
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyasema hayo jana wakati akiahirisha Bunge mjini Dodoma na kuongeza kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yanaenda vizuri.
Alisema vifaa mbalimbali kwa ajili kuufanikisha uchaguzi huo tayari vimeanza kununuliwa.
Pinda alisema kuwa miongoni mwa maandalizi ya uchaguzi huo ni uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 218.
“Bajeti ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni shilingi bilioni 218 wakati hii ya uchaguzi mkuu ni shilingi bilioni 268,” alisema Pinda.
Pinda alisema kuwa changamoto kubwa inayoikabili Serikali kwa sasa ni upatikanaji wa fedha hizo kwa muda muafaka.
“Licha ya changamoto mbalimbali lakini suala hili limepewa kipaumbele, na kipaumbele cha serikali ni kuhakikisha fedha zinapatikana na zoezi hili linafanyika kama lilivyopangwa,” alisema Pinda.
Aidha, Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kupiga kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa.
Pinda aliwaomba wabunge kushirikiana na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuhamasisha wananchi wote wenye sifa wanashiriki katika mazoezi hayo.
Aliahidi kuwa Serikali itahakikisha inasimamia vizuri mazoezi hayo na kufanikisha ipasavyo upigaji kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa sambamba na Uchaguzi Mkuu ujao.
KUHUSU MAABARA
Pinda, amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya, mameya na wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwenye maeneo yao kabla ya muda uliowekwa na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema serikali haina mpango wa kuongeza muda mwingine na kutaka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ihakikishe agizo hilo linatekelezwa kwa muda uliopangwa.
Kuhusu hali ya akiba ya chakula, alisema ipo vizuri ambapo hadi mwezi Januari mwaka huu, Wakala wa Chakula wa Taifa (NFRA) walikuwa wameshanunua jumla ya tani 298,122.3 za nafaka ambazo ni sawa na asilimia 107.1 ya lengo lililokusudiwa.
Alisema kuwa hadi Januari 29, mwaka huu kiasi cha chakula kilichochukuliwa katika maghala kilikuwa ni tani 29,290.5, huku jumla ya tani 1,175.5 zilikuwa njiani kutoka kwenye vituo vya vijijini kwenda NFRA.
Pinda alisema changamoto inayoikabili NFRA ni tatizo la uhaba wa maghala ya kuhifadhia nafaka na kusababisha nyingine kufunikwa kwa maturubai nje ya maghala hayo.
SEKTA YA NISHATI
Pinda alisema serikali imedhamiria kuongeza kiwango cha huduma za upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini ili kujenga msingi wa uchumi imara na wa kisasa wa taifa linalojitegemea.
Alisema kuwa ili kufikia azma hiyo, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) umeanza kutekeleza mradi kabambe wa awamu ya pili unaohusisha usambazaji wa umeme vijiji katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Kuhusu ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Jijini Dar es Salaam, Pinda alisema kuwa hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu zaidi ya asilimia 97 ya mradi huo itakuwa imekamilika.
UCHAGUZI S/MTAA
Pinda alisema kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana ulimalizika vizuri licha ya kukabiliwa na changamoto ndogo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment