Advertisements

Sunday, February 1, 2015

WAZIRI DKT. MAGUFULI AKAGUA BARABARA MKOANI MBEYA.

aziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amekagua barabara mkoani Mbeya na kuahidi ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ya Mpemba-Isongole yenye urefu wa KM 58 Wilayani Ileje.
Akizungumza mara baada ya kufungua sehemu ya barabara ya lami wilayani humo kati ya Isongole hadi Itumba KM 9, Waziri Magufuli amesema Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpemba-Itumba KM 58, ili kufungua fursa za uchumi wilayani Ileje na kuhakikisha barabara hiyo inaungana na nchi ya malawi kwa lami na kuhuisha sekta ya uchukuzi na biashara baina ya nchi hizo.
“Barabara ya lami ni muhimu kujengwa katika Wilaya ya Ileje ili kukuza uchumi wa wananchi ambao wana mazao mengi yanayohitaji usafiri wa uhakika kufikia masoko”, amefafanua Dkt. Magufuli.
Waziri Magufuli amezungumzia umuhimu wa kuiunganisha Wilaya ya Ileje na mtandao wa barabara unaoanzia Bukoba –Biharamulo- Uvinza-Mpanda-Sumbawanga-Tunduma-Mpemba-Isongole hadi Chitipa nchini Malawi ambapo ikikamilika kwa lami itafungua ukanda muhimu wa biashara na kukuza uchumi wa nchi.
Amehimiza umuhimu wa Wilaya ya Ileje kutumia fedha za mfuko wa barabara kujenga barabara za lami ili kurahisisha huduma za usafiri na kuvutia wataalam wengi kufanyakazi na kuishi wilayani humo.
“Hakikisheni mnafanyakazi kwa umoja na mshikamano kwa kuepuka majungu na rushwa ili mfikie malengo na mwaka huu tutawapa shilingi milioni 721 kwaajili ya barabara”, amesisitiza Waziri Magufuli.
Awali Waziri Magufuli alikagua mizani ya Mpemba wilayani Momba na kuhimiza wafanyakazi wa mizani hiyo kufanyakazi kwa weledi na uadilifu kwa kuzingatia elimu walizonazo na hivyo kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki kwa wasafirishaji na kulinda barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa.
Naye Katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe amesema barabara ya Mpemba hadi Isongole itakayojengwa kwa kiwango cha lami ilikuwa barabara ya Wilaya lakini kutokana na umuhimu wake Serikali imeipandisha hadhi kuwa ya mkoa na tayari upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa barabara hiyo umekamilika.
Naye mkuu wa wilaya ya Ileje Rosemary   Sinyamule amemhakikishia Waziri Magufuli kuwa Wilaya hiyo ina upungufu wa barabara za lami hivyo ujenzi wake utavutia watumishi kuishi na kufanya kazi katika wilaya hiyo inayopakana na nchi za Malawi na Zambia na kuhuisha fursa za uchumi zilizomo wilayani humo.
Zaidi ya KM 11,154 za barabara za lami zinajengwa nchini kote ambapo inatarajiwa hadi mwishoni mwa mwaka huu Tanzania itakuwa na jumla ya barabara  za lami zenye urefu wa KM 18,000  zinazounganisha mikoa na nchi jirani.
Mwisho.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi

No comments: