Ofisi ya Rais, tume ya mipango imepongezwa kwa hatua kubwa iliyopiga katika kutekeleza majukumu mbalimbli ya kitaifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango lililofanyikia mjini Kibaha mwishoni mwa juma.
Mheshimiwa Ndikilo alieleza kuwa Tume ya mipango imepiga hatua kubwa katika kutekeleza majukumu yake ambayo ni pamoja na kutayarisha mpango wa taifa wa kila mwaka, kusambaza machapisho mbalimbali ya Tume ya Mipango, Kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya taifa, na kufanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano (2011/12-2015/16).
Pamoja na mafanikio makubwa katika kutekeleza majukumu ya Tume, Mkuu wa Mkoa alieleza kufurahishwa kwake na ufanisi wa viongozi pamoja na watumishi wa Tume ya Mipango kwa kuandaa mwongozo wa usimamizi wa uwekezaji wa umma, “ninaipongeza tume ya mipango kwa kundaa mwongozo wa usimamizi wa uwekezaji wa umma (Public Investment Management Manual), pamoja na kukamilisha tafiti mbalimbali zinazoharakisha mendeleo ya uchumi wa nchi yetu na mahitaji ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Mendeleo 2025.”
Vilevile uongozi wa Tume ya mipango umepongezwa kwa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake wa kada mbalimbali kwa kuwapeleka mfunzo ya muda mrefu na mfupi, semina na warsha zinazofanyika ndani na nje ya nchi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku.
Aidha Mheshimiwa Ndikilo amesisitiza wajumbe wa baraza hilo kuwaelimisha watumishi wenzao juu ya umuhimu wa kila mfanyakazi kutimiza wajibu wake katika sehemu ya kazi ili kufikia malengo ya pamoja baina ya mwajiri na watumishi.
“Pamoja na mambo mengine Baraza linawajibu wa kuishauri Tume kwa lengo la kuleta tija na mshikamano baina ya mtumishi na mwajiri, si jambo la busara kwa watumishi kutumia muda mwingi katika kudai maslahi zaidi kuliko kupima kiwango cha utekelezaji wa wajibu wao,” alisisitiza mhandisi Ndikilo.
Awali, Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, alieleza kuwa katika mkutano huo wajumbe watapata fursa kujadili mada nne amabazo ni mpango wa makisio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2015/16, Elimu ya jinsia mahala pa kazi, utekelezaji wa sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 na kanuni zake za mwaka 2013, na haki na wajibu wa mwajiriwa mahala pa kazi. Lengo la mada hizo ni kutoa fursa kwa watumishi kujifunza zaidi ili kuweza kuboresha utendaji wao wa kazi ili kufikia lengo la Tume ya mipango la kukuza uchumi wa Taifa.
Mkutano huo wa siku mbili unaozingatia mwongozo wa Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Baraza hilo limehudhuriwa na wakuu wote wa Klasta, Idara na vitengo, wajumbe wa TUGHE Taifa, TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya TUGHE tawi la Tume ya Mipango, pamoja na mjumbe mmoja mmoja kutoka klasta, Idara na Vitengo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akihutubia wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, ambapo alionesha kuridhishwa na viongozi na wafanyakazi wa Ofisi hiyo kwa weledi wao katika kutekeleza majukumu ya Taifa.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akisisitiza juu ya umuhimu wa wafanyakazi kuzingatia maadili sehemu za kazi. Kushoto ni Mwenyekeiti wa Baraza hilo Bibi Florence Mwanri na kulia ni Katibu wa Baraza hilo Bw. Senya Robert.
Mjumbe wa Baraza, Bw. Maduka Kessy, ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia Sekta za Uzalishaji akiwa anachangia mjadala wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi.
Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Mhandisi Happiness Mgalula (kulia), ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji, anayesimamia Klasta ya Miundombinu na Huduma akiwa na Bw. E. Maina (kushoto) ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wakiwa kwenye hali ya utulivu wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi.
Mjumbe Zena Hussein akijadili mada katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi. Wa kwanza kulia (mwenye shati ya mikono mirefu) ni Bw. Omary Abdallah ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mipango na Usimamizi, akifuatiwa na Bw. Dunstan Nyeme ambaye pia ni Kaimu Mhasibu mkuu, na kulia ni mjumbe Bw. S. Fisoo
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakiwa wanafuatilia kwa makini mada zinazotolewa wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakati mjini kibaha.
Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi, Bibi Florence Mwanri (katikati) pamoja na Katibu wa Baraza hilo, Bw. Senya Robert (Kulia), na Katibu msaidizi, Bibi Rukia Abel (kushoto) wakichukua maoni ya wajumbe katika mjadala wa kikao hicho.
Muwakilishi kutoka TUGHE Taifa Bw. Hassan Kaumo akichangia mada wakati wa mjadala ndani ya kikao, pembeni yake ni mwakilishi wa TUGHE mkoa wa Dar es Salaam Bw. Gaudensi Kadyango.
Mjumbe wa baraza bibi Mary Mwangisa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, akichangia mjadala wakati wa majadiliano ya wajumbe ndani ya mkutano.
Picha ya Pamoja ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi Ofisi ya Raisi, Tume ya Mipango wakiwa pamoja na Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.
No comments:
Post a Comment