Advertisements

Tuesday, March 3, 2015

JE, UNGEKUWA HUJAFANYIWA KITCHEN PARTY?!-2

JUMANNE zinakuja kama mvua! Imeshafika Jumanne nyingine huku nikiamini wasomaji wangu wote mko na afya njema kabisa baada ya kuachana wiki iliyopita katika mada hiihii ya Je, Ungekuwa Hujafanyiwa Kitchen Party?

Wiki iliyopita tuliishia pale ambapo nilisema nilijaribu kuchunguza kwa muda mrefu kuhusu wanandoa wanawake ambao walipata mafunzo ya Kitchen Party nikagundua kuwa, wengi wao wanapoingia ukumbini siku ya sherehe mawazo yao ni kutuzwa vyombo ili wajifananishe na mashoga zao waliotangulia.

Wiki hii ninaendelea kwa kusema kuwa, naamini hali hiyo ya kuwa na mchecheto wa vyombo husababisha bi harusi mtarajiwa kuhamishia umakini wake kwa kila mwalikwa anayeingia ukumbini kuona amebeba chombo gani hivyo masikio yake kupoteza uwezo wa kudaka maneno ya mafunzo yanayotolewa na watu waliomzidi umri.

FAIDA YA UPANDE MMOJA
Ukiangalia kwa macho ya kujiongeza utaona kuwa, Kitchen Party za miaka hii ni za kupoteza muda tu lakini zinatoa faida kwenye vyombo basi! Ndiyo maana wanandoa wa siku hizi wanapokwenda kuanza maisha vitu vingi ni vipyaa!

Kuna ma bi harusi ambao ndani ya ukumbi peke yake hupata kitanda, godoro, kabati kubwa la nguo, kabati la vyombo, sofa na vyombo vyote vya jikoni. Mungu ampe nini tena!

HILI NALO NENO
Huwa najiuliza, kama mke ndani ya ndoa anakwenda kuwa mlopolopo (kidomodomo) na amefanyiwa Kitchen Party, je angekuwa hajafanyiwa angekuwaje?Hili jambo ni la kuliangalia kwa umakini mkubwa hasa kwa wazazi wa kike ambao wanawaandaa mabinti zao kuingia kwenye ndoa.

MAFUNZO NI MUHIMU
Mafunzo kabla ya kuingia kwenye ndoa ni muhimu sana kuliko vitu. Haitasaidia bi harusi kuwa na vitu vingi huku ndani ya nyumba kukienda kuwaka moto wa manenomaneno.

WAPO WA KUNDI HILI
Utafiti wangu umebaini kuwa, wapo wanawake wamebahatika kuingia kwenye ndoa pasipo kupewa mafunzo ya aina yoyote ile zaidi ya yale ya kutoka kwa mama, shangazi, bibi kutoka kwenye familia yake na wamekwenda kuwa na heshima kubwa ndani ya ndoa zao.

NI HESHIMA KUBWA KATIKA FAMILIA
Ninavyoamini mimi ni kwamba, mwanamke anapokuwa amefundwa anaonekana hata katika macho ya kawaida. Watu mtaani kwake watamjua na watamheshimu kwa sababu heshima itaanzia kwake kwenda kwa wengine.

Mwanamke ambaye hakufundwa au alifundwa lakini ndiyo wale wa kutaka vyombo tu, hata jamii itawajua kwa staili ya maisha yao ya kila siku ambapo wengi wanaishi maisha yasiyo na hofu wala heshima, wengine hufikia mahali husema ‘naishi nitakavyo mimi’ kumbe maisha ya kuishi atakavyo mtu ndiyo mabaya zaidi kuliko yale ya kuifanya jamii ikuheshimu.

Nihitimishe mada hii kwa kukumbuka maneno ya mzee mmoja alikuwa akiitwa mzee Musa, kwa sasa ni marehemu, yeye alisema kwamba ndani ya ndoa, maisha ya kila mmoja na malezi yake ya awali huonekana vizuri kuliko wasio kwenye ndoa.

Alisema hivi: “Kijana wangu, wawili wakioana, kwa sababu kila mmoja katoka kwenye malezi yake, ni rahisi kujua mwenza wako alilelewaje kutokana na atakavyokuwa akiishi.“Ukimwona mke au mume ni mkofori sana ni picha halisi ya malezi. Hasa mwanamke, akiwa mkorofikorofi ndani ya ndoa, ujue alilelewa katika misingi iliyokosa maandalizi ya maisha yake ya ndoa badala yake wazazi wake walidhani ataishi peke yake maisha.Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

No comments: