
Ngasa alilazimika kukopa fedha benki baada ya kuamriwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuilipa Simba Sh. milioni 45 alizochukua ili ajiunge nayo lakini akaikacha na kutua Yanga. Kamati hiyo pia ilimfungia mechi sita za awali za Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita kufuatia kesi yake hiyo dhidi ya Simba.
Hata hivyo, Yanga haikuwa tayari kutaja kiasi ambacho mchezaji huyo alikopa benki, alichokatwa na viongozi ambacho hakikupelekwa benki, wala kiasi cha deni kilichobaki.
Akizungumza jana jijini, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro, alisema kuwa tayari wamepokea maombi ya Ngasa lakini Yanga itatekeleza maombi hayo kwa masharti maalum.
Muro alisema kuwa ndani ya kipindi cha wiki moja Yanga itakuwa imelitatua suala la mshambuliaji huyo ili aweze kuitumikia vyema timu hiyo inayoongoza Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
"Kulipa deni kuna taratibu zake, fedha za Yanga ni za wanachama na ni lazima utaratibu ufuatwe kabla ya kumlipia. Ngasa ameomba kulipiwa nasi tutamlipia kwa sababu bado tunamhitaji naye pia anatuhitaji," alisema Muro.
Alisema kwamba Yanga ilipokea barua kutoka benki ya CRDB ikiulizia malipo ya deni la mchezaji huyo ambaye mshahara wake alikuwa anapewa mkononi badala ya kupitia benki ili akatwe na walipoamua kufuata makubaliano mshambuliaji huyo alikatwa fedha zote kufuatia 'kukacha' deni kwa muda mrefu.
Muro pia alisema uongozi utafuatilia kujua fedha za Ngasa zilizokuwa zinakatwa zilikuwa zinaenda wapi na kuahidi kukomesha tabia ya 'ufisadi' ambayo ilikuwa inafanywa ndani ya klabu hiyo.
Ngasa alisema kuwa baada ya CRDB kuchukua mishahara yake ya miezi miwili ili kufidia makato ya awali ya deni 'yaliyokwepwa', hali hiyo ilimuathiri na kufanya ashindwe kuichezea kikamilifu timu yake lakini sasa anaahidi kurejea kwenye kiwango chake endapo suala lake litafanyiwa kazi.
Alisema kwamba yeye hawezi kuisaliti Yanga, anaipenda na hatarajii kusaini klabu nyingine ya hapa nchini endapo timu hiyo haitampa mkataba mpya.
"Kwanza nilikuwa na matatizo ya kifamilia, nikayatatua, suala la deni kwanza nilijua viongozi wangu wangenisaidia kulipa lakini haikuwa hivyo, hivi karibuni ndiyo deni lilinizidia. Endapo watanisaidia kulipa naahidi kuwa mfungaji bora msimu huu ingawa hadi leo nina magoli mawili," alisema Ngasa, ambaye alifunga kwa mara ya kwanza msimu huu Jumapili 'alipotupia' mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na kuipandisha timu yake kileleni mwa msimamo.
Yanga jana ililazimika kutoa tamko hilo kufuatia kauli ya mchezaji huyo aliyoitoa Jumapili kwamba licha ya kuitumikia vyema timu hiyo, bado anaijutia ofa 'nono' ya kujiunga na El Merreikh ya Sudan ambayo aliikataa mwaka 2012 na kujiunga na Yanga kutokana na 'mapenzi' aliyonayo.
VIINGILIO KWA BDF
Aidha, Yanga jana ilitangaza kuwa kiingilio cha chini katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF IX itakayofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni Sh.5,000 huku cha juu kikiwa ni Sh.30,000.
Muro alitaja viingilio vingine katika mchezo huo kuwa ni Sh.20,000 kwa eneo la VIP B, Sh.15,000 (VIP C), Sh.10,000 (viti vya bluu) na Sh.7,000 viti vya rangi ya machungwa.
Muro alisema kuwa ili Yanga iweze kupata fedha za kujiendesha na kufanya maandalizi yake ya mechi hiyo mashabiki wanatakiwa kujitokeza kununua tiketi mapema kwa sababu mechi hiyo haitarajii kuonyeshwa hewani moja kwa moja kupitia televisheni.
"Kama wapo watu watakaa majumbani wakisubiri kuiona mechi hiyo, wasikae na ndoto hizo, labda kitokee kituo ambacho kitatupa fedha zinazofanana na thamani ya mchezo huo, na ikitoa, hatutatoa 'signal' Dar es Salaam," alisema Muro.
Aliongeza kuwa tiketi za mchezo huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa katika maeneo mbalimbali jijini kuanzia Ijumaa asubuhi.
"Tumeweka viingilio vidogo kwa sababu tunawahitaji mashabiki kushirikiana nasi kutoa hamasa, uwapo wao ni muhimu katika kuhamasisha ushindi wa timu katika mechi hii ya kwanza tukiwa nyumbani," Muro aliongeza.
Alisema kwamba kikosi cha timu hiyo kiliingia kambini Jumapili jioni baada ya kumaliza mechi yao ya Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Mtibwa Sugar na kuanzia jana kinafanya mazoezi yake mara mbili kwenye Uwanja wa Taifa.
Alisema pia wachezaji wote wa timu hiyo waliokuwa majeruhi ambao ni pamoja na Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Deogratius Munishi 'Dida' wamepona na wanafanya mazoezi na wenzao.
Mbali na Yanga, wawakilishi wengine wa Bara katika mashindano ya kimataifa mwaka huu ni Azam ambao wanashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na wataanza kampeni ya kuwania ubingwa huo kwa kuwakaribisha El Merreikh kutoka Sudan Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment