Advertisements

Tuesday, March 31, 2015

Bastola ya Gwajima utata.


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, akimjulia hali Askofu Josephat Gwajima, wa Kanisa la Ufufuo na Uzima aliyelazwa kwenye hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam kwa matibabu. PICHA: Tryphone Mweji
Mwenyekiti wa taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, akimjulia hali Askofu Gwajima leo Jumatatu Machi 30, 2015
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda akimjulia hali Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aliyelazwa Hospitali ya TMJ kwa ajili ya matibabu baada ya kupata mshituko katika mahojiano na polisi akituhumiwa kutoa lugha isiyofaa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.

Kiongozi wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amefunguka na kueleza kuwa bastola aliyokutwa nayo mmoja wa wafuasi wake, ni mali yake anayoimiliki kihalali.

Hata hivyo, suala la umiliki wa bastola hiyo limeibua utata baada ya Jeshi la Polisi kusema kuwa inamilikiwa kinyume cha sheria.

Akizungumza kwa mara ya kwanza siku chache baada ya kuishiwa nguvu na kuzirai kisha kulazwa hospitalini, Askofu Gwajima alisema kuwa aliwatuma wasaidizi wake waichukue bastola hiyo nyumbani kwake kumpelekea hospitalini alikolazwa.


Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana akiwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) kufuatia kukamatwa kwa wafuasi wa kanisa lake 15.
Wafuasi hao wanatuhumiwa kupanga njama za kumtorosha kiongozi huyo kutoka Hospitali ya TMJ alikolazwa.

Askofu Gwajima alisema baada ya kuzagaa kwa taarifa za uvumi katika mitandao ya kijamii kwamba amefariki dunia, aliwaita wasaidizi wake kumlinda hospitalini hapo akihofia kuwapo kwa njama za kumuua.

Askofu Gwajima aliyekuwa akizungumza kwa shida kutokana na hali yake ya kiafya, alisema miongoni mwa wasaidizi hao aliwatuma kwenda nyumbani kwake kuchukua mkoba uliokuwa na silaha hiyo ndani yake wampelekee hospitalini hapo kwa ajili ya kile alichokiita kujikinga mwenyewe.

Aliongeza kuwa kabla ya wasaidizi wake kumkabidhi mkoba huo, ndipo Polisi walipowavamia na kuwakamata kisha kuondoka nao ukiwa na bastola ndani yake.

“Ile bastola ni ya kwangu na ninaimiliki kihalali, hata nyaraka zake ninazo, lakini ninawashangaa polisi hawajaja kuniuliza wala kuniomba document (nyaraka) za umiliki wake,” alisema Gwajima kwa taabu huku akijishika tumbo.

Kutokana na hali hiyo, Askofu Gwajima alisema kuanzia sasa hana imani na Jeshi la Polisi kutokana na vitendo wanavyomfanyia pamoja na wafuasi wake.

Kadhalika, Askofu huyo alisema hana ugomvi wowote na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, bali alimtolea maneno kauli anazodaiwa kumtukana na kumkashifu kwa kwa lengo la kumkosoa lilifuatia kutoa kauli iliyopingana na tamko lililotolewa na Jukwaa la Kikristo Tanzania (TCF).

Askofu Gwajima alipoulizwa anasemaje baada ya Askofu Pengo kutangaza kwamba amemsamehe, alijibu kuwa anamheshimu Askofu na hana ugomvi bali alimkemea tu.

Alisema Askofu Pengo hajaonyesha nia ya kumshtaki wala kumdhihaki bali Jeshi la Polisi ndilo linalokuza mambo.

ALIVYOPATA TAARIFA
Askofu Gwajima alisema kuwa alipokuwa jijini Arusha alisoma matangazo na taarifa za vyombo vya habari kuwa anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano.

Alisema alirudi jijini Dar es Salaam na kwenda Kituo Kikuu cha Polisi na kuonana na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, na ndipo alipoanza kuhojiwa. “Mimi sikupigiwa simu wala sikupewa taarifa, ila niliona matangazo katika vyombo vya habari kuwa ninatafutwa na Polisi kwa mahojiano, ndipo nilipotii amri na kwenda Kituo Kikuu cha Polisi,” alisema Gwajima.

CHANZO CHA KUUGUA
Askofu Gwajima akizungumza huku akihema, alisema akiwa katika mahojiano na Polisi, ghafla alisikia maumivu makali ya kichwa.

POLISI: ANAMILIKI SILAHA KINYUME
Wakati Askofu Gwajima akidai ana umiliki halali wa bastola hiyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema silaha waliokamatwa nayo wafuasi wa Askofu Gwajima, haimilikiwi kihalali na wafuasi hao wala Askofu Gwajima mwenyewe.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kufahamu hatma ya wafuasi hao waliokamatwa tangu juzi na jeshi hilo.

Kova alisema hilo ni jambo jipya ambalo wamelibaini na kwamba umiliki wa silaha hiyo ni kinyume cha sheria kwa kuwa haionyeshi mmiliki kati ya pande hizo mbili.

“Wafuasi wa Askofu Gwajima bado tunawahoji, lakini jambo jipya ambalo tumebaini ni kwamba silaha waliokamatwa nayo haionyeshi mmiliki kati ya wao na Askofu Gwajima mwenyewe,” alisema Kova na kuongeza:

“Kuhusiana na sababu zilizosababisha wafuasi hao kutaka kumtorosha Gwajima bado tunaendelea kuwahoji na tunatarajia kukamilisha uchunguzi haraka iwezekanavyo.”

Hata hivyo, Kova hakutaja sababu zilizosababisha Askofu Gwajima kuzimia, akisema daktari wake ndiye anayeweza kuelezea hilo.

LIPUMBA, SLAA WAMTEMBELEA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, jana alimtembea Askofu Gwajima hospitalini hapo kumjulia hali. Hata hivyo, Prof. Lipumba alishangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kutotii sheria za haki za binadamu. Alisema Askofu Gwajima alikuwa anatoa hisia zake baada ya TCF kutoa tamko lao.

Alisema Polisi wanapaswa kulaumiwa kwa kusababisha maradhi ya Askofu Gwajima.

Alisema hata yeye aliwahi kuugua ghafla akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi akihojiwa na alipowaeleza hawakulizingatia. Aliongeza kwamba kwa kuwa Kardinali Pengo ameshatangaza msamaha kwa Askofu Gwajima, hakuna haja ya kuendelea kumshikilia.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alifika hospitalini hapo kumjulia hali Gwajima na kusema Polisi ndiyo wanaopaswa kulaumiwa kwa kusababisha afya ya Askofu Gwajima kudhoofika ghafla.

DC MAKONDA: NAMSUBIRI
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, naye alifika hospitalini hapo kumjulia hali Askofu Gwajima na kusema kuwa jana Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ilipanga kukutana na Askofu kwa mahojiano.

Alisema yeye (Makonda) kama Mwenyekiti wa kamati hiyo, ana jukumu la kuhakikisha kunakuwapo na usalama katika wilaya.

Alisema hadi sasa kamati hiyo haina uhakika kama maneno yaliyomo katika mitandao yalitamkwa na Askofu Gwajima na ndiyo maana wanahitaji kumhoji.

Makonda alisema Askofu Gwajima atakapotoka hospitalini kamati hiyo itamhoji ili kujiridhisha kama kweli maneno hayo aliyatoa mwenyewe.

Alipoulizwa ikibainika ni kweli maneno hayo ni ya Askofu Gwajima watamchulia adhabu gani, Makonda alisema Kamati ndiyo itakayoamua.

“Tutamhoji ili tujiridhishe, tutamuuliza kama maneno yale ni ya kwake kweli, na kama anafahamu uhuru wa kusifu na kuabudu,” alisema Makonda.
Alisema ni jambo la ajabu na la aibu kwa kiongozi kama Gwajima kumtukana Askofu Pengo kwa matusi makubwa hadharani.

DAKTARI AZUNGUMZA
Daktari anayemtibu Askofu Gwajima, Dk. Fortunatus Mazigo, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Askofu Gwajima anaendelea vizuri na kwa sasa anatarajia kuanza mazoezi mepesi.

Alisema Askofu Gwajima anatibiwa na jopo la madaktari watatu na anaweza kuruhusiwa wakati wowote.

Hata hivyo, taarifa tulizozipata kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakati tukienda mitambozi zilieleza kuwa uchunguzi wa kina umebaini kuwa Askofu Gwajima anamiliki bastola hiyo hiyo kihalali.

"Uchunguzi wa kina na wa kitaalam sasa umethibitisha kwamba silaha hiyo inamilikiwa kihalali na Askofu Josephat Gwajima. Kuhusu risasi 17 za shotgun ni kwamba Askofu Gwajima anamiliki bunduki aina ya shotgun yenye namba 102837 ambayo inatumia risasi za aina ya hizo zilizokamatwa," ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova.

Iliongeza: "Kuhusu watu 15 wanaotuhumiwa kujaribu kumtorosha Askofu Josephat Gwajima, bado uchunguzi unaendelea. Aidha, watu hao pia wanahojiwa kuhusu suala la kukutwa na silaha na risasi zilizotajwa hapo juu wakati wao siyo wamiliki halali za silaha hiyo na risasi hizo na idadi iliyotajwa kwa mujibu wa sheria."

Taarifa ilisisitiza kuwa baada ya uchunguzi wa suala hilo, jalada la kesi litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali kabla hawajafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Imeandikwa na Gwamapa Alipipi, Elizabeth Zaya na Mary Geofrey
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

siku ile alivyokuwa anahojiwa na kuumwa kichwa, mimi ningemwona wa ukweli kama angekikemea hicho kichwa kipone, badala yake kazimia yeye!!! aache kushindana na Mungu!! Gwajima wewe si Mungu!!!! Mungu akitaka viumbe wake waache waenda warudi kwa Mungu! mwacheni Mungu aitwe Mungu!!!hauwezi kufufua mtu wewe, danganya waumini uliowateka akili zao

Anonymous said...

Asante. DC P makonda na yale uliyotoa kwa Mr Lowassa yalikuwa ya kweli? Unaonaje ukianza na hilo pamoja na kamati yako ya usalama??