Advertisements

Tuesday, March 31, 2015

SHERIA HAILAZIMISHI KUTOA MATUNZO YA MTOTO KULIKO UWEZO WAKO.

Na Bashir Yakub.

Suala la matunzo ya watoto/mtoto lim ekuwa ni suala ambalo wasomaji wengi wamekuwa wakiniuliza sana. Wengi wao wanaouliza ni wale ambao wamezaa nje ya ndoa na hivyo kuna utata wa matunzo ya watoto na wale ambao wamekuwa wana ndoa lakini sasa tayari wametengana aidha kwa talaka au bila talaka. Niseme tu kwa ufupi kuwa suala la matunzo ya watoto linajumuisha mambo mengi nami nitaeleza baadhi tu. 1.

HUWEZI KUMLAZIMISHA MTOA MATUNZO KUTOA AMBACHO HANA. Kumekuwepo na tabia ya wazazi hasa upande wa wazazi wa kike kuwalazimisha wanaume ambao wamezaa nao na kutengana nao kutoa matunzo ya watoto kwa kiwango cha juu kabisa ambacho pengine kinazidi hata kipato cha mtoaji.

Hili si sawa. Ni kweli sheria inamlazimisha mwanaume kutoa matunzo ya mtoto lakini haimlazimishi kutoa kuliko anachopata. Sheria haiseme kwakuwa mwanamke anaishi na mtoto wa mtu basi mwanaume ndio sasa afanywe kitega uchumi.

Inafikia hatua mwanamke hafanyi kazi yoyote isipokuwa anategemea ile pesa ya matunzo ya mtoto ndio iwe kila kitu katika maisha yake. Hii ndio sababu hata akipewa kiasi kinachotosha haoni kama kinatosha kwakuwa kinakuwa na njia nyingi kama saluni, nguo za kuvaa, pesa ya upatu, michango ya harusi na kitchen party na kila kitu kinachohusu maisha yake binafsi.

Ieleweke wazi kuwa kwa mujibu wa sheria pesa ya matunzo ya mtoto haihusiki na haya. Pesa ya matunzo ya mtoto ni pesa ya matunzo ya mtoto kama neno lenyewe lilivyo na linavyojieleza si vinginevyo.

2.INARUHUSIWA KUKATAA IKIWA UNALAZIMISHWA KUTOA MATUNZO YANAYOZIDI UWEZO WAKO. Ikiwa mwanaume analazimishwa kutoa kuliko kipato chake basi anaruhusiwa kukataa hata kama amri hiyo imetolewa na mahakama. Wengine huandikishana polisi lakini bado haibadili maana kwakuwa mtu anatakiwa kutoa kulingana na uwezo wake au kipato chake. Wapo wazazi hasa wa kike ambao huwalazimisha wanaume kutoa matunzo ya kuwasomesha watoto international schools wakati kipato cha mwanume ni shule ya kata.

Sheria inachokataza ni kukataa kabisa kutoa matunzo ya mtoto lakini haimlazimishi mtu kutoa kilichomzidi. Au wengine hulazimisha kuwekewa mpaka wafanykazi wa ndani( house girl) wakati kipato cha mwanaume hakiruhusu jambo hilo. Huu nao ni unayanyasaji kwa upande wa wanaume na haukubaliwi na sheria.

La msingi ni kuwa iwapo utalazimishwa kutoa kuliko uwezo wako we kataa. Na kama uamuzi huo umetolewa na mahakama basi kataa kwa kukata rufaa kupinga kabisa jambo hilo. Sheria inaposema matunzo ya watoto haisemi kuwa watu watoe kuliko uwezo wao hapana. Sheria ni haki na haki huzingatia ukweli na hali halisi ya jambo.

3. UMRI WA WATOTO KUISHI NA MAMA AU BABA. Mara nyingi sheria imeelekeza watoto walio chini ya umri wa miaka kumi yaani kuanzia miaka tisa kushuka chini kuishi na mama. Aidha kuanzia miaka kumi kwenda mbele mtoto anaweza kuchagua aishi na nani kati ya baba au mama.

Kwahiyo iwapo mtoto amefikisha umri wa miaka kumi au zaidi basi baba anaweza kumchukua mtoto wake iwapo pia mtoto atapenda kukaa na baba yake. Wapo wazazi ambao wamekuwa wakiwagangania watoto hata baada ya watoto kuvuka umri huo ili waendelee kuwafanya vitega uchumi kupitia kudai matunzo. Hili si sawa hasa iwapo mtoto yuko tayari kukaa na baba yake.

4. BABA ANAWEZA KUOMBA KUKAA NA WATOTO HATA KAMA NI WADOGO SANA. Hapo juu tumeona kuwa ni lazima mtoto kukaa na mama iwapo ana umri chini ya miaka kumi. Msimamo huu unaweza kubadilika iwapo baba atatoa sababu za msingi za kuomba mama asikae na watoto. Hii haijalishi watoto wana umri gani iwapo tu ana sababu za msingi basi ataomba kukaa na watoto/mtoto wake. Sababu kubwa za kuomba watoto ni iwapo mama ana ugonjwa wa akili na hivyo kuwa hatari kwa ustawi wa mtoto/watoto.

Pia iwapo mama anakaa na watoto katika mazingira hatarishi kama danguro, baa, sehemu za madisco, au mama anajihusisha na vitendo vya ukahaba ambavyo si vyema kabisa kwa makuzi ya mtoto. Hii inajumuisha matendo yote maovu ambayo kukaa na watoto/mtoto yanaweza kuleta athari mbaya kwake na ni hapo baba atakapoomba kuchukua mtoto/watoto na atakubaliwa bila kujali umri wa watoto.

5. HAKI YA KWENDA KUWAONA WATOTO. Wapo watu ambao huzuiwa kuwaona watoto. Wengine huruhusiwa lakini kwa masharti maalum na kwa kupewa muda wa kuzungumza. Hii haikubaliki kisheria mzazi anapaswa kuwaona watoto kwa uhuru na bila masharti yanayolenga kumwondolea haki hiyo.

Ikiwa mzazi anazuiwa kuwaona watoto/mtoto au anawekewa masharti magumu basi anaweza kudai haki hii kwa kupeleka malalamiko ustawi wa jamiii au mahakamani haraka iwezekanavyo. MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com. KUPATA USHAURI WA SHERIA ZA ARDHI, NDOA, MIRATHI, MAKAMPUNI,N.K TEMBELEA sheriayakub. blogspot. Com

No comments: