Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe.
Jeshi la Polisi mkoani Kagera, limewatia mbaroni watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na mifupa ya viungo vya mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi
(albino), Zeulia Justus, aliyefariki dunia mwaka 2006 baada ya kujifungua mtoto katika kijiji cha Rushwa Kata Mshabago Tarafa ya Nshamba Wilaya ya
Muleba, mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Lutozi (66) na Emmanuel Karoli (50), wakazi wa
Kijiji cha Kyota Tarafa Kimwani wilayani humo.
Mwaibambe alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na mifupa mitatu ya mwanamke huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kijijini
humo kuwa kuna watu wanauza viungo vya albino kwa Sh. milioni tatu.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 20, mwaka huu, wakiwa na mfupa mmoja na walipopekuliwa kwenye makazi yao, walikutwa na mifupa
mingine miwili.
“Katika mahojiano, watuhumiwa hawa walikiri kwamba, mifupa hiyo ni ya albino aliyefariki mwaka 2006 katika Kijiji cha Rushwa, Kata Mshabago,
Tarafa Nshamba, wilayani Muleba,” alisema Kamanda Mwaibambe.
Alisema watuhumiwa hao walidai kuwa mifupa hiyo waliipata baada ya kufukua kaburi alimozikwa albino huyo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga
wa jadi, Mutalemwa Revocatus.
Mwaibambe alisema polisi waliiomba mahakama mkoani hapa kibali cha kufukua kaburi na kupewa.
Alisema polisi walikwenda kwenye kaburi hilo Machi 23, mwaka huu na kulifukua na kujiridhisha kuwa mifupa hiyo ilikuwa ni ya viungo vya albino
huyo.
Mwaibambe alisema polisi wanamsaka mganga huyo kwa tuhuma za kuwashawishi watuhumiwa kufukua kaburi la albino huyo na kuchukua mifupa ya
viungo vyake.
Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa atakayemuona kwa kutoa taarifa polisi ili mganga huyo akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu
mashtaka.
Alisema atakayetoa taarifa na kuwezesha kukamatwa kwa mganga huyo, jeshi hilo litampa zawadi nono.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Mbaroni ya nini PIGA RISASI
Post a Comment