ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 8, 2015

Taasisi zinazotuhumiwa kwa rushwa zaja juu

Baadhi ya viongozi wa taasisi zinazotuhumiwa kuwa vinara wala rushwa wameonyeshwa kushangazwa na ripoti ya utafiti wa Afrobarometer huku wakihoji vigezo vilivyotumika.

Juzi Afrobarometer wakitangaza utafiti wao huku wakitaja taasisi hizo na asilimia zake kwenye mabano kuwa ni Polisi (50), Mamlaka ya Mapato nchini (37), Majaji na Mahakimu (36), Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (29), Maofisa wa serikali za mitaa (25), Watumishi wa Umma (25), Wabunge (22) na Rais na Maofisa wa Ikulu (14).

Wakizungumza na NIPASHE Jumapili kwa nyakati tofauti taasisi hizo zimeonyesha kushangazwa na matokeo ya utafiti huo huku wengine wakihoji vigezo gani vilivyotumika.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, alisema kuwa bado hajaipata ripoti ya utafiti huo na kuahidi pindi utakapomfikia atauzungumzia.
Alisema jeshi la polisi hawajajua ni vitu gani vilivyobainishwa kwenye utafiti huo na kuifanya polisi kuwa kinara.

“Tukiupata tutauzungumzia kwani mpaka wamefikia maamuzi haya inawezekana kuna vitu wameviona na sisi hatuvijui,” alisema Mangu.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah alisema kuwa hayupo tayari kujiingiza katika malumbana yoyote na kwamba yaliyosemwa dhidi ya taasisi yake hayamuumizi kichwa kwa kuwa anajua anachokifanya.

Dk. Hoseah alisema hayupo tayari kulumbana na mawazo ya watu kwa kuwa nchi inajiongoza kidemokrasia na kila mmoja ana haki ya kuzungumza.

“Katika kundi la watu hawakosekani wabaya wapo ambao hawatafanya vizuri hakuna aliye malaika hata unapokuwa na watoto siyo wote watafanana kwa tabia,” alisema.

Alisema anashukuru kwa mawazo hayo na kwamba watayaangalia na pale penye upungufu wataufanyia kazi.

Aidha, Dk. Hoseah alitahadharisha kuwa ifike pahala nchi iheshimike na siyo kila wakati ionekane kuwa ni chafu ama haina maana.

Naye Mkurugenzi wa Elimu kutoka TRA, Richard Kayombo, alisema utafiti huo haujawafikia zaidi ya kuusikia kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, alisema kuna vitu wanavifanya katika kudhibiti masuala ya rushwa ambapo wameweka misingi ya maadili katika kuhakikisha kila mtumishi wa TRA anapatiwa mafunzo ya maadili.

Alisema kila mwaka mtumishi wa TRA anajaza fomu za kuonyesha mali anazomiliki.

Kayombo alisema wana idara ya maadili ambayo inafuatilia masuala ya tuhuma pale zinapotajwa na hatua kuchukuliwa.

Alisema wakiipata ripoti hiyo na kuonyesha maeneo ambayo yenye miale ya rushwa wataifanyia kazi.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipohojiwa kuhusiana na wabunge kutajwa katika ripoti hiyo alisema ni vigumu kujua kwa haraka na inawezekana mazingira hayo kuwapo.

Alisema bado hajausoma utafiti huo na kueleza kuwa kama wabunge wametajwa itabidi wakutane na watafiti hao ili wawaeleze jinsi wabunge wanavyoingia katika suala hilo la rushwa .
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: