Tuesday, March 24, 2015

Mansour ajitosa uwakilishi Kiembesamaki

mansour-yussuf-himidSARAH MOSSI NA IS-HAKA HASSAN, ZANZIBAR
WAZIRI wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansour Himid Yussuf, ametangaza kujitosa katika kinyang’anyiro cha Uwakilishi katika jimbo la Kiembesamaki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Atachukua fomu ya kuwania jimbo hilo kupitia CUF.
Mansour ambaye alifukuzwa uanachama ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Agosti 26 mwaka huu, baadaye alitangaza kujiunga na CUF.
Akituhubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Bustanini, Kiembesamaki, alisema tayari amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na ameirejesha.
Mwanasiasa huyo alitumia mkutano huo kuwaomba radhi kwa matendo aliyokuwa akiyaona wakitendewa Wazanzibari, yakiwamo kupigwa na kudhalilishwa na Serikali wakati wote akiwa ndani ya Serikali.
Akizungumzia safari yake ya kujiunga na CUF, Mansour alisema haikuwa rahisi kwake kwani wazee wa Kiembesamaki na wananchi waliamini amekwisha katika siasa.
“Mlilia sana, niliwaambia tulieni wakati bado…milinifariji katika safari yangu ya kujiunga CUF, pamoja na ugumu uliopo lazima niseme ukweli, mlikuwa na wasiwasi kwamba baada ya mimi kwenda jela labda sitogombea.
“Mliona nilikuwa taabani na nawapa pole wale wote waliopata misukosuko kama yangu, wazee walikuwa na wasiwasi labda sitogombea lakini sasa nasema wazi sitorudi nyuma,” alisema Mnsour.

Mansour alisema katika harakati zake za kuwania uwakilishi katika jimbo hilo ataomba kura hata katika matawi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani ni yeye ndiye aliyejenga matawi hayo.
“Sitoogopa kuingia katika tawi lolote la CCM kuomba kura, yote nimejenga mwenyewe, nitakwenda humo humo, hizi ndiyo siasa za CUF za leo, CCM na CUF wote wangu,” alisema Mansour.
Mansour alisema hajuti kufukuzwa kwake CCM wala hawezi kumnunia mtu yeyote lakini akasisitiza ataendelea kuwaheshimu kwa vile ni chama chao.
Alisema mwaka 2010 yalipokuwapo mazungumzo ya maridhiano aliwaambia wananchi wa Kiembesamaki umuhimu wa maridhiano hayo katika kujenga jamii iliyotulia Zanzibar.
Alisema ingawa wawakilishi wengi walipinga ndani ya Baraza la Wawakilishi lakini hakutetereka kwa kuwa aliamini lengo la maridhiano haikuwa ni kumtengenezea Seif nafasi ya uongozi au mawaziri saba kutoka CUF.
“Maalim hana njaa, mawaziri hawana njaa, lengo ni kuleta utulivu, Maalim anaumwa na siasa hizi za ufisadi, lengo ni kuondoa chuki na kujenga historia mpya na kujenga vyombo vya Serikali vinavyowajibika kwa dola,” alisema Mansour.
Katika mkutano huo, Makamu wa Kwanza wa Rais Serikali Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Seif Sharif Hamad aliwataka viongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar kusoma sheria ya vyama vya siasa na kuacha kuiburuza CUF.
Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alilazimika kutoa ushauri huo baada ya kile kinachodaiwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mjini kuuzuia mkutano kwa sababu zisizoeleweka.
Alisema CUF haitaweza kuendelea kuvumilia uonevu unaofanywa na jeshi hilo kwa kuzuia mikutano yao kwa sababu chama hicho kina haki sawa katika serikali ya umoja wa taifa kama ilivyo CCM.
Akizungumzia hatua ya Mansour, Seif alisema Mansour ndiye mgombea sahihi wa Kiembesamaki kwa Chama cha Wananchi (CUF).
Mtanzania

No comments: