Mada inajieleza hapo juu, kutokana na visa na uzoefu mbalimbali waliopitia, wanawake wamekuwa na mtazamo tofauti juu ya wanaume ambao wanatumia kilevi.Wapo wanaoamini kwamba mwanaume ambaye anatumia kilevi hafai kuwa mume lakini wapo wengine ambao wanaamini kwamba anafaa.
Wale wanaosema hafai wanakuwa na hoja zao mkononi lakini hata wale ambao wanasema anafaa, nao wanakuwa na hoja zenye mashiko.
Kabla hatujaanza kujadili kwa kina mada hii, tupate mfano mmoja kutoka kwa msomaji ambaye alinitumia ujumbe mfupi kuomba msaada kuhusu mpenzi wake ambaye alidai anapoteza sifa za kuwa mume kutokana na utumiaji wa kilevi.
“Naomba msaada wako anko kwani nimeteseka kwa muda mrefu, nimekuwa siishi kwa amani na mpenzi wangu kutokana na ulevi. Akishakunywa kidogo tu, hamuelewani.
“Mkikutana ni ugomvi mwanzo mwisho, ananitukana matusi ya nguoni, ananiambia sistahili kuwa mkewe, ananiambia mimi ni masikini tu, amenichukua ili kunisaidia maana maisha yangu na ndugu zangu wote ni kapuku hivyo nikiendelea kumsumbuasumbua ataniacha na umaskini wangu. Hana malengo ya mbeleni, yeye ni kutumia mwanzo mwisho.”
Kwa mfano huo, mwanamke huyo anaonesha dhahiri kwamba hawezi kumuona mwanaume anayetumia kilevi kwamba ni sahihi kwake, ataamini kabisa kwamba kilevi ndicho kinachosababisha mpenzi wake huyo amfanyie vituko na penzi lao kusuasua.
POMBE NDIYO CHANZO CHA TATIZO?
Ukweli ni kwamba, pombe ni kichocheo tu cha mtu mwenye tabia mbaya kufanya ubaya wake. Pombe pekee haimsababishi mtu afanye tukio baya bali mtu mwenye tabia mbaya anapoongezea na pombe ndipo anapata nguvu zaidi kufanikisha azma yake.
Ukiona mtu anakutukana, anakukashifu, anakutendea ubaya wa aina yoyote anapokuwa amelewa basi ujue ndiyo tabia yake hata kama anakuwa hajalewa.Ndiyo maana utawasikia watumiaji wa pombe wakikwambia, ngoja nimnywee ili nikamchambe fulani. Mawazo ya kwenda kumchamba fulani huwa yanakuja kabla hajanywa lakini anakwenda kunywa ili kupata chachu ya kutimiza tabia yake mbaya.
MNYWAJI ANAFAA KUWA MUME?
Kimsingi anayekunywa pombe anaweza kuwa mume kama ataweza kuifanyia kazi tabia yake na kuamua kubadilika, mwanamke ambaye anakutana na mwanaume wa aina hii, anaweza kufanikiwa kumfanya mwanaume huyo kuwa mume.
Ambadilishe tabia kwa kutumia lugha nzuri, usimfanye ajione mkosaji kwa kitendo chake cha kuwa mnywaji. Mueleze kistaarabu kwamba anapaswa kubadilika tabia yake kwanza ili muweze kuishi kwa amani na upendo.
MATHARA YA POMBE
Mueleze kwamba pombe inachochea matatizo mengi hususan pale anapokunywa kupindukia. Maamuzi yanakuwa si ya akili yake pale tu ulevi unapokuwa umemkolea. Ni vyema akapunguza unywaji, akanywa kidogo kiasi cha kujitambua na kuweza kufanya uamuzi sahihi.
Mueleze kwamba unywaji pombe kupita kiasi ni hasara. Gharama hizo ni bora akaelekeza nguvu na fedha zake katika mambo mengine ya maendeleo.Unatakiwa kumueleza kwamba, ili muwe na mipango endelevu, abadili tabia na kweli uone amebadilika. Aoneshe kwa vitendo kuwa amebadilika, pombe isiwe kisingizio, akibadilika anaweza kuwa mume.
MPE MUDA
Baada ya kumpa ushauri wa kubadilika kitabia, kama kweli ni muungwana atabadilika. Atakuwa mume, mtaishi vizuri. Tabia itakuwa njema, awe amekunywa au hajanywa. Asipobadilika tabia, hafai ni bora ukajiepusha naye mapema na kusubiri yule ambaye atakuwa msafi kitabia.
GPL
No comments:
Post a Comment