Advertisements

Tuesday, March 31, 2015

MIMI ‘MTU WANGU MZUNGU’ NDIYO NINI SASA? - 2


Karibuni sana wasomaji wangu wapendwa katika safu hii maalum kwa ajili ya kuelekezana mambo mbalimbali yanayohusu maisha kwa ujumla hasa upande wa mapenzi kama siyo mahaba.Mfano wa mambo hayo ni namna wenza wanaoishi na ndugu au wazazi wao wanavyopaswa kuishi kwa hekima bila kuwakwaza.

Kujiepusha na kauli zisizofaa ambazo mara nyingi zimekuwa zikiharibu uhusiano wao, kujiweka katika mazingira ya usafi wa nyumba na mavazi.Mambo mengine ni kuwa waaminifu katika uhusiano wao kwa sababu wenza wakiwa na michepuko huweza kuleta maradhi ndani ikiwa ni pamoja na migogoro inayosababisha kuachana.

KWA NINI UZUNGU UAMBATANE NA USALITI?
Wiki iliyopita tuliishia kwenye neno hili; ni sababu mbaya sana kusema ‘mtu wangu Mzungu’. Kisa hakuchunguzi, hakufuatilii.

Wengi wanaotoa madai au sifa hizo ni wale wasio na uadilifu na siku zote watu wasio na uadilifu ndiyo wanafurahia sana maisha ya kutofuatiliwa.Ukimwona mtu anasema mtu wake ni Mzungu maana yake ana mambo yake mengi ya siri lakini hayafuatiliwi kiasi cha kuwa kukamatwa au kujulikana nyendo zake.

Hii sifa imeshamiri sana katika jamii ya ‘Kiswahili’. Lakini wewe msomaji wangu ambaye upo katika uhusiano, chukulia kwamba, una mwenza anakusaliti lakini wewe hujui kwa sababu hufuatilii na unaitwa Mzungu. Je, siku ukijua Uzungu utauonaje?

DHANA MBAYA KUWA NZURI
Mambo ya kutofuatiliwa yanaambatana na mawazo ya ubaya kuwa mzuri. Kwa nini nasema hivi? Kuna watu wanadiriki kusema hadharani maneno haya:“Mimi bwana simu yangu mwenzangu hashiki kabisa. Mimi sishiki yake na yeye hashiki yangu.”Hawa wanaosema hivi ni wana ndoa zaidi. Wanamwagiana sifa kwa kila mmoja kutoshika simu ya mwenzake, kwamba ni sifa kwao.

Lakini kusema ule ukweli, hata wewe msomaji tafakari kwa makini sana ukitumia akili za ndani. Je, ni sawa kwa wanandoa kuogopana kwenye simu? Mna nini cha siri ambacho mwenzako hatakiwi kushika?
Kama ni kitu cha siri, siri gani mwenza wako asiijue. Ni usaliti tu na si lingine. Nadhani kama mwana ndoa ana akili zake timamu, hata kama hashiki simu ya mwenzake, lakini si suala la kulisema bayana, ni aibu!

MZUNGU MWENYEWE SASA
Kama utamkuta Mzungu anayesifiwa kwa kutokuwa na tabia ya kufuatilia mambo ya watu, atakwambia sababu kubwa ni kuamini.Niliwahi kuzungumza na mtu (Mzungu) mmoja anaitwa Frank, alisema kuwa, kwa Wazungu mtu kufumaniwa ni nadra sana kwani walio wengi ni waaminifu.

Alisema Wazungu wanaofumaniwa historia zao zinaonesha kuwa, alishatoka Uzunguni na kwenda kuishi mbali na kujikuta akibeba tabia za ugenini.Kwa hiyo ninapenda kumalizia mada yangu leo kwa kusema kwamba, matumizi ya neno ‘mi mtu wangu Mzungu’ yasiambatane na usaliti wowote. Wapo wenza ambao hawaaminiki si kwa sababu wasiowaamini wana tabia za wivu uliopitiliza, bali kwa sababu ya matukio mbalimbali ya usaliti ya hao wasioaminika!

KUNA HULKA YA USALITI
Mbaya zaidi ni pale baadhi ya wenza kuwa na hulka ya usaliti. Wapo ambao hata akinaswa akisaliti si dawa ya kuachana na tabia hiyo, hao ndiyo wale ambao hupenda kuwaita wenza wao Wazungu. Tujisahihishe kuhusu hilo.Huu mwisho wa makala hii, tuungane wiki ijayo katika makala nyingine.

GPL

No comments: