ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 28, 2015

MAMBO 15 YATAKAYOTULETEA VURUGU UCHAGUZI MKUU YASIPODHIBITIWA

Rais wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete akiwa Ikulu katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa siasa nchini.

Eric Shigongo

TUANZE makala haya kwa kumsifu Mungu aliye hai kwa kutupa uzima siku ya leo, hakika hakuna Mungu kama yeye.

Baada ya kusema hayo niseme kwamba mataifa mengi ya Kiafrika yamekuwa yakiingia katika vurugu na machafuko makubwa unapofika uchaguzi mkuu kwani wakati huo vyama vya upinzani huwa vinaomba ridhaa ya wananchi kuchaguliwa kushika dola, huku chama tawala kikiomba kuendelea kuongoza.

Watanzania tutaingia katika Uchaguzi mkuu mwaka huu Oktoba katika mazingira tofauti kabisa na chaguzi zilizopita kutokana na kuwepo na uelewa mkubwa wa mambo ya kisiasa kwa wananchi.

Nasema hivyo kwa sababu hadi sasa hoja nyingi zimeibuliwa bungeni na hata nje ya bunge na zitakuwa ni ajenda kwenye mikutano ya vyama vya siasa majukwaani kwa kuwa baadhi majibu yake ni magumu sana.

Moja ya hoja hizo ni suala la Katiba Mpya ya Tanzania kwani kuna ‘vita’ ya maneno kati ya maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba na kilichoandikwa na Bunge Maalum la Katiba katika Katiba Inayopendekezwa.

Pili, hatua walizochukuliwa watuhumiwa wa ufisadi wa Escrow na wezi wengine wa mali za umma, tatu, suala la uandikishwaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura na hata sifa za wagombea wa urais, ubunge na udiwani.

Kuna hoja pia ya wapinzani kuungana kupitia Ukawa huku kukiwepo na msuguano ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM kuhusu makundi na kuanzishwa chama kipya cha ACT- Wazalendo na Zitto Zuberi Kabwe ambacho mengi yamesemwa kuhusu chama hicho.

Yatakayovuruga uchaguzi mkuu yasipoangaliwa mwaka huu yapo mengi.

Mambo hayo ni kutofanyika kwa marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi kwa lengo la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, matokeo ya rais kuhojiwa mahakamani na kuruhusiwa kwa wagombea binafsi.

Lakini pia suala la jeshi letu la polisi kutumia nguvu kubwa kupita kiasi kukabiliana hasa na vyama vya upinzani wakati wa mikutano yao ya kampeni itakapoanza kunaweza kusababisha tatizo.

Jeshi la polisi lisipokuwa huru, matumizi mabaya ya makundi ya ulinzi ya vyama yasipodhibitiwa, chama tawala kikiendela kutumia vyombo vya serikali katika kampeni zake, tutakuwa tunapandikiza vurugu.

Miaka yote Tume ya Uchaguzi hutumia wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi, hili ni tatizo kwa sababu kuna upande hauwaamini na kutotolewa kwa elimu ya kutosha ya wasimamizi wa uchaguzi kunaweza kusababisha vurugu.

Lakini hili la viongozi wa dini kufanya kampeni katika majumba ya ibada na watu waliotimiza umri wa kupiga kura kutoandikishwa katika daftari la wapiga kura likiwepo, ni tatizo tena zito.

Jambo lingine ni vituo vya kupigia kura kutoandaliwa vizuri, kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzia na pia wanasiasa kutohubiri amani wakati wa kampeni za uchaguzi, kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Vyombo vya habari pia vinaweza kuchochea vurugu kama visipofuata maadili, au vikihongwa na kutumiwa na baadhi ya wagombea au chama kimoja pekee na vyombo vya serikali vikitumika kufanya kampeni kunaweza kuzua vurugu nchini.

Ukweli ni kwamba Uchaguzi Mkuu 2015 unaweza kuwa wa amani na utulivu kama kila chombo kitatimiza wajibu wake.

Tume ikiwa huru, polisi wakiwa huru, wanasiasa na viongozi wa dini wakihubiri amani, sidhani kama tutakuwa na matatizo.

Lakini pia sheria za uchaguzi ambazo zinalalamikiwa, zikifanyiwa marekebisho na kama haki ikifuatwa katika kila hatua amani na utulivu itadumu.

Hakika uchaguzi siyo kazi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi pekee, ni ushirikiano wa wadau wote wa siasa na wananchi wa kawaida.

Tume ya Uchaguzi inatakiwa kutekeleza wajibu wao licha ya upungufu wa kisheria uliopo. Wadau wengine watekeleze wajibu wao ili uchaguzi uwe wa amani na utulivu vinashamiri wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Naungana na Watanzania wenzangu wanaopenda kuona uchaguzi mkuu mwaka huu unakuwa wa amani na utulivu, lakini ni jukumu la wadau wote kuondoa hofu iliyotanda kwamba huenda uchaguzi ukavurugika kama baadhi ya mambo yanayopaswa kufanyika, hayajafanyika, kila mdau au chombo cha serikali kihakikishe kinazingatia ushauri huu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

GPL

No comments: