Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Bibi Pavu Juma, katika tukio hilo vijana waliokuwa katika gari eneo la Fuoni Taveta visiwani humo, wakiwa na mapanga, nondo na mawe walianza kuwarushia mawe wafuasi wa CUF waliokuwa kwenye magari wakitokea katika mkutano wa hadhara, Makunduchi na kuwajeruhi vibaya wafuasi 25 wa chama hicho.
“Baadhi ya majeruhi wamepata majeraha makubwa na wamelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, na wengine wamesafirishwa hadi Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,” alikaririwa Pavu.
Kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wafuasi wa chama chake kutolipiza kisasi.
Maalim Seif aliyazungumza hayo hivi karibuni baada ya kuwatembelea na kuwafariji baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Wakati wa ziara hiyo, Maalim Seif alisema watu waliowajeruhi wafuasi wa CUF wamefanya hivyo baada ya chama chao kukosa sera za kuwaeleza wananchi na sasa wameamua kufanya hujuma ambazo amesema hazitawasaidia.
“Natoa wito na kuwataka wanachama na wafuasi wa CUF wawe watulivu, chama chetu kinafuatilia kwa karibu hujuma zote zinazofanywa dhidi yetu hasa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
“CUF inalitaka jeshi la polisi kutodharau hujuma zinazofanywa dhidi yake hivyo lifuatilie kwa kina na kubaini njama za upangaji wa mipango ya hujuma kwa kuwachukulia hatua za kisheria bila ya kujali cheo cha yeyote miongoni mwao wale wote wanaochochea na kushabikia dhuluma za aina hii kwa wananchi,” alisema Maalim Seif.
Kabla ya kutokea kwa tukio hilo, akihutubia katika mkutano wa hadhara, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alitahadharisha kuwa kuna taarifa za uhakika zilizoletwa uwanjani hapo kuwa kuna mpango ulioandaliwa wa kuwadhuru kwa kuwashambulia wananchi waliohudhuria mkutano huo na kulitaka jeshi la polisi kuhakikisha ulinzi katika maeneo yote ili kudhibiti na kuzima mpango huo.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CUF, Salim Bimani alisema licha ya tahadhari hizo zilizotolewa mapema, jeshi la polisi lilishindwa kutoa ushirikiano kwa kuwapatia wananchi hao ulinzi hali iliyosababisha msafara uliokuwa ukitoka katika mkutano huo kuvamiwa, na wafuasi wa CUF kupigwa na kujeruhiwa vibaya.
Wakati hayo yakitokea, juzi Jumanne, hali ya hewa katika Baraza la Wawakilishi ilichafuka wakati wawakilishi hao walipokuwa wakichangia hoja binafsi iliyotolewa na mwakilishi wa Ole (CUF), Hamad Masoud Hamad na kusababisha wafuasi wa vyama vya CUF na CCM vyenye nguvu visiwani humo, kutaka kuzichapa kavukavu.
Kufuatia vurugu hizo, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alilazimika kuahirisha baraza lakini wawakilishi hao waliendelea kulumbana hadi nje ya ukumbi, huku mara kwa mara wakitaka kuvaana mwilini, hadi jeshi la polisi lilipoingilia kati na kuweka mambo sawa.
Tukio hilo ni la pili kutokea ndani ya kipindi cha wiki mbili, ambapo uhasimu kati ya CCM na CUF umeendelea kupamba moto, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Hali hiyo inawatia wasiwasi wananchi na kuwakumbusha matukio yaliyowahi kutingisha visiwani humo, yaliyotokea Januari 26 na 27, 2001 ambapo polisi walizuia maandamano ya wana CUF na kusababisha mauaji makubwa ambayo yalitokana na mgongano wa vyama hivyo viwili ambapo baadaye serikali ilipiga marufuku mikutano ya hadhara.
“Yarabi toba tumuombe Mungu atuepushie na haya yanayoendelea, hatutaki kupoteza ndugu zetu kwa sababu za kisiasa, tunaiomba serikali itulinde jamani,” alikaririwa Mahmoud Omary, mkazi wa Forodhani aliyezungumza na Uwazi Mizengwe
GPL
No comments:
Post a Comment