Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha TLP , Augustine Mrema
Dar es Salaam. Mwasisi wa chama cha TLP, Stanley Ndamugoba amemburuza mahakamani Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Augustine Mrema akidai si kiongozi halali.
Kesi hiyo ya madai namba 33/2015 ilifunguliwa na Ndamugoba Ijumaa iliyopita katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam ikiambatanishwa na hati ya usikilizwaji wa haraka.
Katika kesi hiyo ambayo Baraza la Wadhamini limeunganishwa kama mdaiwa wa pili, Ndamugoba ameiomba mahakama itamke uongozi wa Mrema ulifikia kikomo mwaka mmoja uliopita. Mdai anaiomba mahakama kuu itamke kuwa kwa vile muda wake wa uongozi ulimalizika mwaka mmoja uliopita, Mrema hana mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu wa uchaguzi.
Ndamugoba mwenyewe alilithibitishia gazeti hili jana kufungua kesi hiyo akisema leo atakwenda Mahakama Kuu ili kuchukua samansi za kumuita Mrema shaurini pamoja na Baraza la Wadhamini.
“Ni kweli nimefungua kesi na nafikiri kesho (leo) samansi zitatoka,” alisema.
Hata hivyo Mrema alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu kuwapo kwa kesi hiyo, alisema yeye hakujiongezea muda kwa nguvu bali katiba ya TLP ndiyo ilimwongezea muda huo.
“Mimi sikujiongezea muda kwa nguvu wala sikuongezewa na mtu yeyote. Sisi tunafuata katiba ya TLP. Tatizo hapa ninaloliona ni vita ya ubunge Jimbo la Vunjo,” alisema Mrema.
Mrema alifafanua kuwa kamati kuu iliyopita, ilifanya uamuzi na kumpitisha yeye kuwa mgombea ubunge Jimbo la Vunjo na mgombea pekee wa nafasi ya uenyekiti wa TLP Taifa.
Bila kutaja kifungu cha katiba, Mrema alisema halmashauri kuu ya TLP imetoa madaraka kwa kamati kuu kufanya kazi kwa niaba yake na mkutano mkuu wa TLP.
“Katiba iko wazi kwamba endapo kuna mazingira yatajitokeza, kamati kuu imepewa mamlaka ya kufanya kazi za halmashauri kuu na mkutano mkuu na uamuzi huu ulifikiwa 2007,” alisema. “Tulitumia kipengele hicho kusogeza mbele mkutano mkuu wa uchaguzi kwa mwaka mmoja na tumeshatangaza mkutano mkuu wa uchaguzi utafanyika Aprili 23, mwaka huu,” alisisitiza.
Mrema alisema maelezo hayo ndiyo ambayo waliyatoa pia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi baada ya baadhi ya wanachama kulalamika na huo ndiyo msimamo wa kikatiba.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment