ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 27, 2015

Kagame ammwagia sifa Kikwete

Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda, Paul Kagame wakiteta jambo wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa nchi sita. Picha na Venance Nestory

Dar es Salaam. Rais wa Rwanda, Paul Kagame amemwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa kuboresha huduma za Bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha mizigo inayosafirishwa kwenda Rwanda kufika mapema zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Akizungumza kwa furaha wakati marais hao walipotembelea kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS bandarini hapo jana, Rais Kagame alisema hatua iliyopigwa ni mafanikio kwa Rwanda.
“Napenda nimpongeze Rais Kikwete kwa mafanikio yaliyopatikana bandarini, kazi ikiwa nzuri (bandarini Dar), huko kwetu Rwanda tunafaidika,” alisema Rais Kagame. Alisema Rwanda itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufaika kibiashara.
Rais Kikwete alisema tangu ameingia madarakani, ameitembelea Bandari ya Dar es Salaam mara nne, lakini ziara tatu za mwanzo hazikuwa za furaha kutokana na wizi, ucheleweshaji wa mizigo na malalamiko yaliyokuwa yamekithiri bandarini hapo.
Huku akionekana mwenye furaha, Rais Kikwete alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatakiwa ipongezwe kwa kufanikiwa kuwaondoa wezi waliokuwa wakiirudisha nyuma.
“Kwa hiyo kusikia habari nzuri zinazofanywa hapa mnanifurahisha sana. Kulikuwa na genge la wezi, sifa mbaya, meli zinakaa siku 23, mambo ya ajabu sana, leo meli zinakaa kwa muda mfupi na hakuna udokozi, kumbe mnaweza kuwa waaminifu,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa kutokana na uhalifu uliokuwa unafanyika bandarini hapo, Burundi nayo ilikuwa ikiilalamikia Tanzania.
“Burundi walilalamika mambo tunayowafanyia, lakini ukiwaangalia ni kama vile wanamlaumu Mungu kwa nini aliiweka Tanzania katikati yao na bahari, pengine ingekuwa nchi nyingine ingewafanyia tofauti,” alisema Rais Kikwete.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Awadhi Massawe alisema tangu kufanyika kwa maboresho bandarini hapo, idadi ya mizigo inayopelekwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda imeongezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TICTS, Walles Paul alisema pamoja na kitengo hicho kuboresha utoaji wa huduma zake, bado kinakabiliwa na changamoto ya eneo la kufanyia kazi.
“Nafasi haitoshi tunahitaji kuongezewa ili tusirudi nyuma tulikotoka,” alisema Paul.
Mapema jana asubuhi katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa wawekezaji, Rais Kagame alisema ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi, ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya uchukuzi hasa reli inaboreshwa.
Alisema maboresho na mikakati ya kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge Railway - SGR) ni hatua nzuri lakini Serikali peke yake haitaweza kukamilisha mradi huo.
“Mkakati huu unahitaji ushirikiano kati ya Serikali za nchi washirika pamoja na sekta binafsi kwa sababu inahitaji uwekezaji mkubwa,” alisema Rais Kagame mbele ya wawekezaji zaidi ya 300 wa miradi 23 ya ukanda wa kati.
Rais huyo alisema umefika wakati kwa nchi wanachama kuhakikisha kuwa mipango yote inayopangwa inatekelezwa kwa muda na kwa wakati.
“Siyo mara ya kwanza tunakutana kujadili masuala kama haya. Lakini sasa umefika wakati wa sisi kwenda mbele na siyo kurudi nyuma tena. Ukanda huu ni muhimu sana kwani unawaunganisha watu wetu pamoja, unasaidia kuchochea na kuongeza fursa mbalimbali za uchumi kwa nchi zetu.”
Alisema nchi wanachama wa ukanda wa kati zinatakiwa kutambua mchango wa uwekezaji katika ukanda huo kwani matunda yake yataliwa kwa ujumla.
Akizungumzia uwekezaji katika miradi hiyo, Rais Kikwete alisema Serikali imejitahidi kuboresha miundombinu ya barabara, hivyo wakati huu inahitaji kushirikisha sekta binafsi.
Alisema mradi huo wa reli hiyo unahitaji Dola za Marekani 5.5 bilioni hadi kukamilika... “Tumeona ni vyema kuwashirika wadau kutoka sekta binafsi katika hili ili na sisi tuweze kupata mchango wao.”
Alisema anatamani nchi hizo zingeweza kujenga reli ya kiwango cha kisasa yenye kutumia treni za kisasa za mabehewa 100 zenye uwezo wa kubeba kontena 300 kwa safari moja.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza aliyesema kuwa anatamani nchi hizo zifikie hapo kwani hakuna treni wala lori linaloweza kubeba mizigo kwa kiwango hicho.
Hata hivyo, alisema nchi hizo zina kila sababu ya kufikia malengo hayo kwani amani na utulivu vimetawala tofauti na ilivyokuwa kwa baadhi ya nchi hapo zamani.
MWANANCHI

2 comments:

Anonymous said...

Urafiki feki

Anonymous said...

Huo ndio ujirani mwema. God bless Kikwete