Viongozi wa Chama Cha Albino Tanzania wakiwasili Ikulu jijini Dar es salaam leo Alhamisi Machi 5, 2015 kuonana na Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyewakaribisha ili kuwasikiliaza matatizo yao na kujadiliana nao mikakati ya namna ya kukomesha ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini
Rais Kikwete akisalimiana na Viongozi wa Chama Cha Albino Tanzania Ikulu jijini Dar es salaam leo Alhamisi Machi 5, 2015 alipowakaribisha ili kusikiliza matatizo yao na kujadiliana nao mikakati ya namna ya kukomesha ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini
Rais Kikwete akiongea na Viongozi wa Chama Cha Albino Tanzania Ikulu jijini Dar es salaam leo Alhamisi Machi 5, 2015 alipowakaribisha ili kusikiliza matatizo yao na kujadiliana nao mikakati ya namna ya kukomesha ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini
Dr Possy akimsomea Rais Kikwete Mapendekezo ya Viongozi wa Chama Cha Albino Tanzania juu ya namna ya kupambana na kukomesha ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini
Dr Possy akimkabidhi Rais Kikwete Mapendekezo ya Viongozi wa Chama Cha Albino Tanzania juu ya namna ya kupambana na kukomesha ukatili na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini
PICHA NA IKULU
MAPENDEKEZO YAMEAMBATANISHWA HAPO CHINI BOFYA SOMA ZAIDI
MAPENDEKEZO KWA DK. JAKAYA KIKWETE, RAIS
WA JAMHURI YA MAUUNGANO WA TANZANIA KATIKA KIKAO CHAKE NA WAWAKILISHI WA CHAMA
CHA ALBINO TANZANIA, IKULU, TAREHE 5/3/2015
JUU YA NAMNA YA KUSAIDIA KUKOMESHA MAUAJI, UKATAJI VIUNGO, UTEKAJI NA
UKATILI DHIDI YA WATU WENYE UALBINO NA FAMILIA ZAO
Mh. Rais,
Kutokana na kuendelea
kushamiri kwa mauaji, ukataji viungo, utekwaji na ukatili dhidi ya watu wenye
ualbino na familia zao, Chama Cha Albino Tanzania kina mapendekezo yafuatayo
kwako:
1.
Ushughulikiwaji
wa kesi zinazohusiana na mauaji, ukataji viungo, utekwaji na ukatili wa aina
hiyo kwa watu wenye ualbino upewe kipaumbele, kupitia mkakati maalum, kwamba:
a.
Mashauri yote
ambayo hayajapelekwa mahakamani uchunguzi na upelelezi ukamilishwe mapema na
yapelekwe mahakamani;
b.
Kesi zilizoko
mahakamani zisikilizwe mapema, kupitia mahakama au utaratibu maalum na kwa
watakaokutwa na makosa hukumu itekelezwe mara moja;
c.
Kuwepo mpango
maalum wa kufuatilia kesi hizi, hasa kupitia Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora, ili kutoa msaada wa kisheria ikiwemo kwa wale ambao
hawajaridhishwa na maamuzi ya mahakama waweze kukata rufaa.
2.
Ulinzi shirikishi
katika jamii uimarishwe katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya vijiji au mitaa
zijengewe uwezo ili ziwe na mipango maalum ya kutoa ulinzi kwa watu wenye
ualbino kwa kushirikiana na jamii kwani pia wao ndio wanaowatambua wageni na
kupitia wao ni rahisi hata kupata ushahidi katika kesi mbalimbali. Ni rahisi
pia kupitia kamati hizi kuzitambua kaya zilizoko katika mazingira ambayo sio
salama na kufanya uraghbishi, ikiwemo kuzihamishia katika makazi salama.
3.
Serikali iwe na
mkakati maalum, endelevu na shirikishi wa kuelimisha jamii juu ya ualbino na
haki za binadamu na mpango huu wa elimu kwa jamii uwe na bajeti maalum ambayo
itakuwa vyema kwa kuanzia ijadiliwe katika bunge lijalo la bajeti;
4.
Wahanga wa
matukio haya wakiwemo watoto wasaidiwe ili kuboresha maisha yao na kuwajengea
misingi mizuri ya maisha ya baadae:
a.
Watoto walio
katika kambi wasaidiwe kupata mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, afya,
malazi na mavazi kupitia serikali;
b.
Kambi hizi
ziangaliwe kwa namna pana, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo kupitia vyuo
mbalimbali vijana walioishi kwa muda mrefu kambini ili waweze kujitegemea na
pia kupunguza athari nyingine zinazoweza kutokea,ikiwemo mimba na
udhalilishwaji wa kingono kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa katika taarifa
mbalimbali;
c.
Watu wazima
wanaoishi katika kambi hizi wasaidiwe kuishi maisha ya staha, ikiwemo kupata
ajira japo ndani ya kambi hizo hizo ili waweze kujikimu na kutoa mchango wao
kwa kuwatunza watoto wakati huu ambao hawawezi kurudi nyumbani;
d.
Wale waliopata
ulemavu au kujeruhiwa serikali iwasaidie waweze kujimudu. Kuna ambao maisha yao
yamekuwa ya magumu sana kwa mambo mengi hivyo kuwa mzigo mzito kwa familia zao
ambazo nazo nyingi ni masikini;
e.
Kambi hizi
zisichukuliwe kama za kudumu,ila zijengewe mazingira ya kutoa elimu jumuishi,
kuanzia elimu ya awali;
f.
Wahanga na
familia zao wapewe ushauri (counseling) kwani wengi huwa wanaathirika sana
kisaikolojia na hapajawa na mkakati wa kuwafuatilia.
5.
Kwa kuwa mauaji
yanayoendelea yanatokana na imani za kishirikina, na katika matukio waganga wa
kienyeji wanahusika, Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala pamoja na Sheria ya
Uchawi zipitiwe upya, zifanyiwe maboresho ili kuweza kutofautisha vizuri juu ya
aina hizi za tiba au huduma, na jamii ishirikishwe katika uratibu wa shughuli
za waganga wa tiba mbadala au tiba asili.
6.
Kiundwe Kikosi
Kazi maalum kufanya uchunguzi wa kina kubaini wanaotuma na wanaoununua viungo
vya watu wenye ualbino ili washughulikiwe na kuondoa kabisa jambo hili ambalo
limekuwa na kadhia kubwa kwa watu wenye ualbino, familia zao na jamii na Taifa
kwa ujumla.
7.
Itengenezwe
kanzidata (database) kwa watu wenye ualbino kote nchini ambayo itakuwa na
taarifa mbalimbali (demographic information), zikiwemo idadi na mahali (makazi);
jinsi na umri; elimu na ajira na; hali ya saratani ya ngozi, ili kuisaidia
serikali na wadau wengine waweze kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya
ulinzi na jinsi ya kuboresha maisha ya watu wenye ualbino kwa ustawi wa jamii
na maendeleo ya Taifa letu.
8.
Tunapendekeza
kukawepo na Kamati Maalum ya Kitaifa, ambayo ni jumuishi, iwe inakutana kwa
vipindi maalum (mara kwa mara) kila mwaka kujadili, kutoa mrejesho na kuishauri
serikali na wadau wengine. Kamati hii iwe chini ya Ofisi ya Rais au Makamu wa
Rais au Waziri Mkuu ili iwe rahisi kuratibu mambo yake kwa kushirikiana na
Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu. Kwa kuanzia, kamati hiyo pia ifuatilie
utekelezaji wa mapendekezo haya kama ambavyo utaona yafaa, Mh. Rais.
Mh. Rais tunakushukuru sana
kwa kutusikiliza. Mapendekezo haya na mengine yatakayochangiwa na wadau
yatasaidia kukomesha mauaji na kuwafanya watu wenye ualbino na familia zao
kuishi kwa amani kama watu wengine. Utayari wetu wa kushirikiana nawe na
serikali yetu kama ambavyo tumekuwa tukifanya wakati wote hauhitaji msisitizo.
_________________
Ernest N. Kimaya
Mwenyekiti wa Chama Cha Albino Tanzania
1 comment:
Aibu kubwa sana kwa taifa. Sasa hivi ukiandika neno Albino kwenye mtandao Tanzania inatokea. Hawa investors tunawatafuta tutawatoa wapi ? Kikwete aondoke tu
Post a Comment