Shabiki wa Newcastle John Kearsley aliyeuawa na Pundamilia.
Mwandishi wetu
INASHANGAZA! Shabiki mmoja aliyekuwa amevalia jezi ya timu ya Newcastle, John Kearsley (38) ameuawa baada ya kukanyagwa na pundamilia alipokuwa matembezini katika mbuga za wanyama nchini Tanzania.
John, alikuwa na ziara ya siku 12 nchini Tanzania ambayo aliiandaa kwa muda mrefu kwa lengo la kusherehekea kutimiza miaka 10 ya ndoa yake na mkewe, Doreen akiongozana na ndugu zake wawili katika ziara hiyo iliyoishia kwa majonzi.
Kwa mujibu wa Gazeti la Sunday Sports la nchini Uingereza na ripoti ya tume ya uchunguzi, kabla hawajaingia mbugani hapo, John alikuwa amekunywa pombe nyingi sambamba na vilevi vingine ambavyo havikubainishwa.
Mke wa John, Doreen aliliambia gazeti hilo kuwa, baada ya mumewe kumuona pundamilia alianza kumdhihaki na kumchezea. “Kila mara John alikuwa akipenda kuchekacheka hovyo na kufanya kama utani na alipomuona pundamilia alisema ‘hoy hinniny’ nafanana na mwili wa pundamilia.
“Niwe mkweli tu, mambo mengi aliyokuwa akifanya, aliyafanya kwa utani na alichokuwa akitaka ni kufananisha jezi yake na ngozi ya pundamilia. Alishuka kwenye gari letu (Toyota, Land Rover) na kumfuata pundamilia aliyekuwa umbali wa kama mita 100 huku akimuonesha fulana yake (yenye rangi ya pundamilia),” alisema Doreen.
Doreen aliongeza kuwa pundamilia huyo mwenye jinsi ya kiume, alimfuata John na kumpiga kikumbo kilichomuangusha chini na kisha akaanza kupigwa mateke. Alisema kuwa punda huyo alimuumiza sana mumewe na kumsababishia kifo baada ya saa kadhaa kupita bila kupatiwa huduma ya haraka.
Taarifa juu ya kufariki kwa John zilitangazwa baadaye na timu ya madaktari baada ya kufika eneo la tukio kwa kutumia helkopta.
GPL KWA MSAADA WA MTANDAO
No comments:
Post a Comment