Mbwana Samatta
By Gift Macha (email the author)
Straika huyo amejipatia umaarufu mkubwa miaka ya hivi karibuni kutokana na umahiri wake uwanjani hasa katika kufunga mabao. Anayafanya haya akiwa na klabu yake ya TP Mazembe pamoja na timu ya Taifa Tanzania.
HAKUNA ubishi kwamba straika wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta, ndiye mwanasoka mahiri wa Tanzania katika zama hizi. Wapo wengi wanaotamba, lakini Samatta ni funga kazi kwa sasa.
Straika huyo amejipatia umaarufu mkubwa miaka ya hivi karibuni kutokana na umahiri wake uwanjani hasa katika kufunga mabao. Anayafanya haya akiwa na klabu yake ya TP Mazembe pamoja na timu ya Taifa Tanzania.
Samatta mzaliwa wa Mbagala Rangi Tatu, jijini Dar es Salaam, alisajiliwa na Mazembe mwaka 2011 akitokea Simba. Alisaini mkataba wa miaka mitano na sasa amebakiza mwaka mmoja tu.
Mwanaspoti, ambalo limeweka kambi kwa wiki nzima hapa Lubumbashi, limefanya mahojiano na Samatta na kuzungumzia masuala kadhaa kama ifuatavyo;
Dili la kwenda Urusi
Samatta alirejea hapa Lubumbashi Alhamisi ya wiki iliyopita akitokea Urusi ambako alikwenda kufanya majaribio ya soka la kulipwa katika klabu ya CSKA Moscow.
“Mwanzoni ilikuwa nisajiliwe moja kwa moja, lakini CSKA wakasema niende kwa ajili ya majaribio kwa wiki moja, nilishindwa kufanya katika siku mbili za mwanzoni kutokana na kuumia enka, lakini siku nyingine tano nilifanya,” anasema.
“Walivutiwa na mimi, hivyo kazi ikawa ni kuzungumza na klabu, nadhani Moise (Katumbi) kawatajia dau kubwa ndiyo maana imekuwa ngumu na mpaka sasa unaona kimya.
“Dirisha la usajili kule lilifungwa mwishoni mwa mwezi uliopita, hivyo inabidi nisubiri dirisha kubwa la usajili. Sina uhakika kama mabosi wa Mazembe wataniruhusu kuondoka kabla ya mkataba wangu kumalizika, lakini nitajitahidi kwa kadiri inavyowezekana kwa sababu nimebaini nina kiwango cha kutosha kucheza Ulaya.
“Tatizo kubwa timu nyingi za Ulaya zinafikiri wachezaji wa Afrika ni wa bei chee jambo ambalo bosi wetu hakubaliani nalo kabisa, anataka dau la maana.”
Maisha ya Lubumbashi
“Nimeshapazoea hapa, yaani ni kama nipo nyumbani vile. Nina marafiki wengi kwa sababu muda mwingi nipo huku,” anasema kwa tabasamu.
“Kwa sasa naishi kwangu, lakini mwanzoni nilipofika nilifikia kwenye nyumba za klabu, palikuwa kama kifungoni kwani muda mwingi nilikuwa mpweke, niliyakumbuka sana maisha ya Tanzania wakati ule.”
Programu yake ya mazoezi
Samatta anasema mbali na mambo mengine, anapenda mazoezi kupita kiasi na kila siku lazima afanye mara mbili, ikiwamo kwenda gym kujiweka fiti.
“Kila siku kabla ya mazoezi ya kawaida ya timu huwa nawahi nusu saa zaidi, natumia muda huo kufanya mazoezi binafsi kama kupiga mipira ya faulo na kujaribu kufunga kwa mbali,” anasema.
“Kama napiga faulo huwa natumia goli la mazoezi kama ukuta, huwa naliweka mbele ya goli halisi la uwanjani na najitahidi kuvusha mpira na kufunga, huwa sihitaji kipa kwa mazoezi haya, hayanisaidii sana lakini kuna nyakati huwa naona umuhimu wake.
“Tukiwa na mazoezi ya mara moja kwa siku, huwa natumia muda mwingine wa jioni kama kuanzia saa nane mchana kwenda gym, nafanya mazoezi ili kuwa fiti zaidi, nikifanya mazoezi kwa siku mara moja huwa naona hayatoshi, siku za mapumziko huwa nafanya mazoezi ya kukimbia barabarani, kuruka kamba na pushapu.”
Umaarufu wake
Samatta ni maarufu hapa Lubumbashi, ukiwa hapa hauhitaji kuambiwa na mtu utabaini tu. Mara baada ya mechi ya Mazembe, mashabiki wengi hutamani kupiga naye picha. Wengi hutamani kubeba begi na viatu vyake. Kwa kifupi ni kwamba Samatta anapendwa sana hapa.
“Ni vizuri pale unapokuwa na watu wengi wanaokukubali, hiyo inaonyesha namna kazi yako inavyowavutia, haikuwa kazi rahisi kupata watu wengi ambao wako upande wangu, nilipambana sana wakati nafika.” anaongeza kusema mtoto huyo wa mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Ally Samatta.
“Muda mwingine hii inakuwa ni changamoto, nikitaka hata kwenda dukani inakuwa shida, inabidi kwanza nitazame chini pana watu wangapi, ni furaha lakini siyo kila muda mtu unaweza kuwa kwenye furaha.”
Posho za maana
“Hapa tunapata posho nyingi na zinakuwa tofauti kutokana na aina ya mechi tunayocheza, inakuwa tofauti pia kulingana na mashindano na hatua tunayocheza,” anafafanua.
“Mfano mechi kubwa hapa ni sisi na AS Vita ya Kinshasa, ni mechi kama vita na huwa ina hamasa kubwa, posho ya mechi hiyo ni kubwa kuliko zile nyingine.
“Posho ya mechi za kimataifa ni kubwa pia, inapanda kulingana na namna tunavyozidi kusonga mbele, ni mara chache hapa wasitoe posho.”
Watanua na magari yao
Wachezaji wa TP Mazembe wanaonekana kuwa na maisha ya tofauti na yale ya wachezaji wa Tanzania kwani, wachezaji wengi wa timu hiyo hufika mazoezini na hata kwa baadhi ya mechi wakitokea makwao. Hutumia magari binafsi pia.
Kwenye mechi ya Jumamosi kati ya Mazembe na Don Bosco, asilimia 90 ya wachezaji wa Mazembe walikuja kwa magari yao, wachache walitumia basi dogo la klabu.
“Hapa tunaruhusiwa kutumia magari yetu, tunakuja nayo mazoezini na hata kwenye baadhi ya mechi, kama tumeweka kambi huwa tunatumia basi kubwa la klabu ama pale tunapocheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika,” anasema Samatta.
Fursa ya Watanzania ipo
“Nikitazama wachezaji wanaokuja kucheza hapa, hata wa kwetu Tanzania wanaweza, ni jambo la kuamua tu kwamba nakwenda kucheza Mazembe ama timu nyingine kubwa,” anasema.
“Kuna changamoto kadhaa, lakini vipaji ndivyo vitakavyowabeba, hakuna mtu anayeweza kufunika kipaji chako, mwanzo utakuwa mgumu lakini baada ya muda utafika mbali.”
Picha yake uwanjani
Unapoingia tu kwenye Uwanja wa Mazembe ukitokea katika vyumba vya kubadilishia nguo, kumechorwa picha za mastaa kadhaa waliotamba na wanaotamba na timu hiyo, picha ya Samatta pia ipo.
“Kuchorwa kwa picha yako pale si kazi rahisi na ndiyo sababu unaona siyo wote kwenye timu wamechorwa pale, inahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuwavutia mabosi,” anasema kwa kujiamini.
“Nafurahi maana kumbukumbu yangu imebaki pale, hata nikiondoka Mtanzania mwingine akija kucheza hapa ataiona kumbukumbu yangu, ni jambo la kufurahia sana.
”SOURCE:MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment