ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 27, 2015

Mavazi ni sehemu ya kampeni Nigeria

Bango likimwonyesha rais Goodluck Jonathan mjini Abuja, Nigeria. (Chris
Wananchi wa Nigeria wanapiga kura Jumamosi March 28 katika uchaguzi mkuu wa rais unaowapambanisha kiongozi wa sasa Goodluck Jonathan na kiongozi wa zamani Muhammadu Buhari. Wanapoingia jukwaani katika kampeni wananchi wengi wanataka kuona wagombea hawa wamevaaje.
Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria na mpinzani wake Jen. Muhammadu Buhari

Wakati suti na tai ya kimagharibi ndio staili inayotumiwa na marais na mawaziri wakuu sehemu nyingi barani Afrika, nchini Nigeria, taifa lenye watu wapatao milioni 174 na lugha kadha tofauti, kuvaa nguo za kiasili ni muhimu sana katika kujitambulisha na wapiga kura.

Katika kipindi cha mwezi uliopita wote Rais Jonathan na mpinzani Muhammadu Buhari wamekuwa wakikonga nyoyo za watu kwa mavazi ya kiasili kulingana na sehemu ya nchi wanapofanya kampeni, kuanzia mavazi ya agbada yanayopendelewa na watu wa kabila la Hausa waliopo kaskazini mwa nchi, mpaka kofia nyekundu za tunga zinazopendelewa sana watu wa kabila Igbo, yote katika hatua za kuvutia kura.

“Ni muhimu kwa yeyote yule anayegombania urais Nigeria kujaribu kuvutia makundi ya watu mbali mbali nchini, “ anasema Abubakar Kari, mwalimu katika chuo kikuu cha Abuja. “Moja ya njia kuu ya kufanya hivyo ni kwa mgombea kuvaa kama vile wanavyovyaa wale watu anaojaribu kuwaomba kura zao.”

Kwenye moja ya barabara kuu mjini Abuja, mji mkuu wa wa Nigeria, mabango yanayomwunga mkono Bw Jonathan yanamwonyesha akitabasamu huku akiwa amevaa shati aina ya polo na staili ambazo zinatumiwa sana katika eneo la Niger Delta. Bw. Buhari naye anatumia mkakati huo huo. Wakati katika mitandao ya kijamii anakuwa amevaa suti na tai anajulikana zaidi kutokea katika mabango na mikutano akiwa amevaa agbada – maarufu katika maeneo ya wahausa kaskazini mwa nchi.

Vazi ambalo Buhari havai ni la kijeshi, licha ya kuwa alikuwa jenerali wa jeshi ambaye alipindua nchi katika mapinduzi ya mwaka 1983, kabla na yeye kuondolewa madarakani na jeshi miaka kadha baadaye.

Chanzo: VOA

No comments: