ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 31, 2015

UCHAGUZI MKUU: Mwezi mgumu kwa Lowassa

Dar es Salaam. Kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kitafikia katika hatua ngumu mwezi ujao kitakapochukua uamuzi mgumu dhidi ya baadhi ya makada wake walioonyesha nia ya kuwania urais, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Kiongozi huyo pamoja na makada wengine sita wa CCM, walipewa kifungo cha miezi 12 kwa madai ya kuanza kampeni za urais mapema kinyume na taratibu za chama hicho iliyomalizika katikati ya mwezi uliopita na sasa wanasubiri kwa hamu, tangazo la Kamati Kuu (CC-CCM) ili wawe huru kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho na kuendelea na shughuli nyingine za kujiandalia mazingira ya kupitishwa.
Mbali ya Lowassa, wengine waliofungiwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinasema baadhi ya wagombea huenda wakaongezewa adhabu kutokana na kuendelea na kampeni kabla ya wakati wake na kwenda kinyume na taratibu za chama hicho.
“Kuna wagombea wataongezewa adhabu kwa kukiuka utaratibu wa chama kwa kuendelea kufanya kampeni za mapema,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hana taarifa kwa kuwa uchunguzi dhidi ya makada hao bado haujakamilika. “Uchunguzi hata nusu haujafika. Kuna watu wanahangaika kwa sababu hawana sifa za kutosha na ndiyo wanaotengeneza hizo taarifa,” alisema Nape na kuongeza:
“Mtu yeyote ambaye hajavunja taratibu hana sababu ya kuwa na hofu na kama kuna watu wamevunja taratibu hawana namna ya kukwepa mkono wa chama.”
Hivi karibuni, kumeibuka wimbi la watu wa kada mbalimbali kujitokeza kwa makundi kwenda nyumbani kwa Lowassa Mjini Dodoma, kumshawishi achukue fomu za kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi hatua ambayo ilikemewa na Nape ambaye alimtaka kuacha mara moja.
Hivi karibuni, Nape alikaririwa na vyombo vya habari akisema vitendo vinavyofanywa na Lowassa ni kampeni za wazi za urais kabla ya muda kufika na hivyo kukiuka kanuni za chama hicho kitendo kinachoweza kumnyima sifa za kugombea nafasi ya urais.
“Anachokifanya Lowasa ni kuvunja kanuni na kiburi, ni matendo ya wazi ya kampeni, bila shaka anajua adhabu yake. Matendo hayo yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia CCM,” Nape alikaririwa akisema.
Alisema Lowassa ni miongoni mwa makada ambao walipewa adhabu na mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.
Lowassa alijibu onyo hilo la Nape kwa kuyazuia makundi hayo kuendelea kufika kwake kumshawishi lakini akihoji kuwa kauli hiyo imetokana na uamuzi wa kikao gani ndani ya CCM. Alisema hayo siku ambayo aliwapokea vijana waendesha pikipiki(bodaboda) zaidi ya 60 na wananchi wa kawaida waliokuwa wamefunga safari kutoka Mbarali Mkoa wa Mbeya kwenda kumshawishi agombee urais.
Lowassa alisema CCM ina utaratibu wake wa kujadili mambo kama hayo.
Mbali ya vijana hao kundi jingine lililokwenda kwa Lowassa ni la wachungaji ambao walimweleza kwamba wameamua kumshawishi wakiamini kuwa ndiye chaguo sahihi kwao.
Kundi la kwanza kwenda kumshawishi Lowassa lilikuwa la Masheikh 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo, Pwani ambalo alilieleza kwamba ameshawishika kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya watu walioshiriki katika safari hizo za ushawishi wamejikuta katika wakati mgumu kutokana na kuhojiwa na baadhi ya taasisi zikiwemo vyuo na za dini kujitokeza na kusema hazihusiki na suala hilo.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alijitokeza na kulaani kitendo hicho akisema si cha kiungwana na kwamba kila mgombea anaweza kufanya hivyo, lakini wanaheshimu kanuni na katiba ya CCM.
January alipoulizwa jana kuhusu kuongezwa kwa adhabu kwa baadhi ya makada, hakusema kama anazijua au hazijui taarifa hizo lakini alieleza kuwa kati ya watu waliopewa onyo wapo waliobaki kwenye misingi na wengine wameendelea kukusanya makundi... “Ushahidi unakusanywa na wale ambao hawakubaki kwenye misingi watachukuliwa hatua.”
Ofisa Habari wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema jana kwamba hawajasikia lolote kuhusu kuongezwa adhabu kwa baadhi ya wagombea waliokuwa wamefungiwa.
MWANANCHI

No comments: