Advertisements

Sunday, February 1, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA UJERUMANI HAPA NCHINI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
 
                                                 

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

 

                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM,  
                                    Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Ujerumani, Mhe. Joachim Gauck anatarajiwa kuwasili nchini usiku wa tarehe 02 Februari, 2015 kwa ziara ya kitaifa ya siku tano kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mhe. Rais Gauck atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Kikwete Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 03 Februari, 2015 na atakagua Gwaride la Heshima na kupigiwa mizinga 21. Wananchi wanaombwa kuwa watulivu wakati mizinga hii ikipigwa kwani ni salama.
Baada ya mapokezi hayo, Mhe. Gauck atafanya mazungumzo ya faragha na Rais Kikwete yakifuatiwa na mazungumzo rasmi. Aidha Marais hao watakutana na Waandishi wa Habari.

Baadaye siku hiyo ya Februari 03, Mhe. Rais Gauck atakutana na Wafanyabiashara, atatembelea Kanisa la Kilutheri la Azania Front, atakutana na Wawakilishi wa Taasisi za Kiraia na kushiriki Dhifa ya Kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake Mhe. Rais Kikwete, Ikulu.
Mhe. Rais Gauck ambaye ameongozana na Mke wake Bibi Schadt, Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Ujerumani na Ujumbe wa Wafanyabiashara tisa, ataondoka Dar es Salaam kuelekea Zanzibar tarehe 04 Februari, 2015 ambapo atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kabla ya kushiriki kwenye Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Viongozi wa Dini kuhusu Amani. Rais Gauck pia atakutana na Vijana kutoka Ujerumani wanaojitolea katika Programu ya Weltwarts Visiwani humo.
Jioni ya Februari 04, Mhe. Gauck ataondoka Zanzibar kuelekea Mkoani Arusha. Akiwa Mkoani humo siku ya tarehe 05 Februari, 2015 atatembelea Taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kuhutubia Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA). Mhe. Gauck na ujumbe wake watatembelea pia Hifadhi ya Wanyama ya Serengeti ambapo atazindua Kituo kipya cha kudhibiti Ujangili.
Mhe. Rais Gauck anatarajiwa kumaliza ziara yake hapa nchini tarehe 06 Februari, 2015 na kuondokea  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kurejea Ujerumani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

01 Februari, 2015

No comments: