Swahili Blues Band ya Tanzania ikiwa katika uwanja wa kimataifa wa Mwl JK Nyerere tayari kuanza safari ya kuelekea mjini Addis Ababa.
Bendi ikikaribishwa rasmi na mwenyeji wao Dr Mulatu katika klabu ya African Jazz Village
Leo Mkanyia akihojiwa na moja ya redio ya Addis Ababa akiwa na Dr Mulatu
Leo Mkanyia and Swahili Blues Band iko mjini Addis Ababa Ethiopia kwa mwaliko maalumu toka kwa gwiji la muziki barani Afrika na ulimwenguni kote Dr Mulatu Astakte.
Swahili Blues Band ilifika mjini Addis Ababa siku ya tarehe 16 Machi 2015 na wanatarajiwa kurudi mjini Dar es Salaam siku ya tarehe 16 April 2015. Bendi hiyo imepata mwaliko huo mahususi baada ya Dr Mulatu, maarufu kama King of Ethio- Jazz, kupata wazo la kufanya utafiti wa muziki halisi kutoka Afrika Mashariki. Katika mpango huo Dr Mulatu ataalika bendi moja kutoka Kenya na Uganda vilevile baada ya Swahili Blues Band kumaliza muda wao mjini Addis Ababa. Kwa mujibu wa kiongozi wa Bendi Bwana Leo Mkanyia, Dr Mulatu alifanya mawasiliano nao baada ya kufanya utafiti wake mwenyewe kwa bendi kadhaa za Kitanzania na hatimaye akaamua kuwa Swahili Blues Band iwakilishe muziki kutoka Tanzania. Mkanyia aliendelea kusema kuwa Dr Mulatu alipendezwa na muziki wao huo ulio na mizizi ya mirindimo ya kitamaduni kutoka Tanzania na vionjo vya kimataifa.
Bendi hiyo imepangiwa kufanya maonyesho kadhaa mjini Addis Ababa na makao yao makuu yatakuwa katika klabu maarufu na ya kisasa kabisa inayomilikiwa na Dr Mulatu ijulikanayo kama African Jazz Village. Bendi hiyo iliianza onyesho lao la kwanza siku ya Jumamosi ya tarehe 21 Machi ambapo mamia ya watu kutoka mataifa mbalimbali walionekana kukunwa vilivyo na muziki huo wa kitanzania. Wapenzi hao walionekana kuguswa zaidi na nyimbo kama Afrika, Mdundiko, Moro Moro na Wazazi Wangu kujaribu kuzitaja kwa uchache.
Swahili Blues Band wataendelea kuwaburudisha wakazi wa mjini Addis Ababa mwishoni mwa wiki hii ambapo wanatarajia kushirikiana na wanamuziki mbalimbali maarufu kutoka Ethiopia. Mmoja aliyedokezwa kufanya ushirikiano huo ni mpuliza saxophone maarufu ajulikanaye kama Danny Boy.
No comments:
Post a Comment