutamfanyia tathmini baada ya mechi kadhaa na kweli kumekuwa na kikao hicho ambacho kiligundua kuwa amekuwa na mafanikio kwa asilimia nyingi zaidi.

“Kutokana na hilo, tumegundua ni kocha anayetufaa kwa misimu mingine, hivyo tuna lengo kubwa la kuendelea kuwa naye hapa, tunaangalia pia jinsi gani tunaweza kuzungumza naye na kumpa mkataba wa kuendelea kuwa nasi,” alisema Muro.

Pluijm ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu, mpaka sasa ameiongoza timu hiyo kwenye michezo sita ya Ligi Kuu Bara, akishinda mitatu na kusuluhu mitatu. Kwenye Kombe la Mapinduzi, Yanga ilijitupa dimbani mara nne, ikashinda mara tatu na kufungwa mara moja.

Mechi za Pluijm:
Kushinda: Polisi Moro 1-0, Coastal 1-0, Mtibwa 2-0, Taifa Jang’ombe 4-0, Polisi 4-0, Shaba 1-0, BDF XI 2-0
Sare: Azam 2-2, Ruvu Shooting 0-0, Ndanda 0-0
Kufungwa: JKU 1-0.
Source:GPL

No comments: